The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Musa:
2“Tengeneza tarumbeta mbili za fedha ya kufua, uzitumie kwa kuita jumuiya pamoja na wakati wa kuvunja makambi ili kuondoka.
3Tarumbeta zote mbili zikipigwa, jumuiya yote itakusanyika mbele yako katika ingilio la Hema la Kukutania.
4Kama tarumbeta moja tu ikipigwa, viongozi, yaani wakuu wa koo za Israeli, ndio watakaokusanyika mbele yako.
5Mlio wa kujulisha hatari ukipigwa, makabila yaliyo na makambi upande wa mashariki yataondoka.
6Mlio wa pili ukipigwa, walio kwenye makambi ya kusini wataondoka. Mlio huo wa kujulisha hatari utakuwa ishara ya kuondoka.
7Ili kuwakusanya watu, piga tarumbeta zote, lakini siyo kwa mlio wa kujulisha hatari.
8“Wana wa Haruni, makuhani, ndio watakaopiga hizo tarumbeta. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu na kwa vizazi vijavyo.
9Mtakapopigana vita katika nchi yenu wenyewe dhidi ya adui anayewaonea, piga tarumbeta kwa mlio wa kujulisha hatari. Ndipo utakumbukwa na Bwana Mungu wenu na kuokolewa kutoka kwa adui zenu.
10Pia nyakati za furaha yenu, yaani sikukuu zenu zilizoamriwa na sikukuu za Mwezi Mwandamo, mtapiga tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za amani, nazo zitakuwa ukumbusho kwa ajili yenu mbele za Mungu wenu. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.”
11Katika siku ya ishirini ya mwezi wa pili wa mwaka wa pili, wingu liliinuka kutoka juu ya Maskani ya Ushuhuda.
12Ndipo Waisraeli wakaondoka kutoka Jangwa la Sinai wakasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine hadi wingu lilipotua katika Jangwa la Parani.
13Waliondoka kwa mara ya kwanza kwa agizo la Bwana kupitia kwa Musa.
14Vikosi vya kambi ya Yuda vilitangulia kwanza chini ya beramu yao. Nashoni mwana wa Aminadabu alikuwa kiongozi wao.
15Nethaneli mwana wa Suari alikuwa kiongozi wa kabila la Isakari,
16naye Eliabu mwana wa Heloni alikuwa kiongozi wa kabila la Zabuloni.
17Ndipo Maskani iliposhushwa, nao wana wa Gershoni na wana wa Merari ambao waliibeba wakaondoka.
18Vikosi vya kambi ya Reubeni vilifuata, chini ya beramu yao. Elisuri mwana wa Shedeuri alikuwa kiongozi wao.
19Shelumieli mwana wa Surishadai aliongoza kikosi cha kabila la Simeoni,
20naye Eliasafu mwana wa Deueli aliongoza kikosi cha kabila la Gadi.
21Kisha Wakohathi wakaondoka, wakichukua vitu vitakatifu. Maskani ilipaswa kusimamishwa kabla wao hawajafika.
22Vikosi vya kambi ya Efraimu vilifuata, chini ya beramu yao. Elishama mwana wa Amihudi alikuwa kiongozi wao.
23Gamalieli mwana wa Pedasuri aliongoza kikosi cha kabila la Manase,
24naye Abidani mwana wa Gideoni alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Benyamini.
25Mwishowe, kama kikosi cha nyuma cha ulinzi wa vikosi vyote, vikosi vya kambi ya Dani viliondoka chini ya beramu yao. Ahiezeri mwana wa Amishadai alikuwa kiongozi wao.
26Pagieli mwana wa Okrani aliongoza kikosi cha kabila la Asheri,
27naye Ahira mwana wa Enani aliongoza kikosi cha kabila la Naftali.
28Huu ndio ulikuwa utaratibu wa kuondoka wa vikosi vya Waisraeli walipokuwa wanaondoka.
29Basi Musa akamwambia Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwewe Musa, “Tunaondoka kwenda mahali ambapo Bwana amesema ‘Nitawapa ninyi mahali hapo.’ Twende pamoja, nasi tutakutendea mema, kwa maana Bwana ameahidi mambo mema kwa Israeli.”
30Akajibu, “Hapana, sitaenda; nitarudi kwenye nchi yangu mwenyewe na watu wangu mwenyewe.”
31Lakini Musa akasema, “Tafadhali usituache. Wewe unajua mahali yatupasa kupiga kambi jangwani, nawe unaweza kuwa macho yetu.
32Ikiwa utafuatana nasi, tutashirikiana nawe mema yoyote tutakayopewa na Bwana .”
33Hivyo waliondoka kutoka mlima wa Bwana , nao wakasafiri kwa siku tatu. Sanduku la Agano la Bwana liliwatangulia kwa zile siku tatu ili kuwatafutia mahali pa kupumzika.
34Wingu la Bwana lilikuwa juu yao wakati wa mchana walipoondoka kambini.
35Wakati wowote Sanduku lilipoondoka, Musa alisema,
“Ee Bwana , inuka!
Watesi wako na watawanyike;
adui zako na wakimbie mbele zako.”
36Wakati wowote Sanduku liliposimama, alisema,
“Ee Bwana , rudi,
kwa maelfu ya Waisraeli wasiohesabika.”