The chat will start when you send the first message.
1Basi Sulemani, mwana wa Daudi, alijiimarisha katika ufalme wake, naye BWANA, Mungu wake, alikuwa pamoja naye, akamtukuza mno.[#1 Fal 2:46; Mwa 21:22; 39:2; 1 Nya 17:8; 29:25; Mt 28:20]
2Sulemani akawaita Israeli wote, na makamanda wa maelfu, na wa mamia, na waamuzi, na kila kiongozi wa Israeli, na wakuu wa familia.[#1 Nya 27:1; 2 Nya 29:20; 30:2]
3Basi Sulemani akaenda mahali pa juu pa Gibeoni, na kusanyiko lote naye; kwani ndipo lilipokuwako hema la kukutania la Mungu, alilolifanya Musa mtumishi wa BWANA jangwani.[#1 Fal 3:4]
4Lakini sanduku la Mungu, Daudi alikuwa amelipandisha kutoka Kiriath-yearimu mpaka mahali Daudi alipolitengenezea; maana amelitandia hema katika Yerusalemu.[#2 Sam 6:2; 1 Nya 15:1]
5Tena madhabahu ya shaba, aliyoifanya Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwako huko mbele ya maskani ya BWANA; Sulemani na kusanyiko wakaiendea.[#Kut 27:1; 38:1; 31:2]
6Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za BWANA, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu yake.[#1 Fal 3:4]
7Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe.[#1 Fal 3:5; Mit 3:5; Isa 58:9]
8Sulemani akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake.[#1 Nya 28:5]
9Basi sasa, Ee BWANA Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi.[#1 Fal 3:7]
10Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwatawala watu wako hawa walio wengi?[#1 Fal 3:9; Zab 119:34,73; Mit 3:13; Yak 1:5; Hes 27:17; Kum 31:2]
11Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha ya wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwatawala watu wangu, niliokutawaza juu yao;[#1 Sam 16:7; 1 Fal 3:11; 8:18]
12basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.[#Zab 34:9,10; Mt 6:33; Efe 3:20; 1 Nya 29:25; 2 Nya 9:22; Mhu 2:9]
13Basi Sulemani akatoka mahali pa juu pa Gibeoni, toka mbele ya Hema la kukutania, akaja mpaka Yerusalemu; akatawala Israeli.
14Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu moja na mia nne, na wapandao farasi elfu kumi na mbili, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.[#1 Fal 4:26]
15Mfalme akafanya fedha na dhahabu kuwa kama mawe humo Yerusalemu, na mierezi akaifanya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi.[#1 Fal 10:27; Ayu 22:24]
16Nao farasi, aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi; kila kundi na thamani yake.
17Nao walipandisha na kununua gari kutoka Misri kwa shekeli mia sita za fedha; na farasi kwa mia moja na hamsini, vivyo hivyo wakawauzia wafalme wote Wahiti na wafalme wa Shamu.[#1:17 Katika Kiebrania maana ya mstari huu sio dhahiri.]