The chat will start when you send the first message.
1Bwana akawaambia Musa na Haruni,
2“Iwapo mtu yeyote atakuwa na uvimbe, au upele, au alama nyeupe juu ya ngozi yake, ambayo yaweza kuwa ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, ni lazima aletwe kwa kuhani Haruni, au kwa mmoja wa wanawe, hao makuhani.[#13:2 yaani ukoma ; ni neno lililotumika kueleza magonjwa mbalimbali ya ngozi, ambayo si lazima yawe ni ukoma halisi (pia 13:47)]
3Kuhani atachunguza hicho kidonda kilichopo juu ya ngozi yake, na kama nywele za mahali palipo na kidonda zimebadilika kuwa nyeupe, na ikiwa kidonda kimeingia ndani ya ngozi, basi ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, yaani ukoma. Kuhani atakapomchunguza, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi.
4Kama alama juu ya ngozi yake ni nyeupe, lakini haionekani kuingia ndani ya ngozi, na nywele kwenye alama hiyo hazijageuka kuwa nyeupe, kuhani atamtenga mtu aliyeambukizwa kwa siku saba.
5Siku ya saba, kuhani atamchunguza, na kama hakuona badiliko kwenye kile kidonda na hakijaenea juu ya ngozi, atamtenga kwa siku nyingine saba.
6Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama kidonda kimepungua na hakijaenea juu ya ngozi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa ni safi; ni upele tu. Ni lazima mtu huyo afue mavazi yake, naye atakuwa safi.
7Lakini ikiwa ule upele utaenea katika ngozi yake baada ya yeye kujionesha kwa kuhani na kutangazwa kuwa safi, ni lazima aende tena kwa kuhani.
8Kuhani atamchunguza, na kama upele umeenea kwenye ngozi, atamtangaza kuwa najisi, kwani ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
9“Wakati mtu yeyote ana ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, ni lazima aletwe kwa kuhani.
10Kuhani atamchunguza na kama kuna uvimbe mweupe katika ngozi ambao umefanya nywele kuwa nyeupe, na kama kuna nyama mbichi ndani ya uvimbe,
11ni ugonjwa sugu wa ngozi, na kuhani atamtangaza kuwa najisi. Hatamtenga tena kwa sababu ni najisi tayari.
12“Ikiwa ugonjwa utakuwa umeenea kwenye ngozi yake yote kwa kadiri kuhani atakavyoweza kuona, kwamba umeenea kwenye ngozi yote ya huyo mgonjwa kutoka kichwani hadi wayo,
13kuhani atamchunguza, na kama ugonjwa umeenea mwili mzima, atamtangaza huyo mtu kuwa safi. Kwa kuwa mwili wote umekuwa mweupe, yeye ni safi.
14Lakini itokeapo nyama mbichi kwenye ngozi yake, atakuwa najisi.
15Kuhani atakapoiona hiyo nyama mbichi, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Hiyo nyama mbichi ni najisi, ana ugonjwa wa kuambukiza.
16Hiyo nyama mbichi ikigeuka na kuwa nyeupe, ni lazima amwendee kuhani.
17Kuhani atamchunguza, na kama vidonda vimekuwa vyeupe, kuhani atamtangaza mgonjwa huyo kuwa safi; kisha atakuwa safi.
18“Wakati mtu ana jipu juu ya ngozi yake nalo likapona,
19napo mahali palipokuwa na jipu pakatokea uvimbe mweupe, au alama yenye wekundu na weupe, ni lazima akajioneshe kwa kuhani.
20Kuhani atapachunguza, na kama uvimbe umeingia ndani ya ngozi, na nywele zimegeuka kuwa nyeupe, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza uliojitokeza pale jipu lilipokuwa.
21Lakini ikiwa kuhani anapopachunguza pakawa hapana nywele nyeupe ndani yake, wala hapakuingia ndani ya ngozi, na pameanza kupungua, basi kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku saba.
22Kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
23Lakini ikiwa ile alama haijabadilika wala kuenea, ni kovu tu kutokana na jipu, kuhani atamtangaza kuwa safi.
24“Wakati mtu ameungua kwenye ngozi yake, pakatokea alama yenye wekundu na weupe, au alama nyeupe ikaonekana penye nyama mbichi pale palipoungua,
25kuhani ataichunguza ile alama, na kama nywele zilizo juu yake zimegeuka kuwa nyeupe, na panaonekana kuingia ndani ya ngozi, basi huo ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza ambao umetokea katika jeraha la moto. Kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
26Lakini kuhani akipachunguza na akaona kwamba hakuna nywele nyeupe kwenye alama ile, wala hapakuingia ndani ya ngozi, na pamepungua, basi kuhani atamtenga kwa siku saba.
27Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
28Lakini, kama alama ile haikubadilika na wala haijaenea kwenye ngozi, napo pamepungua, ni uvimbe kutokana na jeraha la moto, na kuhani atamtangaza kuwa safi; ni kovu tu kutokana na kuungua.
29“Ikiwa mwanaume au mwanamke ana kidonda juu ya kichwa au juu ya kidevu,
30kuhani atakichunguza kile kidonda, na kama ataona kuwa kimeingia ndani ya ngozi, na nywele zilizo juu yake ni njano na nyembamba, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza wa kichwa au kidevu.
31Lakini kama kuhani akichunguza aina hii ya kidonda, kionekane kuwa hakijaingia ndani ya ngozi, na hakuna nywele nyeusi juu yake, basi atamtenga mtu huyo kwa siku saba.
32Siku ya saba kuhani atachunguza kidonda kile, na kama hakijaenea, na hakuna nywele za manjano juu yake, wala haukuingia ndani ya ngozi,
33mtu huyo ni lazima anyolewe, isipokuwa mahali palipo na ugonjwa, naye kuhani atamtenga kwa siku nyingine saba.
34Siku ya saba kuhani atachunguza tena kidonda kile; ikiwa hakijaenea kwenye ngozi na hakikuingia ndani ya ngozi, kuhani atamtangaza kuwa safi. Lazima afue nguo zake, naye atakuwa safi.
35Lakini ikiwa kidonda kitaenea katika ngozi baada ya kutangazwa kuwa safi,
36kuhani atamchunguza, na kama kidonda kimeenea kwenye ngozi, kuhani hana haja ya kutazama kama kuna nywele za manjano; mtu huyo ni najisi.
37Hata hivyo, katika uchunguzi wake akiona hapajabadilika, na nywele nyeusi zimeota juu yake, huyo mtu amepona. Yeye si najisi; kuhani atamtangaza kuwa safi.
38“Ikiwa mwanaume au mwanamke ana alama nyeupe juu ya ngozi yake,
39kuhani atamchunguza, na kama alama hizo zina weupe uliofifia, ni vipele visivyo na madhara vilivyojitokeza kwenye ngozi; mtu huyo ni safi.
40“Wakati mwanaume hana nywele naye ana upara, yeye ni safi.
41Ikiwa hana nywele kwenye ngozi ya kichwa chake, na ana upara kwenye paji, ni safi.
42Lakini kama ana kidonda chenye wekundu na weupe kwenye kichwa chake chenye upara, au kwenye paji la uso, ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza unaojitokeza kichwani au kwenye paji lake la uso.
43Kuhani atamchunguza, na kama kidonda kilichovimba juu ya kichwa chake au kwenye paji la uso ni chekundu au cheupe kama ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza,
44mtu huyo ni mgonjwa, na ni najisi. Kuhani atamtangaza kuwa najisi kwa sababu ya kidonda kwenye kichwa chake.
45“Mtu mwenye ugonjwa kama huo wa kuambukiza ni lazima avae nguo zilizoraruka, awachilie nywele zake bila kuzichana, afunike sehemu ya chini ya uso wake, na apige kelele, ‘Najisi! Najisi!’
46Kwa muda wote atakaokuwa na ugonjwa huo wa kuambukiza atabaki kuwa najisi. Ni lazima aishi peke yake; ni lazima aishi nje ya kambi.
47“Kuhusu vazi lolote lililoharibiwa na maambukizo ya ukoma, liwe ni vazi la sufu au kitani,
48vazi lolote lililofumwa au kusokotwa la kitani au sufu, ngozi yoyote au chochote kilichotengenezwa kwa ngozi:
49ikiwa maambukizo kwenye vazi, ngozi, au vazi lililofumwa au kusokotwa la kitani au sufu, au kitu chochote cha ngozi, ni rangi ya kijani au nyekundu, huo ni ukoma unaoenea, na ni lazima kuhani aoneshwe.
50Kuhani atachunguza ukoma huo na kulitenga vazi hilo kwa siku saba.
51Siku ya saba atalichunguza, na kama ukoma umeenea kwenye vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, au ngozi, kwa vyovyote vile itumikavyo, ni ukoma wa kuangamiza; vazi hilo ni najisi.
52Ni lazima achome vazi hilo, liwe ni la sufu au kitani kilichofumwa au kusokotwa, au kitu chochote cha ngozi chenye maambukizo; kwa kuwa ni ukoma wa kuangamiza, vazi lote ni lazima lichomwe moto.
53“Lakini kuhani akilichunguza na akaona kuwa ule ukoma haujaenea kwenye vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, au kitu cha ngozi,
54ataagiza kwamba vazi lenye maambukizo lisafishwe. Kisha atalitenga kwa siku nyingine saba.
55Baada ya vazi lenye maambukizo kusafishwa, kuhani atalichunguza, na kama ukoma haujaonesha badiliko lolote, hata kama haujaenea, ni najisi. Lichome kwa moto, iwe ukoma umeenea upande mmoja au mwingine.
56Kama kuhani ataona kuwa ile alama imefifia baada ya kuoshwa, basi atararua sehemu iliyoambukizwa ya vazi, au ngozi, au vazi lililofumwa au kusokotwa.
57Lakini ikijitokeza tena kwenye vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, ama kitu cha ngozi, ule ni ukoma unaoenea; chochote chenye ukoma ni lazima kichomwe kwa moto.
58Vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, au kitu chochote cha ngozi, baada ya kusafishwa na kuondolewa ukoma, ni lazima lioshwe tena, ili liwe safi.”
59Haya ndio masharti kuhusu maambukizo ya ukoma kwenye mavazi ya sufu au kitani, mavazi yaliyofumwa au kusokotwa, ama kitu chochote cha ngozi, kwa ajili ya kuvitangaza kuwa safi au najisi.