The chat will start when you send the first message.
1Hata hivyo, hakutakuwa huzuni tena kwa wale waliokuwa katika dhiki. Hapo awali aliidhili nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, lakini katika siku zijazo ataipa heshima Galilaya ya Mataifa, karibu na njia ya bahari, ngʼambo ya Yordani:
2Watu wanaotembea katika giza
wameona nuru kuu,
wale wanaoishi katika nchi ya uvuli wa mauti,
nuru imewazukia.
3Umelikuza taifa,
na kuzidisha furaha yao,
wanafurahia mbele zako,
kama watu wanavyofurahia wakati wa mavuno,
kama mashujaa wanavyofurahia
wakigawanya nyara.
4Kama vile siku ya kushindwa kwa Wamidiani,
umevunja nira iliyowalemea,
ile gongo mabegani mwao
na fimbo ya aliyewadhulumu.
5Kila kiatu cha shujaa kilichotumiwa vitani,
na kila vazi lililovingirishwa katika damu
vitawekwa kwa ajili ya kuchomwa,
vitakuwa kuni za kuwasha moto.
6Kwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa,
tumepewa mtoto wa kiume,
nao utawala utakuwa begani mwake.
Naye ataitwa
Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu,
Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.
7Kuongezeka kwa utawala wake na amani
hakutakuwa na mwisho.
Atatawala kwenye kiti cha utawala cha Daudi
na juu ya ufalme wake,
akiuthibitisha na kuutegemeza
kwa haki na kwa adili,
tangu wakati huo na hata milele.
Wivu wa Bwana wa majeshi
utatimiza haya.
8Bwana ametuma ujumbe dhidi ya Yakobo,
utamwangukia Israeli.
9Watu wote watajua hili:
Efraimu na wakazi wa Samaria,
wanaosema kwa kiburi
na majivuno ya mioyo,
10“Matofali yameanguka chini,
lakini tutajenga tena kwa mawe yaliyochongwa,
mikuyu imekatwa,
na tutapanda mierezi badala yake.”
11Lakini Bwana amemtia nguvu adui wa Resini dhidi yao
na kuchochea watesi wao.
12Waaramu kutoka upande wa mashariki
na Wafilisti kutoka upande wa magharibi
wameila Israeli kwa kinywa kilichopanuliwa.
Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,
mkono wake bado umeinuliwa juu.
13Lakini watu hawajamrudia yeye aliyewapiga,
wala hawajamtafuta Bwana wa majeshi.
14Kwa hiyo Bwana atakatilia mbali kutoka Israeli kichwa na mkia,
tawi la mtende na tete katika siku moja.
15Wazee na watu mashuhuri ndio vichwa,
nao manabii wanaofundisha uongo ndio mkia.
16Wale wanaowaongoza watu hawa wanawapotosha,
nao wale wanaoongozwa wamepotoka.
17Kwa hiyo Bwana hatawafurahia vijana,
wala hatawahurumia yatima na wajane,
kwa kuwa kila mmoja wao hamchi Mungu, nao ni waovu,
na kila kinywa kinanena upumbavu.
Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,
mkono wake bado umeinuliwa juu.
18Hakika uovu huwaka kama moto;
huteketeza michongoma na miiba,
huwasha moto vichaka vya msituni,
hujiviringisha kuelekea juu kama nguzo ya moshi.
19Kwa hasira ya Bwana wa majeshi
nchi itachomwa kwa moto,
nao watu watakuwa kuni za kuchochea moto.
Hakuna mtu atakayemhurumia ndugu yake.
20Upande wa kuume watakuwa wakitafuna,
lakini bado wataona njaa;
upande wa kushoto watakuwa wakila,
lakini hawatashiba.
Kila mmoja atajilisha kwa nyama ya uzao wake mwenyewe:
21Manase atamla Efraimu,
naye Efraimu atamla Manase;
nao pamoja watakuwa kinyume na Yuda.
Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,
mkono wake bado umeinuliwa juu.