Isaya 19

Isaya 19

Unabii kuhusu Misri

1Neno la unabii kuhusu Misri:

Tazama, Bwana amepanda juu ya wingu liendalo kwa haraka

naye anakuja Misri.

Sanamu za Misri zinatetemeka mbele yake,

nayo mioyo ya Wamisri inayeyuka ndani yao.

2“Nitamchochea Mmisri dhidi ya Mmisri,

ndugu atapigana dhidi ya ndugu,

jirani dhidi ya jirani,

mji dhidi ya mji,

ufalme dhidi ya ufalme.

3Wamisri watakufa moyo,

na nitaibatilisha mipango yao.

Watatafuta ushauri kwa sanamu na kwa roho za waliokufa,

kwa waaguzi na kwa wale waongeao na mizimu.

4Nitawatia Wamisri

mikononi mwa bwana mkatili

na mfalme mkali atawatawala,”

asema Bwana, Bwana wa majeshi.

5Maji ya mito yatakauka,

chini ya mto kutakauka kwa jua.

6Mifereji itanuka;

vijito vya Misri vitapungua

na kukauka.

Matete na nyasi vitanyauka,

7pia mimea iliyo kando ya Mto Naili,

pale mto unapomwaga maji baharini.

Kila shamba lililopandwa kando ya Mto Naili litakauka,

litapeperushwa na kutoweka kabisa.

8Wavuvi watalia na kuomboleza,

wote watupao ndoana katika Mto Naili,

na watupao nyavu katika maji

watadhoofika kwa majonzi.

9Wale watu wafanyao kazi ya kitani kilichochambuliwa watakata tamaa,

wafumaji wa kitani safi watavunjika moyo.

10Wafanyao kazi ya kufuma nguo watahuzunishwa,

nao vibarua wataugua moyoni.

11Maafisa wa Soani ni wapumbavu kabisa,

washauri wa Farao wenye busara wanatoa ushauri wa kijinga.

Unawezaje kumwambia Farao,

“Mimi ni mmoja wa watu wenye hekima,

mwanafunzi wa wafalme wa zamani”?

12Wako wapi sasa watu wako wenye hekima?

Wao wakuoneshe na kukufahamisha

ni nini Bwana wa majeshi

amepanga dhidi ya Misri.

13Maafisa wa Soani wamekuwa wapumbavu,

viongozi wa Memfisi wamedanganyika,

walio mawe ya pembe ya taifa lake

wameipotosha Misri.

14Bwana amewamwagia

roho ya kizunguzungu;

wanaifanya Misri iyumbayumbe

katika yale yote inayoyafanya,

kama vile mlevi ayumbayumbavyo

katika kutapika kwake.

15Misri haiwezi kufanya kitu chochote,

cha kichwa wala cha mkia,

cha tawi la mtende wala cha tete.

16Katika siku ile Wamisri watakuwa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu mbele ya mkono wa Bwana wa majeshi anaoinua dhidi yao.

17Nayo nchi ya Yuda itawatia hofu Wamisri, kila mmoja atakayetajiwa Yuda ataingiwa na hofu, kwa sababu ya kile ambacho Bwana wa majeshi anapanga dhidi yao.

18Katika siku hiyo miji mitano ya Misri, itazungumza lugha ya Kanaani, na kuapa kumtii Bwana wa majeshi. Mji mmoja utaitwa Mji wa Uharibifu.[#19:18 yaani Heliopoli ( Mji wa Jua )]

19Katika siku hiyo patakuwa na madhabahu ya Bwana katikati ya Misri na mnara wa kumbukumbu kwa Bwana kwenye mpaka wa Misri.

20Itakuwa alama na ushahidi kwa ajili ya Bwana wa majeshi katika nchi ya Misri. Watakapomlilia Bwana kwa sababu ya watesi wao, Mungu atawapelekea mwokozi na mtetezi, naye atawaokoa.

21Hivyo Bwana atajijulisha mwenyewe kwa Wamisri, nao katika siku hiyo watamkubali Bwana . Wataabudu kwa kumtolea dhabihu na sadaka za nafaka, watamwekea Bwana nadhiri na kuzitimiza.

22Bwana ataipiga Misri kwa tauni; atawapiga na kuwaponya. Watamgeukia Bwana , naye atayasikia maombi yao na kuwaponya.

23Katika siku hiyo kutakuwa na njia kuu kutoka Misri hadi Ashuru. Waashuru wataenda Misri, na Wamisri wataenda Ashuru. Wamisri na Waashuru wataabudu pamoja.

24Katika siku hiyo Israeli itakuwa ya tatu, pamoja na Misri na Ashuru, nao watakuwa baraka kwa dunia.

25Bwana wa majeshi atawabariki, akisema, “Baraka iwe kwa Misri watu wangu, kwa Ashuru kazi ya mikono yangu, na kwa Israeli urithi wangu.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.