The chat will start when you send the first message.
1Msifuni Mwenyezi Mungu.[#112:1 kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.]
Heri mtu yule amchaye Mwenyezi Mungu,
mtu yule apendezwaye sana na amri zake.
2Watoto wake watakuwa wenye uwezo katika nchi,
kizazi cha watu waadilifu kitabarikiwa.
3Nyumbani mwake kuna mali na utajiri,
haki yake hudumu milele.
4Hata gizani nuru humzukia mtu mwadilifu,
yule mwenye rehema, huruma na haki.
5Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba,
anayefanya mambo yake kwa haki.
6Hakika hatatikisika kamwe,
mtu mwenye haki atakumbukwa milele.
7Hataogopa habari mbaya,
moyo wake ni thabiti, ukimtegemea Mwenyezi Mungu.
8Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu,
mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake.
9Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini;
haki yake hudumu milele;
pembe yake itatukuzwa kwa heshima.
10Mtu mwovu ataona na kuchukizwa,
atasaga meno yake na kutoweka,
kutamani kwa mtu mwovu kutaishia patupu.