Mika 7

Mika 7

Taabu ya Israeli

1Taabu gani hii niliyo nayo!

Nimefanana na yule akusanyaye

matunda ya kiangazi,

aokotaye masazo baada ya kuvunwa

shamba la mizabibu;

hakuna kishada chenye matunda ya kula,

hakuna hata ile tini ya mwanzoni ninayoitamani.

2Wanaomcha Mungu wameondolewa kutoka nchi;

hakuna mtu mnyofu hata mmoja aliyebaki.

Watu wote wanavizia kumwaga damu,

kila mmoja anamwinda ndugu yake kwa wavu.

3Mikono yote miwili ni hodari katika kufanya ubaya,

mtawala anadai zawadi,

hakimu anapokea rushwa,

wenye nguvu wanaamuru wanachotaka:

wote wanapanga njama pamoja.

4Aliye mwema kupita wote kati yao

ni kama mchongoma,

anayeonekana mnyofu zaidi miongoni mwao

ni mbaya kuliko uzio wa miiba.

Siku ya walinzi wako imewadia,

siku Mungu atakayokutembelea.

Sasa ni wakati wao

wa kuchanganyikiwa.

5Usimtumaini jirani;

usiweke matumaini kwa rafiki.

Hata kwa yule alalaye kifuani mwako

uwe mwangalifu kwa maneno yako.

6Kwa kuwa mwana humdharau baba yake,

naye binti huinuka dhidi ya mama yake,

mkwe kuwa kinyume na mama mkwe wake:

adui wa mtu ni wale wa nyumbani mwake hasa.

7Lakini mimi, namtazama Bwana kwa matumaini,

namngoja Mungu Mwokozi wangu;

Mungu wangu atanisikia mimi.

Israeli atainuka

8Usifurahie msiba wangu, ee adui yangu!

Ingawa nimeanguka, nitainuka.

Japo ninaketi gizani,

Bwana atakuwa nuru yangu.

9Kwa sababu nimetenda dhambi dhidi yake,

nitabeba ghadhabu ya Bwana ,

hadi atakapotetea shauri langu

na kuithibitisha haki yangu.

Atanileta nje kwenye mwanga,

nami nitaiona haki yake.

10Kisha adui yangu ataliona

naye atafunikwa na aibu,

yule aliyeniambia,

“Yu wapi Bwana Mungu wako?”

Macho yangu yataona kuanguka kwake,

hata sasa atakanyagwa chini ya mguu

kama tope barabarani.

11Siku ya kujenga kuta zako itawadia,

siku ya kupanua mipaka yako.

12Siku hiyo watu watakuja kwako

kutoka Ashuru na miji ya Misri,

hata kutoka Misri hadi Mto Frati,

na kutoka bahari hadi bahari,

na kutoka mlima hadi mlima.

13Dunia itakuwa ukiwa kwa sababu ya wakazi wake,

kwa sababu ya matunda ya matendo yao.

Sala na sifa

14Wachunge watu wako kwa fimbo yako,

kundi la urithi wako,

ambalo linaishi peke yake msituni,

katika maeneo ya malisho yenye rutuba.

Waache walishe katika Bashani na Gileadi

kama ilivyokuwa siku za kale.

15“Kama siku zile mlipotoka Misri,

nitawaonesha maajabu yangu.”

16Mataifa yataona na kuaibika,

waliondolewa nguvu zao zote.

Wataweka mikono yao kwenye vinywa vyao

na masikio yao yatakuwa na uziwi.

17Wataramba mavumbi kama nyoka,

kama viumbe vinavyotambaa ardhini.

Watatoka nje ya mapango yao wakitetemeka;

watamgeukia Bwana Mungu wetu kwa hofu

nao watakuogopa.

18Ni nani Mungu kama wewe,

ambaye anaachilia dhambi

na kusamehe makosa

ya mabaki ya urithi wake?

Wewe huwi na hasira milele,

bali unafurahia kuonesha rehema.

19Utatuhurumia tena,

utazikanyaga dhambi zetu

chini ya nyayo zako,

na kutupa maovu yetu yote

katika vilindi vya bahari.

20Utakuwa wa kweli kwa Yakobo,

nawe utamwonesha Abrahamu rehema,

kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu

siku za kale.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.