Isaya 33

Isaya 33

Taabu na msaada

1Ole wako wewe, ee mharibu,

wewe ambaye hukuharibiwa!

Ole wako, ee msaliti,

wewe ambaye hukusalitiwa!

Utakapokwisha kuharibu,

utaharibiwa;

utakapokwisha kusaliti,

utasalitiwa.

2Ee Bwana , uturehemu,

tunakutamani.

Uwe nguvu yetu kila asubuhi

na wokovu wetu wakati wa taabu.

3Kwa ngurumo ya sauti yako, mataifa yanakimbia;

unapoinuka, mataifa hutawanyika.

4Mateka yenu, enyi mataifa, yamevunwa

kama wafanyavyo madumadu,

watu huvamia juu yake

kama kundi la nzige.

5Bwana ametukuka, kwa kuwa anakaa mahali palipoinuka,

ataijaza Sayuni kwa haki na uadilifu.

6Atakuwa msingi ulio imara kwa wakati wenu,

hazina ya wokovu tele, hekima na maarifa;

kumcha Bwana ni ufunguo wa hazina hii.

7Angalia, mashujaa wake wanapiga kelele barabarani,

wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.

8Njia kuu zimeachwa,

hakuna wasafiri barabarani.

Mkataba umevunjika,

mashahidi wake wamedharauliwa,

hakuna anayeheshimiwa.

9Ardhi inaomboleza na kuchakaa,[#33:9 au Ardhi inakauka]

Lebanoni imeaibika na kunyauka;

Sharoni ni kama Araba,

nayo Bashani na Karmeli

wanapukutisha majani yao.

10“Sasa nitainuka,” asema Bwana .

“Sasa nitatukuzwa;

sasa nitainuliwa juu.

11Mlichukua mimba ya makapi,

mkazaa mabua;

pumzi yenu ni moto unaowateketeza.

12Mataifa watachomwa wawe majivu;

kama vichaka vya miiba vilivyokatwa ndivyo watakavyochomwa.”

13Ninyi mlio mbali sana, sikieni lile nililofanya;

ninyi mlio karibu, tambueni uweza wangu!

14Wenye dhambi katika Sayuni wametiwa hofu,

kutetemeka kumewakumba wasiomcha Mungu:

“Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto ulao?

Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto unaowaka milele?”

15Yeye aendaye kwa uadilifu

na kusema lililo haki,

yeye anayekataa faida ipatikanayo kwa dhuluma

na kuizuia mikono yake isipokee rushwa,

yeye azuiaye masikio yake dhidi ya mashauri ya mauaji,

na yeye afumbaye macho yake yasitazame uovu:

16huyu ndiye mtu atakayeishi mahali pa juu,

ambaye kimbilio lake litakuwa ngome ya mlimani.

Atapewa mkate wake,

na maji yake hayatakoma.

17Macho yenu yatamwona mfalme katika uzuri wake

na kuiona nchi inayoenea mbali.

18Katika mawazo yenu mtaifikiria hofu iliyopita:

“Yuko wapi yule afisa mkuu?

Yuko wapi yule aliyechukua ushuru?

Yuko wapi afisa msimamizi wa minara?”

19Hutawaona tena wale watu wenye kiburi,

wale watu wenye usemi wa mafumbo,

wenye lugha ngeni, isiyoeleweka.

20Mtazame Sayuni, mji wa sikukuu zetu;

macho yenu yatauona Yerusalemu,

mahali pa amani pa kuishi, hema ambalo halitaondolewa,

nguzo zake hazitangʼolewa kamwe,

wala hakuna kamba yake yoyote itakayokatika.

21Huko Bwana atakuwa Mwenye Nguvu wetu.

Patakuwa kama mahali pa mito mipana na vijito.

Hakuna jahazi lenye makasia litakalopita huko,

wala hakuna meli yenye nguvu itakayopita huko.

22Kwa kuwa Bwana ni mwamuzi wetu,

Bwana ndiye mtoa sheria wetu,

Bwana ni mfalme wetu,

yeye ndiye atakayetuokoa.

23Kamba zenu za merikebu zimelegea:

Mlingoti haukusimama imara,

nalo tanga halikukunjuliwa.

Wingi wa mateka yatagawanywa,

hata yeye aliye mlemavu atachukua nyara.

24Hakuna yeyote aishiye Sayuni atakayesema,

“Mimi ni mgonjwa”;

nazo dhambi za wale wanaoishi humo

zitasamehewa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.