Yeremia 24

Yeremia 24

Vikapu viwili vya tini

1Baada ya Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na maafisa, mafundi stadi na wahunzi wa Yuda, kuchukuliwa kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli na Nebukadneza, mfalme wa Babeli, Bwana akanionesha vikapu viwili vya tini vilivyowekwa mbele ya Hekalu la Bwana .[#24:1 au Konia ; pia anaitwa Yehoyakini]

2Kikapu kimoja kilikuwa na tini nzuri sana, kama zile za mavuno ya kwanza. Kikapu cha pili kilikuwa na tini dhaifu sana, mbovu mno zisizofaa kuliwa.

3Kisha Bwana akaniuliza, “Je, Yeremia, unaona nini?”

Nikamjibu, “Ninaona tini zilizo nzuri ni nzuri sana, lakini zilizo mbaya, ni mbaya sana zisizofaa kuliwa.”

4Kisha neno la Bwana likanijia:

5“Hili ndilo Bwana , Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kama zilivyo hizi tini nzuri, ndivyo ninavyowaona kuwa bora watu wa uhamisho kutoka Yuda, niliowaondoa kutoka mahali hapa kwenda katika nchi ya Wakaldayo.

6Macho yangu yatakuwa juu yao kwa ajili ya kuwapatia mema, nami nitawarudisha tena katika nchi hii. Nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawangʼoa,

7nitawapa moyo wa kunifahamu mimi, kwamba mimi ndimi Bwana . Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, kwa maana watanirudia kwa moyo wote.

8“ ‘Lakini kama zilivyo zile tini dhaifu, ambazo ni mbovu mno zisizofaa kuliwa,’ asema Bwana , ‘ndivyo nitakavyomtendea Sedekia mfalme wa Yuda, maafisa wake, na mabaki wengine kutoka Yerusalemu, wawe wamebaki katika nchi hii, au wanaishi Misri.

9Nitawafanya kuwa chukizo kabisa na kitu cha kulaumiwa katika mataifa yote ya dunia, watakuwa aibu na kitu cha kudharauliwa, chombo cha dhihaka na kulaaniwa, popote nitakapowafukuzia.

10Nitautuma upanga, njaa na tauni dhidi yao hadi wawe wameangamia kutoka nchi niliyowapa wao na baba zao.’ ”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.