Ufunuo 10

Ufunuo 10

Malaika na kijitabu

1Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua juu ya kichwa chake. Uso wake ulingʼaa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto.

2Mkononi mwake alikuwa ameshika kijitabu kilichokuwa kimefunguliwa. Akauweka mguu wake wa kuume juu ya bahari na mguu wake wa kushoto akauweka juu ya nchi kavu.

3Naye akapaza sauti kwa nguvu kama simba anayenguruma. Aliponguruma, zile radi saba zikatoa ngurumo zake.

4Nazo zile radi saba zilipotoa ngurumo, nilitaka kuanza kuandika, lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Yatie muhuri hayo yaliyosemwa na hizo radi saba na usiyaandike.”

5Kisha yule malaika niliyekuwa nimemwona akiwa amesimama juu ya bahari na juu ya nchi akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni.

6Naye akaapa kwa Yule aishiye milele na milele, aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, dunia na vyote viijazavyo, pamoja na bahari na vyote vilivyomo, akasema, “Hakuna kungoja tena!

7Lakini katika siku zile huyo malaika wa saba atakaribia kuipiga hiyo tarumbeta yake, siri ya Mungu itatimizwa, kama vile alivyowatangazia watumishi wake manabii.”

8Ndipo ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni ikasema nami tena, ikaniambia, “Nenda, chukua kile kitabu kilichofunguliwa kilichoko mkononi mwa yule malaika aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu.”

9Basi nikamwendea nikamwomba yule malaika anipe kile kijitabu. Akaniambia, “Chukua na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako, lakini kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali.”[#10:9 Eze 3:3]

10Hivyo nikakichukua kile kijitabu kutoka mkononi mwa yule malaika, nikakila. Kilikuwa kitamu kama asali kinywani mwangu, lakini baada ya kukila, tumbo langu likatiwa uchungu.

11Kisha nikaambiwa, “Imekupasa kutoa unabii tena kuhusu makabila mengi, mataifa, lugha na wafalme.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.