The chat will start when you send the first message.
1Wakati huu wanaume na wake zao wakalia kilio kikuu dhidi ya ndugu zao Wayahudi.
2Baadhi yao walikuwa wakisema, “Sisi na wana wetu wa kiume na wa kike tuko wengi. Ili tuweze kula na kuishi, ni lazima tupate nafaka.”
3Wengine walikuwa wakisema, “Tunaweka rehani mashamba yetu, mashamba ya mizabibu, na nyumba zetu ili tupate nafaka wakati wa njaa.”
4Bado kukawa na wengine waliokuwa wakisema, “Ilitubidi tukope fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa ajili ya mashamba yetu na mashamba yetu ya mizabibu.
5Ingawa sisi ni mwili na damu moja sawa na watu wa nchi yetu, na ijapo wana wetu ni wazuri kama wana wao, bado inatupasa kuwatoa wana wetu wa kiume na wa kike kwenye utumwa. Baadhi ya binti zetu wameshakuwa watumwa tayari, lakini hatuna uwezo wa kuwakomboa, kwa sababu mashamba yetu na mashamba ya mizabibu yetu ni mali ya watu wengine.”
6Niliposikia kilio chao na malalamiko haya, nilikasirika sana.
7Nikayatafakari katika akili yangu, nikiwalaumu wakuu na maafisa. Nikawaambia, “Mnawaonea ndugu zenu kwa kuwatoza riba!” Basi nikaita mkutano mkubwa ili kukabiliana nao,
8nikasema: “Kulingana na uwezo wetu, tumewakomboa ndugu zetu Wayahudi waliokuwa wameuzwa kwa watu wasioamini. Sasa mnawauza ndugu zenu, ili wauzwe tena kwetu!” Wakanyamaza, kwa sababu hawakupata chochote cha kusema.
9Basi nikaendelea kusema, “Mnachokifanya si sawa. Je, haikuwapasa kutembea katika hofu ya Mungu wetu ili tuepukane na shutuma za adui zetu wasioamini?
10Mimi na ndugu zangu na watu wangu tunawakopesha watu fedha na nafaka. Lakini jambo hili la kutoza riba likome!
11Warudishieni mara moja mashamba yao, mashamba yao ya mizabibu, mashamba yao ya mizeituni, na nyumba zao, pia riba yao mnayowatoza na sehemu ya fungu la mia la fedha, nafaka, divai mpya na mafuta.”
12Wakasema, “Tutawarudishia na hatutataka kitu chochote zaidi kutoka kwao. Tutafanya kama ulivyosema.”
Kisha nikawaita makuhani na kuwafanya wakuu na maafisa kuapa kufanya kile walichoahidi.
13Pia nikakungʼuta makunjo ya vazi langu na kusema, “Kila mtu ambaye hatatimiza ahadi hii, Mungu na amkungʼute hivi kutoka nyumba yake na katika mali yake. Basi mtu kama huyo akungʼutiwe nje na aachwe bila kitu!”
Waliposikia hili, mkutano wote ukasema, “Amen,” na wakamtukuza Bwana . Nao watu wakafanya kama walivyokuwa wameahidi.
14Zaidi ya hayo, kutoka mwaka wa ishirini wa Mfalme Artashasta, wakati nilipoteuliwa kuwa mtawala wao katika nchi ya Yuda, hadi mwaka wake wa thelathini na mbili, yaani miaka kumi na mbili, mimi wala ndugu zangu hatukula chakula ambacho kwa kawaida hupewa watawala.
15Lakini watawala wa mwanzoni, wale walionitangulia, waliwalemea watu na kuchukua kutoka kwao shekeli arobaini za fedha, pamoja na chakula na mvinyo. Wasaidizi wao pia walijifanya wakuu juu ya watu. Lakini kwa kumheshimu Mungu sikufanya hivyo.[#5:15 Shekeli 40 za fedha ni sawa na gramu 456.]
16Badala yake, nilijitoa kwa bidii katika kazi ya ukuta huu. Watu wangu wote walikutanika pale kwa ajili ya kazi. Hatukujipatia shamba lolote.
17Zaidi ya hayo, Wayahudi na maafisa mia moja na hamsini walikula mezani pangu, pamoja na wale waliotujia kutoka mataifa jirani.
18Kila siku niliandaliwa maksai mmoja, kondoo sita wazuri, na kuku, na mvinyo wa kila aina kwa wingi kila baada ya siku kumi. Licha ya mambo haya yote, sikudai chakula kilichokuwa fungu la mtawala, kwa sababu madai yalikuwa mazito sana kwa watu hawa.
19Unikumbuke kwa fadhili, Ee Mungu wangu, kwa yote niliyofanya kwa ajili ya watu hawa.