Yoshua 10

Yoshua 10

Jua lasimama

1Baada ya haya Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu alisikia kuwa Yoshua alikuwa ameteka mji wa Ai na kuuangamiza kabisa, tena alikuwa ameua mfalme wake, kama alivyofanya huko Yeriko na mfalme wake, tena ya kuwa watu wa Gibeoni walikuwa wamefanya mapatano ya amani na Waisraeli, na walikuwa wakiishi karibu yao.

2Yeye na watu wake wakataharuki mno kwa kuwa Gibeoni ulikuwa mji mkubwa kama mmoja wa miji ya kifalme; ulikuwa mkubwa kuliko Ai, na watu wake wote walikuwa mashujaa wa vita.

3Hivyo Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu akaomba msaada kwa Hohamu mfalme wa Hebroni, Piramu mfalme wa Yarmuthi, Yafia mfalme wa Lakishi, na Debiri mfalme wa Egloni.

4Akawaambia, “Njooni mnisaidie kuipiga Gibeoni, kwa sababu imefanya mkataba wa amani na Yoshua na Waisraeli.”

5Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, ambao ni wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni, wakaunganisha majeshi yao. Wakapanda na vikosi vyao vyote, nao wakajipanga dhidi ya Gibeoni na kuishambulia.

6Nao Wagibeoni wakatuma ujumbe kwa Yoshua kwenye kambi ya Gilgali na kumwambia, “Usiwatelekeze watumishi wako. Panda haraka uje kwetu utuokoe! Tusaidie, kwa sababu wafalme wote wa Waamori wanaokaa nchi ya vilima wameunganisha majeshi yao pamoja dhidi yetu.”

7Basi Yoshua akaondoka Gilgali pamoja na jeshi lake lote, wakiwepo mashujaa wote.

8Bwana akamwambia Yoshua, “Usiwaogope watu hao, nimewatia mkononi mwako. Hakuna yeyote atakayeweza kushindana nawe.”

9Baada ya Yoshua kutembea usiku kucha kutoka Gilgali, akawashambulia ghafula.

10Bwana akawafadhaisha mbele ya Waisraeli, naye Yoshua na Waisraeli wakawashinda kwa ushindi mkuu huko Gibeoni. Waisraeli wakawafukuza kwa njia inayopanda kwenda Beth-Horoni, huku wakiwaua hadi kufikia Azeka na Makeda.

11Walipokuwa wanawakimbia Waisraeli kwenye barabara inayoteremka kutoka Beth-Horoni hadi Azeka, Bwana akawavurumishia mawe makubwa kama mvua kutoka mbinguni, na wengi wao walikufa kwa mawe kuliko wale waliokufa kwa panga za Waisraeli.

12Siku ile Bwana alipowakabidhi Waamori kwa Waisraeli, Yoshua akanena na Bwana akiwa mbele ya Waisraeli, akasema:

“Wewe jua, simama juu ya Gibeoni,

wewe mwezi, tulia juu ya Bonde la Aiyaloni.”

13Hivyo jua likasimama,

nao mwezi ukatulia,

hadi taifa hilo lilipokwisha

kujilipizia kisasi kwa adui zake,

kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yashari.

Jua likasimama katikati ya mbingu, likachelewa kuzama muda wa siku nzima.

14Hakujakuwa na siku nyingine kama hiyo kabla au baada, siku ambayo Bwana alimsikiliza mwanadamu. Hakika Bwana alikuwa akiwapigania Israeli.

15Ndipo Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Israeli yote.

Wafalme watano wa Waamori wauawa

16Basi wale wafalme watano wakawa wamekimbia kujificha kwenye pango huko Makeda.

17Yoshua alipoambiwa kuwa wafalme hao watano wamekutwa wakiwa wamejificha ndani ya pango huko Makeda,

18akasema, “Vingirisheni mawe makubwa kwenye mlango wa pango, tena mweke walinzi wa kulilinda.

19Lakini msiwaache! Wafuatieni adui zenu, washambulieni kutoka nyuma, wala msiwaache wafike kwenye miji yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu amewatia mkononi mwenu.”

20Hivyo Yoshua pamoja na Waisraeli wakawaangamiza, isipokuwa wachache waliosalia walifika kwenye miji yao yenye ngome.

21Basi jeshi lote likarudi salama kwa Yoshua kule kambini Makeda, na hakuna yeyote aliyetoa neno kinyume cha Waisraeli.

22Ndipo Yoshua akasema, “Haya fungueni mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano.”

23Kwa hiyo wakawatoa hao wafalme watano nje ya pango: wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni.

24Walipokuwa wamewaleta hawa wafalme kwa Yoshua, akawaita wanaume wote wa Israeli, na kuwaambia majemadari wa vita walioenda pamoja naye, “Njooni hapa mweke nyayo zenu juu ya shingo za hawa wafalme.” Basi wakaja wakaweka nyayo zao shingoni.

25Yoshua akawaambia, “Msiogope, wala msivunjike moyo. Kuweni hodari na wenye ushujaa. Hili ndilo Bwana atakalowatendea adui zenu wote mnaoenda kupigana nao.”

26Ndipo Yoshua akawapiga na kuwaua wale wafalme na kuwatundika juu ya miti mitano, nao wakaachwa wakiningʼinia juu ya ile miti hadi jioni.

27Wakati wa kuzama jua Yoshua akaamuru, nao wakawashusha kutoka ile miti na kuwatupa kwenye lile pango ambalo walikuwa wamejificha. Wakaweka mawe makubwa kwenye mlango wa pango, ambayo yapo hadi leo.

28Siku ile Yoshua akateka Makeda. Akamuua kila mmoja katika ule mji, pamoja na mfalme wake kwa upanga. Hakubakiza mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Makeda kama vile alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.

Israeli yaangamiza miji ya kusini

29Ndipo Yoshua akaondoka Makeda akiwa pamoja na Israeli yote hadi mji wa Libna na kuushambulia.

30Bwana pia akautia huo mji wa Libna pamoja na mfalme wake mikononi mwa Israeli. Yoshua akaangamiza ule mji na kila mtu aliyekuwa ndani yake kwa upanga. Hakubakiza huko mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Libna kama alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.

31Kisha Yoshua akaondoka Libna kwenda Lakishi akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia.

32Bwana akautia Lakishi mikononi mwa Israeli, hivyo Yoshua akauteka siku ya pili. Yoshua akauangamiza mji na kila kilichokuwa ndani yake kwa upanga, kama tu vile alivyokuwa ameufanyia mji wa Libna.

33Wakati huo huo, Horamu mfalme wa Gezeri alikuwa amepanda ili kusaidia Lakishi, lakini Yoshua akamshinda pamoja na jeshi lake, hadi hapakubakia mtu yeyote.

34Ndipo Yoshua akaondoka Lakishi kwenda Egloni akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia.

35Wakauteka mji huo siku ile ile, wakaupiga kwa upanga na kumwangamiza kila mmoja aliyekuwa ndani yake, kama vile walivyokuwa wameufanyia Lakishi.

36Kisha Yoshua na Waisraeli wote wakapanda kutoka Egloni hadi Hebroni, na kuushambulia.

37Wakauteka mji na kuupiga kwa upanga, pamoja na mfalme wake, vijiji vyake na kila mmoja aliyekuwa ndani yake. Hawakubakiza mtu yeyote. Kama vile huko Egloni, waliuangamiza kabisa pamoja na kila mmoja aliyekuwa ndani yake.

38Ndipo Yoshua na Waisraeli wote wakageuka na kushambulia Debiri.

39Wakauteka mji, mfalme wake na vijiji vyake, na kuupiga kwa upanga. Kila mmoja aliyekuwa ndani yake wakamwangamiza kabisa. Hawakubakiza mtu yeyote. Wakaufanyia Debiri na mfalme wake kama vile walivyokuwa wameifanyia miji ya Libna na Hebroni na wafalme wao.

40Hivyo Yoshua akalishinda eneo hilo lote, ikiwa ni pamoja na nchi ya vilima, na Negebu, na Shefela, miteremko ya milima, pamoja na wafalme wake wote. Hakubakiza mtu yeyote. Akaangamiza kabisa kila kitu chenye pumzi, kama vile Bwana , Mungu wa Israeli, alivyokuwa ameamuru.[#10:40 au upande wa magharibi chini ya vilima]

41Yoshua akawashinda kuanzia Kadesh-Barnea hadi Gaza na kutoka eneo lote la Gosheni hadi Gibeoni.

42Wafalme hawa wote pamoja na nchi zao Yoshua aliwashinda kwa wakati mmoja, kwa sababu Bwana , Mungu wa Israeli, aliwapigania Israeli.

43Ndipo Yoshua akarudi pamoja na Israeli yote kwenye kambi huko Gilgali.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.