The chat will start when you send the first message.
1Katika siku ile,
Bwana ataadhibu kwa upanga wake,
upanga wake mkali, mkubwa na wenye nguvu;
ataadhibu Lewiathani yule nyoka apitaye kwa mwendo laini,
Lewiathani yule nyoka mwenye kujipinda;
atamuua yule mnyama mkubwa wa baharini.
2Katika siku ile:
“Imbeni kuhusu shamba la mizabibu lililozaa:
3Mimi, Bwana , ninalitunza,
ninalinywesha maji mfululizo.
Ninalichunga usiku na mchana
ili mtu yeyote asije akalidhuru.
4Mimi sijakasirika.
Laiti michongoma na miiba ingenikabili!
Ningepambana dhidi yake katika vita,
ningeichoma moto yote.
5Au niwaache waje kwangu kwa ajili ya kupata kimbilio,
wao na wafanye amani nami,
naam, wafanye amani nami.”
6Katika siku zijazo, Yakobo atatia mizizi,
Israeli atatoa chipukizi na kuchanua maua,
naye atajaza ulimwengu wote kwa matunda.
7Je, Bwana amempiga
vile alivyowapiga wale waliompiga?
Je, yeye ameuawa
vile walivyouawa wale waliomuua yeye?
8Kwa vita na kwa kumfukuza unapingana naye:
kwa mshindo wake mkali anamfukuza,
kama siku ile uvumapo upepo wa mashariki.
9Kwa hili, basi, hatia ya Yakobo itafanyiwa upatanisho,
nalo hili litakuwa matunda ya utimilizo wa kuondolewa kwa dhambi yake:
Wakati atayafanya mawe yote ya madhabahu
kuwa kama mawe ya chokaa yaliyopondwa vipande vipande,
hakuna nguzo za Ashera au madhabahu za kufukizia uvumba
zitakazobaki zimesimama.
10Mji wenye ngome umebaki ukiwa,
makazi yaliyotelekezwa, yaliyoachwa kama jangwa.
Huko ndama hulisha,
huko hujilaza,
wanakwanyua matawi yake.
11Wakati vijiti vyake vimekauka, huvunjwa
nao wanawake huja na kuwasha navyo moto.
Kwa kuwa hili ni taifa lisilo na ufahamu,
kwa hiyo yeye aliyewafanya hana huruma juu yao,
Muumba wao hawaoneshi fadhili.
12Katika siku ile Bwana atapura kutoka matiririko ya Mto Frati hadi Kijito cha Misri, nanyi ee Waisraeli, mtakusanywa mmoja mmoja.
13Katika siku ile tarumbeta kubwa italia. Wale waliokuwa wakiangamia katika nchi ya Ashuru, nao wale waliokuwa uhamishoni katika nchi ya Misri watakuja na kumwabudu Bwana katika mlima mtakatifu huko Yerusalemu.