The chat will start when you send the first message.
1“Sikilizeni hili, ee nyumba ya Yakobo,
ninyi mnaoitwa kwa jina la Israeli,
na mnaotoka katika ukoo wa Yuda,
ninyi mnaoapa kwa jina la Bwana ,
mnaomwomba Mungu wa Israeli,
lakini si katika kweli au kwa haki;
2ninyi mnaojiita raia wa mji mtakatifu,
na kumtegemea Mungu wa Israeli,
Bwana wa majeshi ndilo jina lake:
3Nilitoa unabii mambo ya kwanza tangu zamani,
kinywa changu kiliyatangaza na kuyafanya yajulikane;
kisha ghafula nikayatenda, nayo yakatokea.
4Kwa kuwa nalijua jinsi ulivyokuwa mkaidi;
mishipa ya shingo yako ilikuwa chuma,
paji la uso wako lilikuwa shaba.
5Kwa hiyo nilikuambia mambo haya tangu zamani,
kabla hayajatokea nilikutangazia
ili usije ukasema,
‘Sanamu zangu zilifanya hayo;
sanamu yangu ya mti, na mungu wangu wa chuma aliyaamuru.’
6Umesikia mambo haya; yaangalie hayo yote.
Je, hutayakubali?
“Kuanzia sasa na kuendelea nitakueleza mambo mapya,
juu ya mambo yaliyofichika usiyoyajua.
7Yameumbwa sasa, wala si tangu zamani;
hukupata kuyasikia kabla ya siku ya leo.
Hivyo huwezi kusema,
‘Naam, niliyajua hayo.’
8Hujayasikia wala kuyaelewa,
tangu zamani sikio lako halikufunguka.
Ninafahamu vyema jinsi ulivyo mdanganyifu,
uliitwa mwasi tangu kuzaliwa kwako.
9Kwa ajili ya Jina langu mwenyewe
ninaichelewesha ghadhabu yangu,
kwa ajili ya sifa zangu nimeizuia isikupate,
ili nisije nikakukatilia mbali.
10Tazama, nimekusafisha, ingawa si kama fedha,
nimekujaribu katika tanuru la mateso.
11Kwa ajili yangu mwenyewe,
kwa ajili yangu mwenyewe, nafanya hili.
Jinsi gani niliache Jina langu lichafuliwe?
Sitautoa utukufu wangu kwa mwingine.
12“Ee Yakobo, nisikilize mimi,
Israeli, ambaye nimekuita:
Mimi ndiye;
mimi ndimi mwanzo na mwisho.
13Mkono wangu mwenyewe uliweka misingi ya dunia,
nao mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu;
niziitapo, zote husimama pamoja.
14“Kusanyikeni, ninyi nyote, msikilize:
Ni ipi miongoni mwa hizo sanamu
ambayo imetabiri vitu hivi?
Watu wa Bwana waliochaguliwa na kuungana
watatimiza kusudi lake dhidi ya Babeli;
mkono wa Mungu utakuwa dhidi ya Wakaldayo.
15Mimi, naam, Mimi, nimenena;
naam, nimemwita yeye.
Nitamleta,
naye atafanikiwa katika lile nililomtuma.
16“Nikaribieni na msikilize hili:
“Tangu tangazo la kwanza sikusema kwa siri;
wakati litokeapo, nitakuwako hapo.”
Sasa Bwana Mwenyezi amenituma,
kwa Roho wake.
17Hili ndilo asemalo Bwana ,
Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:
“Mimi ni Bwana , Mungu wako,
nikufundishaye ili upate faida,
nikuongozaye katika njia ikupasayo kuiendea.
18Laiti ungesikiliza kwa makini maagizo yangu,
amani yako ingekuwa kama mto,
haki yako kama mawimbi ya bahari.
19Wazao wako wangekuwa kama mchanga,
watoto wako kama chembe zake zisizohesabika;
kamwe jina lao lisingefutiliwa mbali,
wala kuangamizwa kutoka mbele zangu.”
20Tokeni huko Babeli,
kimbieni kutoka kwa Wakaldayo!
Tangazeni hili kwa kelele za shangwe
na kulihubiri.
Lipelekeni hadi miisho ya dunia;
semeni, “Bwana amemkomboa
mtumishi wake Yakobo.”
21Hawakuona kiu alipowaongoza kupita jangwani;
alifanya maji yatiririke kutoka mwamba kwa ajili yao;
akapasua mwamba
na maji yakatoka kwa nguvu.
22“Hakuna amani kwa waovu,” asema Bwana .