Luka 1

Luka 1

Utangulizi; kuzaliwa kwa Yesu na ujana wake

Utangulizi

1Kwa kuwa watu wengi wamekaa ili kuandika habari za mambo yaliyotimizwa katikati yetu,

2kama vile yalivyokabidhiwa kwetu na wale waliokuwa mashahidi walioyaona na watumishi wa lile neno tokea mwanzo,

3mimi nami baada ya kuchunguza kila kitu kwa uangalifu kuanzia mwanzo, niliamua kukuandikia habari za mambo hayo, ewe mtukufu Theofilo,

4ili upate kujua ukweli kuhusu yale uliyofundishwa.

Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji kwatabiriwa

5Wakati wa utawala wa Herode mfalme wa Yudea, palikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, aliyekuwa wa ukoo wa kikuhani wa Abiya. Elizabeti mkewe alikuwa pia mzao wa Haruni.

6Zakaria na Elizabeti mkewe wote walikuwa watu wanyofu mbele za Mungu, wakizishika amri zote za Bwana na maagizo yote bila lawama.

7Lakini walikuwa hawana watoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa; nao wote wawili walikuwa wazee sana.

8Siku moja ilipokuwa zamu ya kikundi cha Zakaria, yeye akifanya kazi ya ukuhani Hekaluni mbele za Mungu,

9alichaguliwa kwa kura kwa kufuata desturi za ukuhani, kuingia Hekaluni mwa Bwana ili kufukiza uvumba.

10Nao wakati wa kufukiza uvumba ulipowadia, wale wote waliokuwa wamekusanyika ili kuabudu walikuwa nje wakiomba.

11Ndipo malaika wa Bwana, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zakaria.

12Zakaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana, akajawa na hofu.

13Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina Yohana.

14Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.

15Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake.

16Naye atawageuza wengi wa Waisraeli warudi kwa Bwana Mungu wao.

17Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao, na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki, ili kuwaweka tayari watu walioandaliwa kwa ajili ya Bwana.”

18Zakaria akamuuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.”

19Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema.

20Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.”

21Wakati huo watu walikuwa wanamngojea Zakaria nje huku wakishangaa kukawia kwake mle Hekaluni.

22Alipotoka akawa hawezi kusema nao, wao wakatambua kuwa ameona maono ndani ya Hekalu. Lakini kwa kuwa alikuwa bubu, akawa anawaashiria kwa mikono.

23Muda wake wa kuhudumu Hekaluni ulipomalizika, akarudi nyumbani mwake.

24Baada ya muda usio mrefu, Elizabeti mkewe akapata mimba, naye akajitenga kwa miezi mitano.

25Elizabeti akasema, “Hili ndilo Bwana alilonitendea aliponipa kibali na kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.”

Kuzaliwa kwa Yesu kwatabiriwa

26Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti,

27kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yusufu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Mariamu.

28Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!”

29Mariamu akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni salamu hii ni ya namna gani.

30Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Mariamu; umepata kibali kwa Mungu.

31Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto wa kiume na utamwita jina Yesu.

32Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. Bwana Mungu atampa kiti cha utawala cha Daudi baba yake.

33Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”

34Mariamu akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”

35Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu.

36Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa.

37Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”

38Mariamu akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha.

Mariamu aenda kumtembelea Elizabeti

39Wakati huo Mariamu akajiandaa, akaharakisha kwenda katika mji mmoja kwenye nchi ya vilima ya Yudea.

40Akaingia nyumbani mwa Zakaria na kumsalimu Elizabeti.

41Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Mariamu, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu,

42akapaza sauti kwa nguvu, akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa.

43Lakini ni kwa nini mimi nimepata kibali kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?

44Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliye tumboni mwangu aliruka kwa furaha.

45Amebarikiwa yeye aliyeamini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.”

Wimbo wa Mariamu

46Naye Mariamu akasema:

“Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,

47nayo roho yangu inamfurahia

Mungu Mwokozi wangu,

48kwa kuwa ameangalia kwa fadhili

unyonge wa mtumishi wake.

Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa,

49kwa maana yeye Mwenye Nguvu

amenitendea mambo ya ajabu:

jina lake ni takatifu.

50Rehema zake hudumu kizazi hadi kizazi,

kwa wale wanaomcha.

51Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake;

amewatawanya wale wenye kiburi

ndani ya mioyo yao.

52Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya utawala,

lakini amewainua wanyenyekevu.

53Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri,

bali matajiri amewafukuza mikono mitupu.

54Amemsaidia mtumishi wake Israeli,

kwa kukumbuka ahadi yake ya kumrehemu

55Abrahamu na uzao wake milele,

kama alivyowaahidi baba zetu.”

56Mariamu akakaa na Elizabeti karibu miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani mwake.

Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji

57Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume.

58Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Bwana alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye.

59Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zakaria, ambalo ndilo jina la baba yake.

60Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yohana.”

61Wakamwambia, “Hakuna mtu yeyote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.”

62Basi wakamfanyia Zakaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani.

63Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yohana.”

64Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kuongea, huku akimsifu Mungu.

65Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu, na katika nchi yote ya vilima ya Yudea watu walikuwa wakinena kuhusu mambo haya yote.

66Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.

Unabii wa Zakaria

67Zakaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu, naye akatoa unabii, akisema:

68“Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,

kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.

69Naye ametusimamishia pembe ya wokovu[#1:69 inamaanisha nguvu]

katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,

70(kama alivyonena kwa vinywa vya manabii wake

watakatifu tangu zamani),

71kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu,

na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:

72ili kuonesha rehema kwa baba zetu

na kukumbuka agano lake takatifu,

73kiapo alichomwapia baba yetu Abrahamu:

74kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu,

tupate kumtumikia yeye pasipo hofu

75katika utakatifu na haki mbele zake,

siku zetu zote.

76“Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana;

kwa kuwa utamtangulia Bwana

na kuandaa njia kwa ajili yake,

77kuwajulisha watu wake wokovu

utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao,

78kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu,

nuru inayotoka juu itatuzukia

79ili kuwaangazia wale wanaoishi gizani

na katika uvuli wa mauti,

kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.”

80Yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu katika roho; akaishi nyikani hadi siku ile alipojionesha hadharani kwa Waisraeli.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.