Isaya 45

Isaya 45

Koreshi ni chombo cha Mungu

1“Hili ndilo asemalo Bwana kwa mpakwa mafuta wake,

Koreshi, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume

kutiisha mataifa mbele yake

na kuwavua wafalme silaha zao,

kufungua milango mbele yake

ili malango yasije yakafungwa:

2Nitaenda mbele yako

na kusawazisha milima;

nitavunjavunja malango ya shaba

na kukatakata mapingo ya chuma.

3Nitakupa hazina za gizani,

mali iliyofichwa mahali pa siri,

ili upate kujua kwamba Mimi ndimi Bwana ,

Mungu wa Israeli, akuitaye kwa jina lako.

4Kwa ajili ya Yakobo mtumishi wangu,

Israeli niliyemchagua,

nimekuita wewe kwa jina lako,

na kukupa jina la heshima,

ingawa wewe hunitambui.

5Mimi ndimi Bwana , wala hakuna mwingine,

zaidi yangu hakuna Mungu.

Nitakutia nguvu,

ingawa wewe hujanitambua,

6ili kutoka mawio ya jua

hadi machweo yake,

watu wapate kujua kwamba hakuna Mungu mwingine ila Mimi.

Mimi ndimi Bwana wala hakuna mwingine.

7Mimi ninaumba nuru na kuhuluku giza,

ninaleta mafanikio na kusababisha maafa.

Mimi, Bwana , huyatenda haya yote.

8“Enyi mbingu juu, nyesheni haki,

mawingu na yaidondoshe.

Dunia na ifunguke sana,

wokovu na uchipuke,

haki na ikue pamoja nao.

Mimi, Bwana , ndiye niliyeiumba.

9“Ole wake yeye ashindanaye na Muumba wake,

yeye ambaye ni kigae tu kati ya vigae juu ya ardhi.

Je, udongo wa kufinyangia humwambia mfinyanzi,

‘Unatengeneza nini wewe?’

Je, kazi yako husema,

‘Hana mikono’?

10Ole wake amwambiaye baba yake,

‘Umezaa nini?’

Au kumwambia mama yake,

‘Umezaa kitu gani?’

11“Hili ndilo asemalo Bwana ,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake:

Kuhusu mambo yatakayokuja,

je, unaniuliza habari za watoto wangu,

au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu?

12Mimi ndiye niliyeumba dunia

na kumuumba mwanadamu juu yake.

Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu,

nikayapanga majeshi yake yote ya angani.

13Mimi nitamwinua Koreshi katika haki yangu:

nitazinyoosha njia zake zote.

Yeye atajenga mji wangu upya,

na kuwaweka huru watu wangu walio uhamishoni,

lakini si kwa kulipiwa fedha wala kupewa zawadi,

asema Bwana wa majeshi.”

14Hili ndilo asemalo Bwana :

“Mazao ya Misri na bidhaa za Kushi,

nao wale Waseba warefu,

watakujia na kuwa wako,

watakujia wakijikokota nyuma yako,

watakujia wamefungwa minyororo.

Watasujudu mbele yako,

wakikusihi na kusema,

‘Hakika Mungu yu pamoja nawe,

wala hakuna mwingine;

hakuna Mungu mwingine.’ ”

15Hakika wewe u Mungu unayejificha,

Ee Mungu na Mwokozi wa Israeli.

16Wote watengenezao sanamu wataaibika na kutahayarika;

wataenda kutahayarika pamoja.

17Lakini Israeli ataokolewa na Bwana

kwa wokovu wa milele;

kamwe hutaaibika wala kutatahayarika,

milele yote.

18Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana ,

yeye aliyeumba mbingu,

ndiye Mungu;

yeye aliyeifanya dunia na kuiumba,

yeye ndiye aliiwekea misingi imara,

hakuiumba ili iwe tupu,

bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake.

Anasema:

“Mimi ndimi Bwana ,

wala hakuna mwingine.

19Sijasema sirini,

kutoka mahali fulani katika nchi ya giza;

sijawaambia wazao wa Yakobo,

‘Nitafuteni bure.’

Mimi, Bwana , nasema kweli;

ninatangaza lililo sahihi.

20“Kusanyikeni pamoja mje,

enyi wakimbizi kutoka mataifa.

Wale wabebao sanamu za mti ni watu wasio na akili,

wale waombao miungu isiyoweza kuokoa.

21Tangazeni litakalokuwepo, lisemeni hilo;

wao na wafanye shauri pamoja.

Ni nani aliyetangulia kusema hili tangu zamani,

aliyelitangaza tangu zamani za kale?

Je, haikuwa Mimi, Bwana ?

Wala hapana Mungu mwingine

zaidi yangu mimi,

Mungu mwenye haki na Mwokozi;

hapana mwingine ila mimi.

22“Nigeukieni mimi, nanyi mkaokolewe,

enyi miisho yote ya dunia;

kwa maana mimi ndimi Mungu,

wala hapana mwingine.

23Nimeapa kwa nafsi yangu,

kinywa changu kimenena katika uadilifu wote

neno ambalo halitatanguka:

Kila goti litapigwa mbele zangu,

kwangu mimi kila ulimi utaapa.

24Watasema kunihusu,

‘Katika Bwana peke yake

ndiko kuna haki na nguvu.’ ”

Wote ambao wamemkasirikia Mungu

watamjia yeye, nao watatahayarika.

25Lakini katika Bwana wazao wote wa Israeli

wataonekana wenye haki na watashangilia.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.