2 Wakorintho 11

2 Wakorintho 11

Paulo na mitume wa uongo

1Laiti mngechukuliana nami katika upumbavu wangu kidogo! Naam, mchukuliane nami.

2Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa niliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.[#Efe 5:26,27]

3Lakini nahofu; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.[#Mwa 3:1-5,13]

4Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au Injili nyingine msiyoikubali, mnavumiliana naye punde![#Gal 1:8,9]

5Maana nadhani ya kuwa mimi sikupungukiwa na kitu walicho nacho mitume walio wakuu.[#2 Kor 12:11; 1 Kor 15:10; Gal 2:6,9]

6Lakini nijapokuwa mimi ni mtu asiyejua kunena, hii si hali yangu katika elimu; ila katika kila neno tumedhihirishwa kwenu.[#1 Kor 2:1,2,13; Efe 3:4]

7Je! Nilifanya dhambi kwa kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa sababu niliwahubiria Injili ya Mungu bila ujira?[#1 Kor 9:12,18]

8Niliwanyang'anya makanisa mengine mali yao, nikitwaa posho yangu ili niwahudumie ninyi.[#Flp 4:10,15]

9Nami nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana hao ndugu waliokuja kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu; nami katika mambo yote najilinda nafsi yangu nisiwalemee hata kidogo; tena najilinda.[#Flp 4:15-18; 2 Kor 12:13]

10Kama vile ile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu atakayenifumba kinywa katika kujisifu huku, katika mipaka ya Akaya.[#1 Kor 9:15]

11Kwa nini? Je! Ni kwa sababu siwapendi ninyi? Mungu anajua.

12Lakini nifanyalo nitalifanya, ili niwapinge hao watafutao nafasi wasipate nafasi; ili kwamba katika neno hilo wajisifialo waonekane kuwa kama sisi.

13Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo.[#2 Kor 2:17; Flp 3:2]

14Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.

15Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.

Mateso ya Paulo kama mtume

16Nasema tena, mtu asidhani ya kuwa mimi ni mpumbavu; lakini mjaponidhania hivi, mnikubali kama mpumbavu; ili mimi nami nipate kujisifu angalau kidogo.[#2 Kor 12:6]

17Ninenalo silineni agizo la Bwana, bali kama kwa upumbavu, katika ujasiri huu wa kujisifu.

18Kwa sababu wengi wanajisifu kwa jinsi ya mwili, mimi nami nitajisifu.

19Ninyi, kwa kuwa mna akili, mnachukuliana na wajinga kwa furaha.

20Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni.

21Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Lakini, ikiwa mtu anao ujasiri kwa lolote, (nanena kipuuzi), mimi nami ninao ujasiri.

22Wao ni Waebrania? Na mimi pia. Wao ni Waisraeli? Na mimi pia. Wao ni uzao wa Abrahamu? Na mimi pia.[#Flp 3:5]

23Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi.[#Mdo 16:23; 1 Kor 15:10]

24Kwa Wayahudi mara tano nilipata mapigo arobaini kasoro moja.[#Kum 25:3]

25Mara tatu nilipigwa kwa bakora; mara moja nilipigwa kwa mawe; mara tatu nilivunjikiwa jahazi; kutwa kucha nimepata kukaa kilindini;[#Mdo 16:22; 14:19]

26katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo;[#Mdo 9:23; 14:15]

27katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi.[#2 Kor 6:5]

28Mbali na mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote.[#Mdo 20:18-21]

29Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe?[#1 Kor 9:22]

30Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu.[#2 Kor 12:6]

31Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo.[#2 Kor 1:23]

32Huko Dameski mtawala wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, ili kunikamata;[#Mdo 9:23-25]

33nami nikateremshwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka katika mikono yake.[#Mdo 9:24,25]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania