Kumbukumbu la Torati 23

Kumbukumbu la Torati 23

Waliokatazwa mkutanoni

1Aliyejeruhika konde, au aliyekatika tupu yake, asiingie mtu huyo katika mkutano wa BWANA.

2Mwana wa haramu asiingie katika mkutano wa BWANA; hata kizazi cha kumi asiingie aliye wake katika mkutano wa BWANA.

3Mwamoni wala Mmoabi wasiingie katika mkutano wa BWANA; wala hata kizazi cha kumi mtu wao asiingie katika mkutano wa BWANA milele;[#Neh 13:1-2; 4:3-7; Rut 4:5]

4kwa sababu hapo mlipotoka Misri hawakuwalaki na chakula wala maji njiani; na kwa kuwa walimwajiri juu yako Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia, aje akulaani.[#Hes 22:1-6; Mwa 14:18; Kum 2:29; 1 Sam 25:11; 1 Fal 18:4; Isa 63:9; Mt 10:40,42; 25:41-46; Yos 24:9]

5Lakini BWANA, Mungu wako, hakukubali kumsikiliza huyo Balaamu; BWANA, Mungu wako, aliyageuza yale maapizo kuwa ni baraka, kwa vile alivyokupenda BWANA, Mungu wako.[#Hes 23:7–24:9; Mit 26:2]

6Usitafute amani yao wala heri yao siku zako zote, milele.[#Ezr 9:12]

7Usimchukie Mwedomi; kwa kuwa ni ndugu yako; usimchukie Mmisri, kwa kuwa ulikuwa mgeni katika nchi yake.[#Mwa 25:24-26; Oba 1:12; Kut 22:21; 23:9; Kum 10:19; Law 19:34]

8Wana wao watakaozaliwa kizazi cha tatu na waingie katika mkutano wa BWANA.

Maagizo kuhusu usafi, ibada na utu

9Utakapotoka kwenda juu ya adui zako nawe u katika kambi, jilinde na kila neno baya.

10Akiwa kwenu mtu awaye yote asiyekuwa ni tohara kwa ajili ya yaliyomtukia usiku, na atoke nje ya kituo, wala asiingie ndani ya kituo;[#Law 15:16; Hes 5:2,3; 1 Kor 5:11,13]

11lakini na iwe ikaribiapo jioni, yeye ataoga maji; na jua likiisha kuchwa ataingia ndani ya kituo.

12Tena uwe na mahali nje ya kituo, kwa kutokea nje;

13nawe uwe na jembe dogo katika silaha zako; napo uotamapo nje uchimbe kwa lile jembe, na kugeuka na kukifunika kikutokacho;

14kwa kuwa BWANA. Mungu wako, yuatembea katika kituo akuokoe, na kukutolea adui zako mbele yako; kwa hiyo na kiwe kitakatifu kituo chako; asije akaona kitu kwako kisichokuwa safi, akageuka na kukuacha.[#Mwa 15:1; Law 26:12; Yer 32:40; 2 Kor 6:16; Kut 3:5]

15Usimrudishe kwa bwana wake mtumwa aliyejiponya kutoka kwa bwana wake kuja kwako;[#1 Sam 30:15]

16na akae nawe, katikati yako, ndani ya malango yako mojawapo, mahali atakapochagua palipo pema machoni pake; usimwonee.[#Kut 22:21; 23:9; Mit 22:22; Yer 7:6; Zek 7:10; Mal 3:5; Yak 2:6]

17Pasiwe na kahaba katika binti za Israeli, wala pasiwe na hanithi katika wana wa Israeli wanaume.[#Law 19:29; Mit 2:16; Mwa 19:5; 2 Fal 23:7]

18Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya BWANA, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yoyote; kwani haya ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako, yote mawili.

19Usimkopeshe ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula, riba ya kitu chochote kikopeshwacho kwa riba;[#Kut 22:25; Law 25:36-37; Kum 15:7-11; Neh 5:2,7; Zab 15:5; Lk 6:34]

20mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; ili BWANA, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki.[#Law 19:34; Kum 15:10]

21Utakapoweka nadhiri kwa BWANA, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako.[#Hes 30:1-16; Mt 5:33; Ayu 22:27; Zab 61:8; Mhu 5:4,5]

22Lakini ukijizuia usiweke nadhiri, haitakuwa dhambi kwako.

23Yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri BWANA, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako.[#Zab 66:13]

24Uingiapo katika shamba la mizabibu la jirani yako, utaweza kula zabibu za kukushibisha, kama upendavyo; ila usitie katika chombo chako.[#Mt 12:1; Lk 12:15; 1 Kor 6:10; Kol 3:5]

25Uingiapo katika mmea wa jirani yako waweza kuyapurura masuke kwa mkono wako; ila usisogeze mundu katika mmea wa jirani yako.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania