The chat will start when you send the first message.
1Hili ndilo asemalo Bwana : “Nenda ukanunue gudulia la udongo kutoka kwa mfinyanzi. Wachukue baadhi ya wazee wa watu na wa makuhani
2na mtoke mwende hadi Bonde la Ben-Hinomu, karibu na ingilio la Lango la Vigae. Huko tangaza maneno ninayokuambia,
3nawe useme, ‘Sikieni neno la Bwana , enyi wafalme wa Yuda na watu wa Yerusalemu. Hili ndilo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo: Sikilizeni! Nitaleta maafa mahali hapa, ambayo yatafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yawashe.
4Kwa kuwa wameniacha na kupafanya mahali hapa kuwa pa miungu ya kigeni. Wamefukizia uvumba miungu ambayo wao, wala baba zao, wala wafalme wa Yuda kamwe hawakuijua, nao wamelijaza eneo hili kwa damu isiyo na hatia.
5Wamejenga mahali pa juu pa kuabudia pa Baali ili kuteketeza wana wao katika moto kuwa sadaka kwa Baali, kitu ambacho sikukiamuru wala kukitaja, wala hakikuingia akilini mwangu.
6Hivyo jihadharini, siku zinakuja, asema Bwana , wakati watu hawatapaita tena mahali hapa Tofethi ama Bonde la Ben-Hinomu, bali Bonde la Machinjo.
7“ ‘Nitaiharibu mipango ya Yuda na Yerusalemu mahali hapa. Nitawafanya waanguke kwa upanga mbele ya adui zao, katika mikono ya wale wanaotafuta uhai wao, nami nitaitoa mizoga yao kuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi.
8Nitauharibu mji huu na kuufanya kitu cha kutisha na cha kudharauliwa. Wote wapitao karibu watashangaa na kuudhihaki kwa sababu ya majeraha yake yote.
9Nitawafanya wao kula nyama ya wana wao wa kiume na wa kike; kila mmoja atakula nyama ya mwenzake wakati wa dhiki ya kuzingirwa na jeshi la adui wanaotafuta uhai wao.’
10“Kisha livunje lile gudulia wale walio pamoja nawe wakiwa wanaangalia,
11uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi: Nitalivunja taifa hili na mji huu kama gudulia hili la mfinyanzi lilivyovunjwa, nalo haliwezi kutengenezeka tena. Watawazika waliokufa huko Tofethi hata isiwepo nafasi zaidi.
12Hivi ndivyo nitakavyopafanya mahali hapa na kwa wale wanaoishi ndani yake, asema Bwana . Nitaufanya mji huu kama Tofethi.
13Nyumba zilizo Yerusalemu na zile za wafalme wa Yuda zitatiwa unajisi kama mahali hapa, Tofethi: yaani nyumba zote ambazo walifukiza uvumba juu ya mapaa yake kwa jeshi lote la angani, na kumimina dhabihu za vinywaji kwa miungu mingine.’ ”
14Kisha Yeremia akarudi kutoka Tofethi, mahali Bwana alikuwa amemtuma kutoa unabii, akasimama katika ua wa Hekalu la Bwana na kuwaambia watu wote,
15“Hili ndilo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya mji huu pamoja na vijiji vinavyouzunguka kila maafa niliyosema dhidi yake, kwa sababu wamekuwa na shingo ngumu, na hawakuyasikiliza maneno yangu.’ ”