Ayubu 24

Ayubu 24

Ayubu anaendelea

1“Kwa nini Mwenyezi asiweke nyakati kwa ajili ya hukumu?

Kwa nini wale wamjuao wazitafute siku kama hizo bila mafanikio?

2Watu husogeza mawe ya mpaka;

huchunga makundi ya wanyama waliyonyangʼanya kwa nguvu.

3Huwanyangʼanya yatima punda wao,

na kumchukua rehani fahali wa mjane.

4Humsukuma mhitaji kutoka njia,

na kuwafanya maskini wote wa nchi kulazimika kujificha.

5Kama punda-mwitu jangwani,

maskini huzunguka katika kazi zao za kutafuta chakula;

mahali palipo jangwa

huwapa chakula cha watoto wao.

6Hukusanya chakula mashambani na kuokota masazo

katika mashamba ya mizabibu ya waovu.

7Kwa kukosa nguo, usiku kucha hukaa uchi;

hawana chochote cha kujifunika baridi.

8Hutota kwa mvua za mlimani,

nao huikumbatia miamba kwa ajili ya kukosa pa kujisitiri.

9Mtoto yatima hupokonywa matitini;

mtoto mchanga wa maskini hunyakuliwa kwa ajili ya deni.

10Kwa kukosa nguo, hutembea uchi;

hubeba miganda ya ngano, lakini huwa na njaa.

11Hukamua zeituni katika mawe ya kusagia;

hukanyaga mashinikizo, lakini wanaona kiu.

12Kilio cha huzuni cha wanaokufa kinapaa kutoka mjini,

nazo nafsi za waliojeruhiwa zinalilia msaada.

Lakini Mungu hamlaumu mtu yeyote

kwa kutenda mabaya.

13“Wako wale wanaoiasi nuru,

wasiofahamu njia zake

wala hawakai katika mapito yake.

14Mwanga wa mchana unapotoweka, muuaji huinuka,

naye huwaua maskini na mhitaji;

wakati wa usiku hunyemelea kama mwizi.

15Jicho la mzinzi hungojea wakati wa giza,

naye hufikiri, ‘Hakuna jicho litakaloniona,’

naye huuficha uso wake.

16Katika giza, huvunja nyumba,

lakini wakati wa mchana hujifungia ndani;

hawataki kufanya lolote nuruni.

17Kwa wote hawa, giza nene ndiyo asubuhi yao;

hujifanya rafiki na vitisho vya gizani.

18“Lakini wao ni povu juu ya maji;

sehemu yao juu ya nchi imelaaniwa,

hivyo hakuna hata mmoja

aendaye kwenye shamba la mizabibu.

19Kama vile joto na hari vinyakuavyo theluji iliyoyeyuka,

ndivyo Kuzimu kuwanyakuavyo waliotenda dhambi.

20Tumbo lililowazaa huwasahau,

nao huwa karamu ya mabuu;

watu waovu hawakumbukwi tena,

lakini huvunjika kama mti.

21Huwafanya mawindo wanawake tasa na wasio na watoto,

nao hawaoneshi huruma kwa wajane.

22Lakini Mungu huwakokota wenye nguvu kwa uwezo wake;

ingawa wamestawi, hawana hakika ya maisha.

23Aweza akawaacha wakapumzika wakijihisi salama,

lakini macho yake yanaona njia zao.

24Kwa kitambo kidogo hutukuka,

hatimaye hutoweka;

hushushwa na kukusanywa

kama wengine wote;

hukatwa kama masuke ya nafaka.

25“Kama hili sivyo, ni nani awezaye

kunithibitisha kuwa mwongo,

na kuyafanya maneno yangu

kuwa si kitu?”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.