Matendo 26

Matendo 26

Paulo ajitetea mbele ya Agripa

1Agripa akamwambia Paulo, Una ruhusa kusema maneno yako. Ndipo Paulo akanyosha mkono wake, akajitetea,

2Najiona nafsi yangu kuwa na heri, Ee mfalme Agripa, kwa kuwa nitajitetea mbele yako leo, katika mambo yale yote niliyoshitakiwa na Wayahudi.

3Hasa kwa sababu wewe unajua sana desturi na maswali yote waliyo nayo Wayahudi; kwa sababu hiyo nakuomba unisikilize kwa uvumilivu.

4Kwa maana Wayahudi wote wanajua maisha yangu tangu ujana, yalivyokuwa tangu mwanzo katika taifa langu huko Yerusalemu,

5wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nilikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa.[#Mdo 23:6; Flp 3:5]

6Na sasa ninasimama hapa nihukumiwe kwa ajili ya tumaini la ahadi waliyopewa baba zetu na Mungu,[#Mdo 28:20]

7ambayo kabila zetu kumi na mbili wanataraji kuifikia, wakimwabudu Mungu kwa bidii mchana na usiku. Nami ninashitakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hilo, Ee Mfalme.[#Mdo 24:15]

8Kwa nini limedhaniwa kwenu kuwa ni neno lisiloaminika, kwamba Mungu awafufua wafu?

9Kweli, mimi mwenyewe niliona ndani ya nafsi yangu kwamba yanipasa kutenda mambo mengi yaliyopingana na jina lake Yesu Mnazareti;[#Mdo 8:3; 22:4-5; #Mdo 9:1-29; 22:3-21]

10nami nikayafanya hayo Yerusalemu; niliwafunga wengi miongoni mwa watakatifu ndani ya magereza, nikiisha kupewa amri na wakuu wa makuhani; na walipouawa nilitoa idhini yangu.

11Na mara nyingi katika masinagogi yote niliwaadhibu, nikawashurutisha kukufuru; nikawaonea hasira kama mwenye wazimu, nikawaudhi hata katika miji ya ugenini.

Paulo asema juu ya kuongoka kwake

12Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani;

13Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani niliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote.

14Tukaanguka chini sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo.

15Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi.

16Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako;[#Eze 2:1,3]

17nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao;[#Yer 1:7; 1 Nya 16:35]

18uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.[#Kum 33:3; Isa 35:5; 42:7,16; Mdo 20:32; Efe 2:2; Kol 1:13]

Paulo aeleza juu ya mahubiri yake

19Kwa hiyo, Ee Mfalme Agripa, sikuyaasi yale maono ya mbinguni,[#Gal 1:16]

20bali kwanza niliwahubiria wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Yudea, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao.[#Mdo 9:20,28-29; Mt 3:8]

21Kwa sababu ya hayo Wayahudi wakanikamata nikiwa ndani ya hekalu wakajaribu kuniua.[#Mdo 21:30,31]

22Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, wala sisemi neno ila yale ambayo manabii na Musa waliyasema, kwamba yatakuwa;[#Lk 24:44-47]

23ya kwamba Kristo hana budi kuteswa na ya kwamba yeye kwanza kwa kufufuliwa katika wafu atatangaza habari za nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa.[#Isa 42:6; 49:6; 1 Kor 15:20]

Paulo amwomba Agripa aamini

24Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili.

25Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili.

26Kwa maana mfalme anajua habari za mambo haya, nami naweza kusema naye kwa ujasiri, kwa sababu najua sana ya kuwa hapana neno moja katika hayo asilolijua; kwa maana jambo hilo halikutendeka pembeni.[#Yn 18:20]

27Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini.

28Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo.[#Mdo 11:26; 1 Pet 4:16]

29Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa kuwa katika minyororo hii.

30Mfalme na mtawala na Bernike na wale walioketi pamoja nao wakasimama;

31hata walipoondoka wakasemezana, wakisema, Mtu huyu hatendi neno linalostahili kifo wala kufungwa.

32Agripa akamwambia Festo, Mtu huyo angeweza kufunguliwa, kama asingalitaka rufani kwa Kaisari.[#Mdo 25:11]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania