The chat will start when you send the first message.
1Siku nyingine wana wa Mungu walienda kujionesha mbele za Bwana . Shetani naye akaja pamoja nao kujionesha mbele zake.
2Bwana akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?”
Shetani akamjibu Bwana , “Natoka kuzunguka duniani, nikitembea huku na huko.”
3Bwana akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, mtu asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Naye bado anadumisha uadilifu wake, ingawa ulinichochea dhidi yake, ili nimwangamize pasipo sababu.”
4Shetani akamjibu Bwana , “Ngozi kwa ngozi! Mwanadamu atatoa vyote alivyo navyo kwa ajili ya uhai wake.
5Lakini nyoosha mkono wako na kuipiga nyama yake na mifupa yake, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”
6Bwana akamwambia Shetani, “Vema sana; kwa hiyo, yeye yumo mikononi mwako, lakini lazima umwachie uhai wake.”
7Basi Shetani akatoka mbele za Bwana , naye akampiga Ayubu kwa majipu mabaya tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa.
8Ndipo Ayubu akachukua kigae na kujikuna nacho, huku akiketi kwenye majivu.
9Mke wake akamwambia, “Je, bado unashikamana na uadilifu wako? Mlaani Mungu nawe ukafe!”
10Akamjibu, “Unazungumza kama mwanamke mpumbavu. Je, tupokee mema kutoka kwa Mungu, bali tusipokee mabaya?”[#2:10 maana yake kupungukiwa maadili]
Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi katika kusema kwake.
11Basi rafiki watatu wa Ayubu, ndio Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi na Sofari Mnaamathi, waliposikia kuhusu taabu yote iliyompata Ayubu, wakajipanga kutoka nyumbani mwao, wakakutana ili kwenda kumtuliza katika taabu hiyo na kumfariji.
12Walipomwona kwa mbali, ilikuwa vigumu kumtambua. Wakaanza kulia kwa sauti kubwa, wakayararua majoho yao na kujirushia mavumbi juu ya vichwa vyao.
13Kisha wakaketi chini kwenye udongo pamoja na Ayubu kwa siku saba usiku na mchana. Hakuna yeyote aliyesema naye neno, kwa sababu waliona jinsi mateso yake yalivyokuwa makubwa.