The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Musa,
2“Waletee Haruni na wanawe mavazi yao, mafuta ya upako, fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kondoo dume wawili na kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu.
3Kisha kusanya watu wote kwenye ingilio la Hema la Kukutania.”
4Musa akafanya kama Bwana alivyomwagiza, na watu wakakusanyika kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
5Musa akawaambia kusanyiko, “Hili ndilo Bwana ameagiza lifanyike.”
6Kisha Musa akamleta Haruni na wanawe mbele, akawaosha kwa maji.
7Akamvika Haruni koti, akamfunga mshipi, akamvika joho, na kumvalisha kizibau. Pia akamfunga hicho kizibau kiunoni mwake kwa mshipi uliofumwa kwa ustadi.
8Akaweka kifuko cha kifuani juu yake, na kuweka Urimu na Thumimu kwenye hicho kifuko.[#8:8 Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha.]
9Kisha akamvika Haruni kilemba kichwani pake, akaweka lile bamba la dhahabu, lile taji takatifu, upande wa mbele wa kilemba, kama Bwana alivyomwagiza Musa.
10Kisha Musa akachukua mafuta ya upako, na kuipaka maskani ya Mungu na kila kitu kilichokuwamo; hivyo akaviweka wakfu.
11Akanyunyiza sehemu ya mafuta juu ya madhabahu mara saba, akaipaka madhabahu mafuta na vyombo vyake vyote, pamoja na sinia na kinara chake, ili kuviweka wakfu.
12Akamimina sehemu ya hayo mafuta ya upako kichwani mwa Haruni, akampaka mafuta ili kumweka wakfu.
13Kisha akawaleta wana wa Haruni mbele, akawavika makoti, akawafunga mishipi na kuwavika vilemba, kama Bwana alivyomwagiza Musa.
14Kisha akamtoa fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, nao Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake.
15Musa akamchinja yule fahali na akachukua sehemu ya hiyo damu, kisha kwa kidole chake akaitia kwenye pembe zote za madhabahu ili kutakasa madhabahu. Akaimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Kwa hiyo akayaweka wakfu ili kufanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu.
16Pia Musa akachukua mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani, na kipande kirefu cha ini, na figo zote mbili pamoja na mafuta yake, akayateketeza juu ya madhabahu.
17Lakini fahali, ikiwa pamoja na ngozi yake na nyama yake na sehemu zake za ndani na matumbo, akaiteketeza nje ya kambi, kama Bwana alivyomwagiza Musa.
18Kisha Musa akamleta kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, naye Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake.
19Ndipo Musa akamchinja yule kondoo dume na kunyunyiza damu yake pande zote za madhabahu.
20Musa akamkata yule kondoo dume vipande vipande na kukiteketeza kichwa, vile vipande na yale mafuta.
21Kisha akamsafisha sehemu za ndani na miguu kwa maji, na kumteketeza yule kondoo dume mzima juu ya madhabahu kuwa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto, kama Bwana alivyomwagiza Musa.
22Kisha Musa akamleta yule kondoo dume wa pili, ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu, naye Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake.
23Musa akamchinja yule kondoo dume, akaichukua sehemu ya damu yake na kuipaka juu ya ncha ya sikio la kuume la Haruni, na juu ya kidole gumba cha mkono wake wa kuume na juu ya kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
24Pia Musa akawaleta hao wana wa Haruni mbele, akaipaka sehemu ya hiyo damu kwenye ncha za masikio yao ya kuume, juu ya vidole gumba vya mikono yao ya kuume, na juu ya vidole vikubwa vya miguu yao ya kuume. Kisha akanyunyiza damu pande zote za madhabahu.
25Akachukua mafuta ya mnyama, mafuta ya mkia, mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani, kipande kirefu cha ini, figo zote mbili pamoja na mafuta yake, na paja la kulia.
26Kisha kutoka kwa kikapu cha mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichokuwa mbele za Bwana , akachukua andazi moja, na jingine lililotengenezwa kwa mafuta, na mkate mwembamba; akaviweka hivi vyote juu ya mafungu ya mafuta ya mnyama, na juu ya lile paja la kulia.
27Akaviweka hivi vyote mikononi mwa Haruni na wanawe, na kuviinua mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa.
28Kisha Musa akavichukua kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kuwa sadaka ya kuwekwa wakfu, harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto.
29Kisha akachukua kidari, kilicho fungu la Musa la kondoo dume kwa ajili ya kuwekwa wakfu, na kukiinua mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa, kama Bwana alivyomwagiza Musa.
30Kisha Musa akachukua sehemu ya mafuta ya upako, na sehemu ya damu kutoka madhabahu, na kuvinyunyiza juu ya Haruni na mavazi yake, na juu ya wanawe na mavazi yao. Kwa hiyo akamweka Haruni na mavazi yake wakfu, pamoja na wanawe na mavazi yao.
31Kisha Musa akamwambia Haruni na wanawe, “Pikeni hiyo nyama kwenye ingilio la Hema la Kukutania, na muile hapo pamoja na mkate kutoka kikapu cha sadaka ya kuweka wakfu, kama nilivyoagiza: ‘Haruni na wanawe wataila.’
32Kisha mteketeze nyama na mikate iliyobaki.
33Msitoke kwenye ingilio la Hema la Kukutania kwa muda wa siku saba, hadi siku zenu za kuwekwa wakfu ziwe zimetimia, kwa kuwa muda wenu wa kuwekwa wakfu utakuwa siku saba.
34Lile lililofanyika leo liliagizwa na Bwana ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
35Lazima mkae kwenye ingilio la Hema la Kukutania usiku na mchana kwa siku saba, na kufanya lile Bwana analolitaka, ili msife; kwa kuwa hilo ndilo nililoamriwa.”
36Kwa hiyo Haruni na wanawe wakafanya kila kitu Bwana alichoamuru kupitia kwa Musa.