The chat will start when you send the first message.
1Yesu akaanza kusema nao kwa mifano, akawaambia: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, na ndani yake akachimba shimo la shinikizo la kukamulia zabibu, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha shamba hilo la mizabibu kwa wakulima fulani, kisha akasafiri hadi nchi nyingine.
2Wakati wa mavuno ulipofika, mwenye shamba akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili kuchukua sehemu yake ya mavuno ya shamba la mizabibu kutoka kwa hao wapangaji.
3Lakini wale wakulima walimkamata yule mtumishi, wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu.
4Kisha yule mwenye shamba akamtuma mtumishi mwingine kwao; nao wale wakulima wakampiga kichwani na kumfanyia mambo ya aibu.
5Kisha akamtuma mtumishi mwingine, naye huyo wakamuua. Akawatuma wengine wengi; baadhi yao wakawapiga, na wengine wakawaua.
6“Mwenye shamba alikuwa bado na mmoja wa kumtuma, mwanawe aliyempenda. Hatimaye akamtuma akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’
7“Lakini wale wapangaji wakasemezana pamoja, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, nao urithi utakuwa wetu.’
8Hivyo wakamchukua na kumuua, wakamtupa nje ya lile shamba la mizabibu.
9“Sasa basi yule mwenye shamba atafanya nini? Atakuja na kuwaua hao wapangaji, kisha atawapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu.
10Je, hamjasoma andiko hili:
“ ‘Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni;
11Bwana ndiye alitenda jambo hili,
nalo ni la kushangaza machoni petu’?”
12Walipotambua kuwa amesema mfano huo kwa ajili yao, wakataka kumkamata, lakini wakaogopa umati ule wa watu. Wakamwacha, wakaenda zao.
13Baadaye wakawatuma baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili wamtege Yesu katika maneno yake.
14Wakamjia, wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu. Wewe huyumbishwi na wanadamu, kwa kuwa huna upendeleo. Lakini wewe huifundisha njia ya Mungu katika kweli. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?
15Je, tulipe kodi au tusilipe?”
Lakini Yesu alijua unafiki wao. Akawauliza, “Mbona mnajaribu kunitega? Nileteeni hiyo dinari niione.”
16Wakamletea hiyo sarafu. Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”
Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”
17Ndipo Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”
Nao wakamstaajabia sana.
18Kisha Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu,
19wakasema, “Mwalimu, Musa alituandikia kuwa kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto.
20Basi kulikuwa na ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa bila kuacha mtoto yeyote.
21Wa pili akamwoa yule mjane, lakini naye akafa bila kuacha mtoto yeyote. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa tatu.
22Hakuna hata mmoja wa hao ndugu saba aliyeacha mtoto. Hatimaye yule mwanamke naye akafa.
23Basi, wakati wa ufufuo yeye atakuwa mke wa nani, maana aliolewa na ndugu wote saba?”
24Yesu akawajibu, “Je, hampotei kwa sababu hamfahamu Maandiko wala uweza wa Mungu?
25Wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni.
26Basi kuhusu wafu kufufuliwa, je hamjasoma katika Kitabu cha Musa jinsi Mungu alivyosema na Musa kutoka kile kichaka akisema, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo’?[#12:26 Kut 3:6]
27Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Kwa hiyo mmekosea kabisa.”
28Mwalimu mmoja wa sheria akaja, akawasikia wakijadiliana. Akiona kwamba Yesu amewajibu vyema, naye akamuuliza, “Katika amri zote, ni ipi iliyo kuu?”
29Yesu akajibu, “Amri iliyo kuu ndiyo hii: ‘Sikia ee Israeli. Bwana Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.
30Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’[#12:30 Kum 6:4, 5]
31Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”[#12:31 Law 19:18]
32Yule mwalimu wa sheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye.
33Kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, na kwa ufahamu wako wote, na kwa nguvu zako zote, na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora kuliko kutoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu zote.”
34Yesu alipoona kwamba amejibu kwa busara, akamwambia, “Wewe huko mbali na ufalme wa Mungu.” Tangu wakati huo, hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumuuliza maswali tena.
35Yesu alipokuwa akifundisha Hekaluni, akauliza, “Imekuwaje walimu wa sheria wanasema kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi?[#12:35 maana yake Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.]
36Kwa maana Daudi mwenyewe, akinena kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, alisema:
“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.”’
37Kwa hiyo Daudi mwenyewe anamwita ‘Bwana.’ Awezaje basi yeye kuwa mwanawe?”
Umati ule wote wa watu wakamsikiliza kwa furaha.
38Alipokuwa akifundisha, Yesu alisema, “Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni.
39Pia wao hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi, na kupewa nafasi za heshima katika karamu.
40Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana.”
41Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha.
42Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.
43Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote.
44Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali yao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”