Kutoka 13

Kutoka 13

Sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu

1BWANA akasema na Musa, akamwambia,

2Nitakasie mimi wazaliwa wa kwanza wote, kila afunguaye tumbo katika wana wa Israeli, wa binadamu na wa mnyama; ni wangu huyo.[#Hes 3:13; 8:16; 18:15; Lk 2:23; Kut 22:29,30; Law 27:26; Kum 15:19]

3Musa akawaambia hao watu, Kumbukeni siku hii, mliyotoka nchi ya Misri, kutoka nyumba ya utumwa; kwa kuwa BWANA aliwatoa mahali hapa kwa nguvu za mkono wake; na usiliwe mkate uliochachwa.[#Kut 12:42; Kum 16:3; Kut 6:1]

4Ninyi mwatoka leo katika mwezi wa Abibu.[#Kut 23:15; 34:18; Kum 16:1]

5Itakuwa hapo BWANA atakapowaleta mpaka nchi ya Wakanaani, na Wahiti, na Waamori, na Wahivi, na Wayebusi, nchi hiyo aliyowaapia baba zako kwamba atakupa wewe, ni nchi imiminikayo maziwa na asali, ndipo mtakapoushika utumishi huu katika mwezi huu.

6Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba, nayo siku ya saba itakuwa ni sikukuu ya BWANA.[#Kut 12:15,16]

7Mikate isiyochachwa italiwa katika hizo siku saba; mkate uliotiwa chachu usionekane kwako, wala chachu isionekane kwako, ndani ya mipaka yako yote.

8Nawe utamwambia mwanao siku hiyo, ukisema, Ni kwa sababu ya hayo BWANA aliyonifanyia hapo nilipotoka Misri.[#Zab 44:1]

9Nayo itakuwa ishara kwako katika mkono wako, na kwa ukumbusho kati ya macho yako, ili kwamba sheria ya BWANA ipate kuwa kinywani mwako; kwani BWANA alikuondoa utoke Misri kwa mkono wenye uwezo.[#Kut 12:14; Hes 15:39; Kum 6:8; 11:18; Isa 49:16; Yer 22:24; Mt 23:5]

10Kwa hiyo utaitunza amri hii kwa wakati wake mwaka baada ya mwaka.

Kuweka wakfu mzaliwa wa kwanza

11Itakuwa hapo BWANA atakapokuleta katika nchi ya Wakanaani, kama alivyokuapia wewe na baba zako, na kukupa,[#Mwa 15:18; 17:8; Zab 105:42-45]

12ndipo utamwekea BWANA kila afunguaye tumbo, na kila mzaliwa wa kwanza uliye naye, azaliwaye na mnyama; hao wa kiume watakuwa ni wa BWANA.[#Kut 34:19-20; Lk 2:23; Kut 22:29; Law 27:26; Hes 18:15; Eze 44:30]

13Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo; na kama hutaki kumkomboa, utamwua; na kila mzaliwa wa kwanza wa binadamu katika wanao utamkomboa.[#Hes 3:46; #13:13 Katika Kiebrania ni: kuvunja shingo.]

14Kisha itakuwa hapo mwanao atakapokuuliza kesho, akisema, Ni nini hivi? Utamwambia, BWANA alimtoa Misri, kutoka ile nyumba ya utumwa, kwa uwezo wa mkono wake;[#Kut 12:26; Kum 6:20; Yos 4:6,21]

15basi ilikuwa hapo Farao alipojifanya kuwa mgumu ili asitupe ruhusa kuondoka, BWANA akawapiga wazaliwa wa kwanza wote waliokuwa katika nchi ya Misri, wa binadamu na wa mnyama; kwa ajili ya hayo namtolea BWANA wote wafunguao tumbo, wakiwa wa kiume; lakini wazaliwa wa kwanza wote wa wana wangu nawakomboa.

16Jambo hilo litakuwa ni ishara mkononi mwako, na utepe katikati ya macho yako; kwa kuwa BWANA alitutoa Misri kwa uwezo wa mkono wake.[#Kum 6:8]

Nguzo za wingu na moto

17Ilikuwa hapo Farao alipowaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakabadili nia watu hawa hapo watakapokumbana na vita, na kurudi Misri;[#Kut 14:11; Hes 14:1; Kum 17:16]

18lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri wakiwa tayari kwa vita.[#Kut 11:2; Hes 33:6; #13:18 Katika Kiebrania ni kuelekea Bahari ya Mafunjo.]

19Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajia ninyi; nanyi mtaichukua mifupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.[#Mwa 50:25; Yos 24:32; Mdo 7:16]

20Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa lile jangwa.[#Hes 33:6]

21BWANA naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku;[#Kum 1:33; Neh 9:12,19; Zab 78:14; Isa 4:5; 1 Kor 10:1]

22ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.[#Zab 121:5-8]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania