Isaya 59

Isaya 59

Dhambi, toba na ukombozi

1Hakika mkono wa Bwana si mfupi hata usiweze kuokoa,

wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia.

2Lakini maovu yenu yamewatenga

ninyi na Mungu wenu,

dhambi zenu zimewaficha ninyi uso wake,

ili asisikie.

3Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu,

na vidole vyenu kwa hatia.

Midomo yenu imenena uongo,

nazo ndimi zenu zimenongʼona mambo maovu.

4Hakuna hata mmoja anayedai kwa haki;

hakuna hata mmoja anayetetea kwa haki.

Wanategemea mabishano matupu na kusema uongo,

huchukua mimba ya magomvi na kuzaa uovu.

5Huangua mayai ya nyoka wenye sumu kali

na kutanda wavu wa buibui.

Yeyote alaye mayai yao atakufa,

nalo moja likianguliwa, nyoka hutoka humo.

6Utando wao wa buibui haufai kwa mavazi;

hawawezi kujifunika kwa kile walichokitengeneza.

Matendo yao ni matendo maovu,

vitendo vya jeuri vipo mikononi mwao.

7Miguu yao hukimbilia kwenye dhambi,

ni myepesi kumwaga damu isiyo na hatia.

Mawazo yao ni mawazo maovu;

uharibifu na maangamizi huonekana katika njia zao.

8Hawajui njia ya amani,

hakuna haki katika mapito yao.

Wameyageuza kuwa njia za upotovu,

hakuna apitaye njia hizo atakayeifahamu amani.

9Hivyo uadilifu uko mbali nasi,

nayo haki haitufikii.

Tunatazamia nuru, kumbe! Yote ni giza,

tunatazamia mwanga, lakini tunatembea katika giza nene.

10Tunapapasa ukuta kama vipofu,

tunapapasa katika njia zetu kama watu wasio na macho.

Adhuhuri tunajikwaa kama wakati wa gizagiza;

kati ya wenye nguvu, tuko kama wafu.

11Wote tunanguruma kama dubu;

tunalia kwa maombolezo kama hua.

Tunatafuta haki, kumbe hakuna kabisa;

tunatafuta wokovu, lakini uko mbali.

12Kwa sababu makosa yetu ni mengi machoni pako,

na dhambi zetu zinashuhudia dhidi yetu.

Makosa yetu yako pamoja nasi daima,

nasi tunayatambua maovu yetu:

13Uasi na udanganyifu dhidi ya Bwana ,

kumgeuzia Mungu wetu kisogo,

tukichochea udhalimu na maasi,

tukinena uongo ambao mioyo yetu imeuhifadhi.

14Hivyo uadilifu umerudishwa nyuma,

nayo haki inasimama mbali,

kweli imejikwaa njiani,

uaminifu hauwezi kuingia.

15Kweli haipatikani popote,

na yeyote aepukaye uovu huwa mawindo.

Bwana alitazama, naye akachukizwa

kwamba hapakuwa na haki.

16Aliona kuwa hapakuwa hata mtu mmoja,

akashangaa kwamba hapakuwa hata mtu mmoja wa kuingilia kati.

Hivyo mkono wake mwenyewe

ndio uliomfanyia wokovu,

nayo haki yake mwenyewe

ndiyo iliyomtegemeza.

17Alivaa haki kama dirii kifuani mwake,

na chapeo ya wokovu kichwani mwake,

alivaa mavazi ya kisasi

naye akajifunga wivu kama joho.

18Kulingana na kile walichokuwa wametenda,

ndivyo atakavyolipa

ghadhabu kwa watesi wake

na kisasi kwa adui zake,

atavilipa visiwa sawa na wanavyostahili.

19Kuanzia magharibi, watu wataliogopa jina la Bwana

na kuanzia mawio ya jua, watauheshimu utukufu wake.

Adui atakapokuja kama mafuriko,

Roho wa Bwana atainua kiwango dhidi yake na kumshinda.

20“Mkombozi atakuja Sayuni,

kwa wale wa Yakobo

wanaozitubu dhambi zao,”

asema Bwana .

21“Bali mimi, hili ndilo agano langu nao,” asema Bwana . “Roho wangu, aliye juu yenu, na maneno yangu niliyoyaweka vinywani vyenu, havitaondoka vinywani mwenu, wala kutoka vinywani mwa watoto wenu, wala kutoka vinywani mwa wazao wao, kuanzia sasa na hata milele,” asema Bwana .

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.