Waamuzi 16

Waamuzi 16

Samsoni na Delila

1Siku moja Samsoni alienda Gaza, akamwona mwanamke kahaba, naye akaingia kwake.

2Watu wa Gaza wakaambiwa, “Samsoni amekuja huku!” Hivyo, wakapazingira mahali pale, nao wakamvizia usiku kucha penye lango la mji. Wakakaa kimya usiku kucha, wakiwaza, “Kutakapopambazuka, tutamuua.”

3Samsoni akalala tu hadi usiku wa manane. Akaamka, na kushika milango ya lango la mji, na miimo yake miwili, akaingʼoa pamoja na makomeo yake. Akaviweka mabegani mwake na kuvipeleka hadi kilele cha mlima unaokabili Hebroni.

4Baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika Bonde la Soreki aliyeitwa Delila.

5Viongozi wa Wafilisti wakamwendea yule mwanamke na kumwambia, “Mshawishi ili upate kujua siri ya nguvu zake zilizo nyingi na jinsi tutakavyoweza kumshinda ili tuweze kumfunga na kumtiisha. Kila mmoja wetu atakupa shekeli elfu moja na mia moja za fedha.”[#16:5 Shekeli 1,100 ni sawa na kilo 13.]

6Hivyo Delila akamwambia Samsoni, “Naomba uniambie siri ya hizi nguvu zako nyingi, na jinsi unavyoweza kufungwa ili kukutiisha.”

7Samsoni akamjibu, “Kama nikifungwa kwa kamba saba za upinde ambazo hazijakauka, hapo ndipo nitakapokuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.”

8Basi viongozi wa Wafilisti wakamletea yule mwanamke kamba saba za upinde ambazo hazijakauka, naye akamfunga Samsoni.

9Wakati watu wakiwa wanamvizia katika chumba cha ndani, yule mwanamke akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Lakini yeye akazikata zile kamba za upinde, kama vile uzi wa pamba unapoguswa na moto. Hivyo siri ya nguvu zake haikujulikana.

10Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Umenifanyia mzaha na kuniambia uongo. Tafadhali niambie unaweza kufungwa kwa kitu gani?”

11Akamwambia, “Kama nikifungwa kwa uthabiti kwa kamba mpya ambazo hazijatumika, basi nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.”

12Hivyo, Delila akachukua kamba mpya na kumfunga nazo. Kisha akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Wale watu waliokuwa wanamvizia walikuwa katika chumba cha ndani. Lakini akazikata zile kamba zilizokuwa zimefunga mikono yake kama nyuzi.

13Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Hata sasa umenifanyia mzaha na kuniambia uongo. Nieleze ni jinsi gani unavyoweza kufungwa.”

Samsoni akamwambia, “Kama ukivifuma hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu kwa nguo iliyo katika mtande, na kuukaza kwa msumari, ndipo nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.” Hivyo, Samsoni alipokuwa amelala, Delila akachukua vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake na kuvifuma pamoja na nguo kwenye mtande,

14na kuukaza kwa msumari.

Kisha akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Samsoni akaamka kutoka usingizini na kungʼoa msumari na mtande, pamoja na ile nguo.

15Ndipo Delila akamwambia, “Wawezaje kusema, ‘Nakupenda,’ wakati moyo wako haupo pamoja nami? Umenifanyia mzaha mara hizi tatu na hujaniambia siri ya hizi nguvu zako nyingi.”

16Hatimaye, baada ya kusumbuliwa kwa maneno kwa siku nyingi na kuudhiwa, roho yake ikataabika kiasi cha kufa.

17Hivyo, akamwambia yule mwanamke siri yake yote, akisema, “Wembe haujapita kamwe kichwani mwangu, kwa kuwa mimi ni Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yangu. Kama nywele za kichwa changu zikinyolewa, nguvu zangu zitanitoka, na nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote!”

18Delila alipoona kuwa amemweleza siri yake yote, akatuma ujumbe kwa viongozi wa Wafilisti na kusema, “Njooni tena mara nyingine, maana amenieleza siri yake yote.” Basi viongozi wa Wafilisti wakarudi kwa Delila, wakiwa na fedha mikononi mwao.

19Delila akamfanya alale usingizi magotini pake, akamwita mtu amnyoe vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake. Delila akaanza kumnyongʼonyesha Samsoni, nazo nguvu zake zikamtoka.

20Yule mwanamke akamwita, “Samsoni! Hao, Wafilisti wanakujia!”

Akaamka toka usingizini, akisema, “Nitatoka nje kama hapo awali; nitajinyoosha, niwe huru.” Lakini hakujua kwamba Bwana alikuwa amemwacha.

21Basi Wafilisti wakamkamata, wakamngʼoa macho yake, wakamteremsha hadi Gaza. Wakamfunga kwa pingu za shaba, wakamweka gerezani ili asage ngano.

22Wakati huo nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa.

Kifo cha Samsoni

23Basi viongozi wa Wafilisti wakakusanyika pamoja ili kutoa kafara kuu kwa mungu wao Dagoni, wakisherehekea na kusema, “Mungu wetu amemtia adui yetu Samsoni mikononi mwetu.”

24Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao, wakisema:

“Sasa mungu wetu amemtia adui yetu

mikononi mwetu,

yule aliyeharibu nchi yetu

na kuwaua watu wengi miongoni mwetu.”

25Mioyo yao ilipokuwa imefurahishwa, wakapaza sauti, wakisema, “Mleteni Samsoni aje ili atutumbuize.” Basi wakamleta Samsoni kutoka gerezani, naye akawatumbuiza.

Wakamsimamisha katikati ya nguzo mbili.

26Samsoni akamwambia mtumishi aliyeushika mkono wake, “Niweke mahali ambapo ninaweza kuzigusa nguzo ambazo zinategemeza jengo ili nipate kuziegemea.”

27Basi lile jengo lilikuwa na wanaume na wanawake wengi; viongozi wote wa Wafilisti walikuwa humo, na kwenye dari walikuwepo watu wapatao elfu tatu, wanaume kwa wanawake, wakimtazama Samsoni akiwatumbuiza.

28Ndipo Samsoni akamwomba Bwana , akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, unikumbuke. Ee Mungu, nakusihi ukanitie nguvu mara hii moja tu, ili kwa tendo hili nipate kulipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa sababu ya macho yangu mawili.”

29Ndipo Samsoni akazikaribia zile nguzo mbili za katikati zilizokuwa zimelisimamisha lile jengo. Akazishika moja kwa mkono wa kuume, na nyingine kwa mkono wa kushoto.

30Samsoni akasema, “Acha nife pamoja na Wafilisti!” Ndipo akazisukuma zile nguzo kwa nguvu zake zote, nalo jengo lile likaanguka juu ya viongozi na watu wote waliokuwamo ndani. Hivyo, akawaua watu wengi wakati wa kufa kwake kuliko siku za uhai wake.

31Basi ndugu zake na jamaa yote ya baba yake wakateremka kwenda kumchukua. Wakampandisha na kumzika kati ya Sora na Eshtaoli, kwenye kaburi la Manoa baba yake. Samsoni alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.