The chat will start when you send the first message.
1Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua na kupona kwake.
2Hezekia akawapokea wale wajumbe kwa furaha na kuwaonesha vitu vile vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha lote, na kila kitu kilichokuwa katika hazina yake. Hapakuwa na kitu katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonesha.
3Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?”
Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kwangu kutoka Babeli.”
4Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?”
Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu. Hakuna kitu katika hazina yangu ambacho sikuwaonesha.”
5Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Bwana wa majeshi:
6Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako la kifalme, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba hadi siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Bwana .
7Nao baadhi ya wazao wako, mwili wako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mbali, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”
8Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Bwana ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Kutakuwa amani na usalama wakati wa uhai wangu.”