The chat will start when you send the first message.
1Mshambuliaji anasogea dhidi yako, Ninawi.
Linda ngome yako,
chunga barabara,
jitieni nguvu wenyewe,
kusanya nguvu zako zote!
2Bwana atarudisha fahari ya Yakobo,
kama fahari ya Israeli,
ingawa waangamizi wamewaacha ukiwa
na wameharibu mizabibu yao.
3Ngao za askari wake ni nyekundu,
mashujaa wamevaa nguo nyekundu.
Chuma kwenye magari ya vita chametameta,
katika siku aliyoyaweka tayari,
mikuki ya msunobari inametameta.
4Magari ya vita yanafanya msukosuko barabarani,
yakikimbia nyuma na mbele uwanjani.
Yanaonekana kama mienge ya moto;
yanaenda kasi kama umeme.
5Anaita vikosi vilivyochaguliwa,
lakini bado wanajikwaa njiani.
Wanakimbilia haraka kwenye ukuta wa mji,
ile ngao ya kuwakinga imetayarishwa.
6Malango ya mto yamefunguliwa wazi,
na jumba la kifalme limeanguka.
7Imeagizwa kwamba mji uchukuliwe
na upelekwe uhamishoni.
Vijakazi wake wanaomboleza kama hua
na kupigapiga vifua vyao.
8Ninawi ni kama dimbwi,
nayo maji yake yanakauka.
Wanalia, “Simama! Simama!”
Lakini hakuna anayegeuka nyuma.
9Chukueni nyara za fedha!
Chukueni nyara za dhahabu!
Wingi wake hauna mwisho,
utajiri kutoka hazina zake zote!
10Ameharibiwa, ametekwa nyara, ameachwa uchi!
Mioyo inayeyuka, magoti yanalegea,
miili inatetemeka,
na kila uso umebadilika rangi.
11Liko wapi sasa pango la simba,
ambapo waliwalisha watoto wao,
ambapo simba dume na simba jike walienda,
na wana simba pia,
bila kuogopa chochote?
12Simba aliua mawindo ya kutosha watoto wake,
alinyonga mawindo kwa ajili ya mwenzi wake,
akijaza makao yake kwa alivyoua
na mapango yake kwa mawindo.
13Bwana wa majeshi anatangaza,
“Mimi ni kinyume na ninyi.
Magari yenu ya vita nitayateketeza kwa moto,
na upanga utakula wana simba wako.
Sitawaachia mawindo juu ya nchi.
Sauti za wajumbe wako
hazitasikika tena.”