Yoshua 3

Yoshua 3

Kuvuka Yordani

1Yoshua na Waisraeli wote wakaondoka asubuhi na mapema kutoka Shitimu, wakaenda hadi Mto Yordani, ambako walipiga kambi kabla ya kuvuka.

2Baada ya siku tatu maafisa wakapita katika kambi yote,

3wakitoa maagizo kwa watu, wakiwaambia: “Mtakapoona Sanduku la Agano la Bwana Mungu wenu, likichukuliwa na Walawi ambao ndio makuhani, mtaondoka hapo mlipo na kulifuata.

4Ndipo mtakapotambua njia mtakayoiendea, kwa kuwa hamjawahi kuipita kabla. Lakini msisogee karibu, bali kuwe na umbali wa dhiraa elfu mbili kati yenu na Sanduku.”[#3:4 Dhiraa 2,000 ni sawa na mita 900.]

5Ndipo Yoshua akawaambia hao watu, “Jitakaseni, kwa kuwa kesho Bwana atatenda mambo ya kushangaza kati yenu.”

6Yoshua akawaambia makuhani, “Liinueni Sanduku la Agano mkatangulie mbele ya watu.” Hivyo wakaliinua na kutangulia mbele yao.

7Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Leo nitaanza kukutukuza machoni pa Israeli yote, ili wapate kujua kuwa niko pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Musa.

8Uwaambie makuhani wanaochukua Sanduku la Agano, ‘Mnapofika kwenye ukingo wa maji ya Yordani, nendeni mkasimame ndani ya mto.’ ”

9Yoshua akawaambia Waisraeli, “Njooni hapa msikilize maneno ya Bwana Mungu wenu.

10Hivi ndivyo mtakavyojua kuwa Mungu aliye hai yupo kati yenu, na kwamba kwa hakika atawaondoa mbele yenu hao Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi.

11Tazameni, Sanduku la Agano la Bwana wa dunia yote litaingia ndani ya Mto Yordani likiwa limewatangulia.

12Sasa basi, chagueni watu kumi na wawili kutoka makabila ya Israeli, mtu mmoja kutoka kila kabila.

13Mara tu nyayo za makuhani walichukualo Sanduku la Bwana , Bwana wa dunia yote, zitakapokanyaga ndani ya Mto Yordani, maji hayo yanayotiririka kutoka juu yatatindika na kusimama kama chuguu.”

14Basi, watu walipovunja kambi ili kuvuka Yordani, makuhani wakiwa wamebeba Sanduku la Agano waliwatangulia.

15Wakati huu ulikuwa wakati wa mavuno, nao Mto Yordani ulikuwa umefurika hadi kwenye kingo zake. Ilikuwa kawaida ya Yordani kufurika nyakati zote za mavuno. Mara tu makuhani wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Agano walipofika mtoni na nyayo zao kuzama ndani ya yale maji,

16maji hayo yaliyotiririka kutoka upande wa juu yaliacha kutiririka yakasimama kama chuguu mbali kabisa nao, kwenye mji ulioitwa Adamu kwenye eneo la Sarethani, wakati yale maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), yalitindika kabisa. Hivyo watu wakavuka kukabili Yeriko.

17Wale makuhani waliobeba Sanduku la Agano la Bwana , wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Mto Yordani, wakati Waisraeli wote wakiwa wanapita hadi taifa lote likaisha kuvuka mahali pakavu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.