The chat will start when you send the first message.
1Utunze mwezi wa Abibu, ukamfanyie Pasaka BWANA, Mungu wako, kwa kuwa ilikuwa ni mwezi wa Abibu alipokutoa Misri usiku BWANA; Mungu wako.[#Kut 12:1-20; Law 23:5-8; Hes 28:16-25; Yn 18:28; 1 Kor 5:7,8; Ebr 11:28]
2Nawe umchinjie Pasaka BWANA, Mungu wako, katika kundi la kondoo na la ng'ombe, mahali atakapochagua BWANA apakalishe jina lake.[#Kut 12:5-7; Hes 28:19; 2 Nya 35:7; Mt 26:2; Mk 14:12; Lk 22:8,15; 1 Kor 5:7]
3Usimle pamoja na mikate iliyotiwa chachu; siku saba utakula naye mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso; kwa maana ulitoka nchi ya Misri kwa haraka; ili upate kukumbuka siku uliyotoka nchi ya Misri, siku zote za maisha yako.[#Kut 12:15,19,39; 13:3; 34:18]
4Wala isionekane kwako chachu muda wa siku saba katika mipaka yako yote; wala katika hiyo nyama uchinjayo siku ya kwanza jioni, kisilale chochote usiku kucha hata asubuhi.[#Kut 12:10; 34:25]
5Usimchinje Pasaka ndani ya malango yako yote akupayo BWANA, Mungu wako;
6ila mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake, ndipo mtakapomchinja Pasaka jioni, katika machweo ya jua, kwa wakati kama uliotoka Misri.[#Mt 27:46]
7Nawe umwoke na kumla mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako; kisha asubuhi yake ugeuke uende hemani mwako.[#Kut 12:8; 2 Nya 35:13; 2 Fal 23:23; Yn 2:13; 11:55]
8Siku sita utakula mikate isiyotiwa chachu; na siku ya saba na uwe mkutano mtukufu kwa BWANA, Mungu wako, usifanye kazi yoyote.[#Kut 12:16; 13:6; Law 23:8]
9Jihesabie majuma saba; tangu wakati uanzao kutia mundu katika mmea utaanza kuhesabu majuma saba.[#Law 23:15-21; Hes 28:26-31; Kut 23:16; 34:22; Mdo 2:1]
10Nawe sikukuu ya majuma umfanyie BWANA, Mungu wako, kwa kutoa sadaka ya hiari ya mkono wako, utakayotoa kwa kadiri akubarikivyo BWANA, Mungu wako;[#Mit 10:22; Yoe 2:14; 1 Kor 16:2]
11nawe utafurahi mbele za BWANA, Mungu wako, wewe na mwana wako na binti yako, na mtumwa wako na mjakazi wako, na Mlawi aliye ndani ya malango yako, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiwa na mumewe, walio katikati yako, katika mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake.[#Lk 14:12]
12Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa huko Misri; tena zishike amri hizi kwa kuzifanya.[#Mwa 15:13; Kut 1:11,14; Kum 15:15; 25:6; Zab 105:23,25]
13Fanya sikukuu ya vibanda siku saba, utakapokwisha kuyakusanya yatokayo katika sakafu yako ya nafaka, na katika kinu chako cha divai;[#Law 23:33-36,39-43; Hes 29:12-38; Kut 23:16]
14nawe utafurahi katika sikukuu yako, wewe, na mwanao, na binti yako, na mtumwa wako, na mjakazi wako, na Mlawi, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiwa na mumewe, walio ndani ya malango yako.[#Kum 26:11; Neh 8:9; Mhu 9:7; Isa 12:1-6; 25:6-8]
15Siku saba mfanyie sikukuu BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua BWANA; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, atakubariki katika mavuno yako yote, na katika kazi zote za mikono yako, nawe uwe katika kufurahi kabisa.
16Mara tatu kwa mwaka na watokee wana wa kiume wako wote mbele za BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala wasitokee mbele za BWANA mikono mitupu.
17Kila mtu na atoe kama awezavyo, kwa kadiri ya baraka za BWANA, Mungu wako, alivyokupa.[#2 Kor 8:12]
18Weka waamuzi na maofisa katika malango yako yote akupayo BWANA, Mungu wako, kwa hesabu ya kabila zako; nao wawaamue watu kwa maamuzi ya haki.
19Usipotoe maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu; wala usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza kesi za wenye haki.[#Kut 23:6-8; Law 19:15; 1 Sam 8:3; 12:3; Ayu 31:21,22; Mit 17:23; 24:23; Mhu 7:7; Isa 1:17,23; Mdo 10:34]
20Yaliyo haki kabisa ndiyo utakayoyafuata, ili upate kuishi na kuirithi nchi upewayo na BWANA, Mungu wako.[#Kum 4:1]
21Usipande mti uwao wote kuwa Ashera kwako kando ya madhabahu utakayofanya ya BWANA, Mungu wako.[#Kut 34:13; Amu 3:7; 1 Fal 14:15; 16:33; 2 Fal 17:16; 21:3; 2 Nya 33:3]
22Wala usisimamishe nguzo; ambayo BWANA, Mungu wako, aichukia.[#Law 26:1]