Ufunuo 7

Ufunuo 7

Waisraeli 144,000 watiwa muhuri

1Baada ya hili nikaona malaika wanne wakiwa wamesimama katika pembe nne za dunia, wakizuia hizo pepo nne za dunia, ili pasiwe na upepo utakaovuma juu ya nchi au juu ya bahari au juu ya mti wowote.

2Nikaona malaika mwingine akipanda kutoka mawio ya jua akiwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Akawaita kwa sauti kubwa wale malaika wanne waliokuwa wamepewa mamlaka ya kuidhuru nchi na bahari, akisema,

3“Msiidhuru nchi wala bahari, wala miti, hadi tuwe tumetia muhuri kwenye paji za nyuso za watumishi wa Mungu wetu.”

4Ndipo nikasikia idadi ya wale waliotiwa muhuri: elfu mia moja na arobaini na nne kutoka makabila yote ya Israeli.

5Kutoka kabila la Yuda elfu kumi na mbili walitiwa muhuri,

kutoka kabila la Reubeni elfu kumi na mbili,

kutoka kabila la Gadi elfu kumi na mbili,

6kutoka kabila la Asheri elfu kumi na mbili,

kutoka kabila la Naftali elfu kumi na mbili,

kutoka kabila la Manase elfu kumi na mbili,

7kutoka kabila la Simeoni elfu kumi na mbili,

kutoka kabila la Lawi elfu kumi na mbili,

kutoka kabila la Isakari elfu kumi na mbili,

8kutoka kabila la Zabuloni elfu kumi na mbili,

kutoka kabila la Yusufu elfu kumi na mbili,

na kutoka kabila la Benyamini elfu kumi na mbili.

Umati mkubwa wa watu kutoka mataifa yote

9Baada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna yeyote awezaye kuwahesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao.

10Nao walikuwa wakipaza sauti kwa nguvu, wakisema:

“Wokovu una Mungu wetu,

yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi,

na Mwana-Kondoo!”

11Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee, na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu,

12wakisema:

“Amen!

Sifa na utukufu

na hekima na shukrani na heshima

na uweza na nguvu

viwe kwa Mungu wetu milele na milele.

Amen!”

13Kisha mmoja wa wale wazee akaniuliza, “Ni nani hawa waliovaa mavazi meupe, nao wametoka wapi?”

14Nikamjibu, “Bwana, wewe unajua.”

Naye akasema, “Hawa ni wale waliotoka katika ile dhiki kuu, nao wamefua mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo na kuyafanya meupe kabisa.

15Kwa hiyo,

“Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu

na kumtumikia usiku na mchana

katika Hekalu lake;

naye aliyeketi katika kile kiti cha enzi

atatanda hema lake juu yao.

16Kamwe hawataona njaa

wala kiu tena.

Jua halitawachoma

wala joto lolote liunguzalo.

17Kwa maana Mwana-Kondoo

aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi

atakuwa Mchungaji wao;

naye atawaongoza kwenda

kwenye chemchemi za maji yaliyo hai.

Naye Mungu atawafuta machozi

kutoka machoni mwao.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.