Isaya 40

Isaya 40

Watu wa Mungu wafarijiwa

1Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu.

2Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa mkono wa BWANA adhabu maradufu kwa dhambi zake zote.

3Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye,[#Mal 3:1; Lk 1:76; Mt 3:3; Mk 1:3; Yn 1:23]

Itengenezeni nyikani njia ya BWANA;

Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu.

4Kila bonde litainuliwa,

Na kila mlima na kilima kitashushwa;

Palipoinuka patakuwa pamenyoka,

Na palipoparuza patasawazishwa;

5Na utukufu wa BWANA utafunuliwa,[#Kut 16:7; Zab 72:19; Eze 36:23; Lk 2:10]

Na watu wote watauona pamoja;

Kwa kuwa kinywa cha BWANA kimenena haya.

6Sikiliza, ni sauti ya mtu asemaye, Lia![#Yak 1:10-11; 1 Pet 1:24-25]

Nikasema,

Nilie nini? Watu wote ni majani,

Na wema wake wote ni kama ua la shambani;

7Majani yakauka, ua lanyauka;

Kwa sababu pumzi ya BWANA yapita juu yake.

Hakika watu ni majani.

8Majani yakauka, ua lanyauka;

Bali neno la Mungu wetu litasimama milele.

9Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema,

Panda juu ya mlima mrefu;

Wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema,

Paza sauti kwa nguvu;

Paza sauti yako, usiogope;

Iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu.

10Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa,[#Isa 62:11; Ufu 22:12]

Na mkono wake ndio utakaomtawalia;

Tazameni, thawabu yake i pamoja naye,

Na fidia yake i mbele zake.

11Atalilisha kundi lake kama mchungaji,[#Eze 34:15,23; Isa 49:10; Ebr 13:20; 1 Pet 2:25; Ufu 7:17; Yn 10:11]

Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake;

Na kuwachukua kifuani mwake,

Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.

12Ni nani aliyeyapima maji kwa konzi ya mkono wake, na kuzikadiria mbingu kwa shubiri, na kuyashika mavumbi ya dunia katika pishi, na kuipima milima kwa uzani, na vilima kama kwa mizani?

13Ni nani aliyemwongoza Roho ya BWANA, na kumfundisha kwa kuwa mshauri wake?[#Rum 11:34; 1 Kor 2:16]

14Alifanya shauri na nani, ni nani aliyemwelimisha na kumfunza njia ya hukumu, na kumfunza maarifa, na kumwonesha njia ya fahamu?

15Tazama, mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, huhesabiwa kuwa kama mavumbi membamba katika mizani; tazama, yeye huvinyanyua visiwa kama ni kitu kidogo sana.

16Lebanoni nao hautoshelezi kwa kuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa kafara.

17Mataifa yote huwa kama si kitu mbele zake; huhesabiwa kwake kuwa duni kabisa na batili.

18Basi, mtamlinganisha Mungu na nani? Au mtamfananisha na mfano wa namna gani?[#Mdo 17:29]

19Sanamu! Fundi mmoja huiyeyusha, na mfua dhahabu huifunika dhahabu, huifulia mikufu ya fedha.

20Yeye aliye maskini sana hata hawezi kutoa sadaka ya namna hii, huchagua mti usiooza, hujitafutia fundi stadi wa kusimamisha sanamu ya kuchonga isiyoweza kutikisika.[#Yer 10:4]

21Je! Hamkujua? Hamkusikia? Hamkuambiwa tokea mwanzo? Hamkufahamu tangu kuwekwa misingi ya dunia?[#Zab 19:1; Mdo 14:17; Rum 1:19]

22Yeye ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia, na hao wanaokaa ndani yake huwa kama panzi; yeye ndiye azitandazaye mbingu kama pazia na kuzikunjua kama hema ya kukaliwa;[#Mwa 1:1,6; Ayu 9:8; Zab 104:2; Yer 10:12]

23ndiye awatanguaye wakuu, na kuwabatilisha waamuzi wa dunia.[#Ayu 12:21]

24Naam, hawakupandwa; hawakutiwa katika ardhi kama mbegu; naam, shina lao halikutia mizizi katika ardhi; tena awapuzia tu, wakanyauka, upepo wa kisulisuli wawaondoa kama mabua makavu.

25Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye? Asema yeye aliye Mtakatifu.[#Kum 4:15; Isa 40:18; Mdo 17:24-29]

26Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake.[#Zab 147:4]

27Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, BWANA asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie?

28Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, BWANA, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki.[#Zab 147:5; Rum 11:33]

29Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.

30Hata vijana watazimia na kuchoka, na vijana wanaume wataanguka;

31bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watakimbia, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.[#Ayu 17:9; Zab 25:3; Isa 8:17; Omb 3:25; 2 Kor 4:8-10,16]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania