Isaya 22

Isaya 22

Unabii kuhusu Yerusalemu

1Neno la unabii kuhusu Bonde la Maono:

Nini kinachokutaabisha sasa,

kwamba ninyi nyote mmepanda juu ya mapaa?

2Ewe mji uliojaa ghasia,

ewe mji wa makelele na sherehe!

Watu wenu waliokufa hawakuuawa kwa upanga,

wala hawakufa vitani.

3Viongozi wako wote wamekimbia pamoja,

wamekamatwa bila kutumia upinde.

Ninyi nyote mliokamatwa mlichukuliwa wafungwa pamoja,

mlikimbia wakati adui alipokuwa bado mbali.

4Kwa hiyo nilisema, “Geukia mbali nami,

niache nilie kwa uchungu.

Usijaribu kunifariji

juu ya maangamizi ya watu wangu.”

5Bwana, Bwana wa majeshi, anayo siku

ya ghasia, ya kukanyaga, na ya kuogofya

katika Bonde la Maono,

siku ya kuangusha kuta

na ya kupiga kelele hadi milimani.

6Elamu analichukua podo,

pamoja na waendesha magari ya vita na farasi.

Kiri anaifungua ngao.

7Mabonde yako yaliyo mazuri sana yamejaa magari ya vita,

nao wapanda farasi wamewekwa kwenye malango ya mji.

8Ulinzi wa Yuda umeondolewa.

Nawe ulitazama siku ile

silaha katika Jumba la Kifalme la Mwituni.

9Mkaona kuwa Mji wa Daudi

una matundu mengi katika ulinzi wake,

mkaweka akiba ya maji

kwenye Bwawa la Chini.

10Mlihesabu majengo katika Yerusalemu

nanyi mkabomoa nyumba ili kuimarisha ukuta.

11Mlijenga bwawa la maji katikati ya kuta mbili

kwa ajili ya maji ya Bwawa la Zamani,

lakini hamkumtazama Yule aliyelitengeneza,

au kuwa na heshima kwa Yule aliyeubuni tangu zamani za kale.

12Bwana, Bwana wa majeshi,

aliwaita siku ile

ili kulia na kuomboleza,

kungʼoa nywele zenu na kuvaa magunia.

13Lakini tazama, kuna furaha na sherehe,

kuchinja ngʼombe na kuchinja kondoo,

kula nyama na kunywa mvinyo!

Mnasema, “Tuleni na kunywa,

kwa kuwa kesho tutakufa!”

14Bwana wa majeshi amelifunua hili nikiwa ninasikia: Bwana, Bwana wa majeshi, asema: “Hadi siku ya kufa kwenu, dhambi hii haitafanyiwa upatanisho.”

15Hili ndilo Bwana, Bwana wa majeshi, asemalo:

“Nenda ukamwambie huyu wakili Shebna,

ambaye ni msimamizi wa jumba la kifalme:

16Unafanya nini hapa, na ni nani aliyekupa ruhusa

kujikatia kaburi lako mwenyewe,

ukichonga kaburi lako mahali palipo juu,

na kutoboa kwa patasi mahali pako pa kupumzikia katika mwamba?

17“Jihadhari, Bwana yu karibu kukukamata thabiti,

na kukutupa mbali, ewe mtu mwenye nguvu.

18Atakuvingirisha uwe kama mpira

na kukutupa katika nchi kubwa.

Huko ndiko utakakofia,

na huko ndiko magari yako ya vita ya fahari yatabakia,

na kuwa fedheha kwa nyumba ya bwana wako!

19Nitakuondoa kutoka kazi yako,

nawe utaondoshwa kutoka nafasi yako.

20“Katika siku ile, nitamwita mtumishi wangu, Eliakimu mwana wa Hilkia.

21Nitamvika joho lako, nami nitamfunga mshipi wako kiunoni mwake, na kumkabidhi mamlaka yako. Yeye atakuwa baba kwa wale wanaoishi Yerusalemu na kwa nyumba ya Yuda.

22Nitaweka begani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Kile afunguacho hakuna awezaye kufunga, na kile afungacho hakuna awezaye kufungua.

23Nitampigilia kama kigingi kilicho mahali palipo imara, naye atakuwa kiti cha heshima kwa ajili ya nyumba ya baba yake.

24Utukufu wote wa jamaa yake utakuwa juu yake: Wazao wa jamaa hiyo na machipukizi yake, vyombo vyake vyote vidogo, tangu bakuli hadi magudulia yote.”

25Bwana wa majeshi asema, “Katika siku ile, kigingi kilichopigiliwa mahali imara kitaachia njia. Kitakatwa, nacho kitaanguka na mzigo ulioningʼinia juu yake utaanguka chini.” Bwana amesema.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.