The chat will start when you send the first message.
1Basi Waefraimu wakamuuliza Gideoni, “Mbona umetutenda hivi? Kwa nini hukutuita ulipoenda kupigana na Wamidiani?” Wakamlaumu kwa ukali sana.
2Gideoni akawajibu, “Nilichofanya mimi ni nini kulinganisha na kile ninyi mlichofanya? Je, kuokoa masazo ya zabibu za Efraimu si bora kuliko mavuno kamili ya zabibu ya Abiezeri?
3Mungu amewatia Orebu na Zeebu, hao viongozi wa Wamidiani, mikononi mwenu. Je, mimi niliweza kufanya nini kulinganisha na mlichofanya ninyi?” Aliposema hili, hasira yao dhidi yake ikatulia.
4Gideoni pamoja na watu wake mia tatu, wakiwa wamechoka sana lakini bado wakiwafuatia, wakafika Yordani na kuuvuka.
5Akawaambia wanaume wa Sukothi, “Tafadhali lipatieni jeshi langu mikate, kwa maana wamechoka, nami ningali ninawafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani.”
6Lakini viongozi wa Sukothi wakasema, “Je, tayari umewakamata Zeba na Salmuna ili tulipatie jeshi lako mikate?”
7Gideoni akajibu, “Kwa ajili ya hilo tu, Bwana atakapowatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, nitaichana nyama ya miili yenu kwenye miiba ya nyikani na kwenye michongoma.”
8Kutoka hapo alikwea hadi Penieli na kutoa ombi lile lile, lakini nao wanaume wa Penieli wakamjibu kama wanaume wa Sukothi walivyokuwa wamemjibu.
9Hivyo akawaambia wanaume wa Penieli, “Nitakaporudi kwa ushindi, nitaubomoa mnara huu.”
10Wakati huu Zeba na Salmuna walikuwa Karkori, wakiwa na jeshi la watu wapatao elfu kumi na tano waliokuwa wamesalia wa mataifa ya mashariki, kwa kuwa watu wapatao elfu mia moja na ishirini wenye panga walikuwa wameuawa.
11Basi Gideoni akakwea kwa njia ya wafugaji wahamaji mashariki mwa Noba na Yogbeha, na kulishambulia jeshi ambalo halikushuku lolote.
12Zeba na Salmuna, hao wafalme wawili wa Midiani, wakakimbia lakini yeye Gideoni akawafuata na kuwakamata, akalishinda hilo jeshi lao lote kabisa.
13Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani kupitia Mwinuko wa Heresi.
14Akamkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumuuliza maswali, naye yule kijana akamwandikia majina ya viongozi sabini na saba wa Sukothi, ambao ni wazee wa mji.
15Ndipo Gideoni akaja na kuwaambia wanaume wa Sukothi, “Tazameni Zeba na Salmuna mlionisimanga kwa ajili yao mkisema, ‘Je, tayari umewakamata Zeba na Salmuna ili tulipatie jeshi lako mikate?’ ”
16Akawachukua hao wazee wa mji, na kuwaadhibu wanaume wa Sukothi kwa kuwachapa kwa miiba na michongoma ya nyikani.
17Pia akaubomoa mnara wa Penieli na kuwaua wanaume wa huo mji.
18Kisha akawauliza Zeba na Salmuna, “Ni wanaume wa aina gani mliowaua huko Tabori?”
Wakajibu, “Ni wanaume kama wewe, kila mmoja wao akiwa anafanana na mwana wa mfalme.”
19Gideoni akajibu, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu hasa. Hakika kama Bwana aishivyo, kama mngekuwa mmewaacha hai, mimi nisingewaua ninyi.”
20Akamgeukia Yetheri, mwanawe mzaliwa wa kwanza, akasema, “Waue hawa!” Lakini Yetheri hakuufuta upanga wake, kwa sababu aliogopa, kwa kuwa alikuwa bado kijana mdogo tu.
21Zeba na Salmuna wakasema, “Njoo ufanye hivyo wewe mwenyewe. ‘Alivyo mwanaume, ndivyo zilivyo nguvu zake.’ ” Hivyo, Gideoni akajitokeza na kuwaua, naye akayaondoa mapambo kwenye shingo za ngamia wao.
22Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Ututawale, wewe, mwanao, na mjukuu wako, kwa kuwa umetuokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani.”
23Lakini Gideoni akawaambia, “Mimi sitawatawala ninyi, wala mwanangu hatawatawala. Bwana ndiye atakayewatawala ninyi.”
24Naye akasema, “Ninalo ombi moja, kwamba kila mmoja wenu anipatie kipuli kutoka fungu lake la nyara.” (Ilikuwa desturi ya Waishmaeli kuvaa vipuli vya dhahabu.)
25Wakajibu, “Tutafurahi kuvitoa.” Hivyo wakatanda vazi chini na kila mwanaume akatupia juu yake pete kutoka fungu lake la nyara.
26Uzito wa pete za dhahabu alizoomba ulikuwa shekeli elfu moja na mia saba, bila kuhesabu mapambo mengine, vidani, na mavazi ya zambarau yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani, au mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia wao.[#8:26 Shekeli 1,700 ni sawa na kilo 19.5.]
27Gideoni akatengeneza kizibau kwa kutumia ile dhahabu, ambacho alikiweka katika mji wake, yaani Ofra. Waisraeli wote wakafanya uasherati kwa kukiabudu huko, nacho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake.
28Hivyo Midiani wakashindwa mbele ya Waisraeli, nao hawakuinua vichwa vyao tena. Wakati wa siku za uhai wa Gideoni, nchi ikafurahia amani miaka arobaini.
29Yerub-Baali mwana wa Yoashi akarudi kwenda kuishi katika nyumba yake.
30Alikuwa na wana sabini wa kwake mwenyewe, kwa kuwa alikuwa na wake wengi.
31Suria wake, aliyekuwa anaishi huko Shekemu, pia alimzalia mwana, akamwita jina Abimeleki.
32Gideoni mwana wa Yoashi akafa akiwa na umri mzuri wa uzee, akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake huko Ofra ya Waabiezeri.
33Mara tu alipofariki Gideoni, Waisraeli wakarudia hali ya uovu na kufanya uasherati kwa kuabudu Mabaali. Wakamsimamisha Baal-Berithi kuwa mungu wao na
34wala hawakumkumbuka Bwana Mungu wao, aliyewaokoa kutoka mikononi mwa adui zao wote kutoka kila upande.
35Pia wakashindwa kuitendea mema jamaa ya Yerub-Baali (yaani Gideoni) kwa ajili ya mambo yote mema aliyokuwa amefanyia Israeli.