Yoshua Mwana wa Sira 13

Yoshua Mwana wa Sira 13

Tahadhari kuhusu Ushirikiano

1Mwenye kugusa lami atatiwa uchafu; naye mwenye kufuatana na mwenye kiburi atapata kufanana naye.

2Usijitwike mzigo upitao nguvu zako; wala usishirikiane na mtu aliye tajiri kuliko wewe. Jinsi gani chungu kushirikiana na birika? Hiyo itagonga na hicho kitavunjwa.

3Tajiri hudhulumu, akaogofya; maskini hudhulumiwa, akasihi.

4Iwapo una faida kwake, tajiri atachuma kwako; ukihitaji atakuacha.

5Kama una kitu, atakaa nawe; hata utakapofilisika, hajuti.

6Je! Ana haja nawe? Basi atakudanganya, na kukushawishi, na kukutia tumaini; atakupa maneno mazuri na kusema, Unahitaji nini?

7Naye atakutahayarisha kwa karamu zake; hata amekukumbia yote mara mbili tatu. Mwishowe atakufanyizia mzaha; atakuahirisha, na kukuacha, na kutikisa kichwa chake.

8Ujihadhari usije ukadanganyika na kufedheheshwa katika uchangamfu wako.

9Mkuu akikualika na uwe makini, hivyo atazidi kukualika.

10Usijitangulize kwake, usije ukakatazwa; wala usijitenge naye, usije ukasahauliwa.

11Usifanye kusema naye kama na mwenzako; wala usisadiki maneno yake mengi; yaani, kwa maongezi mengi atakujaribu, na kwa kukunjua uso atakupeleleza.

12Mtu asiyeficha moyoni mwake yaliyosemwa hana rehema; maana hatajizuia na kuhizi wala na kufunga;

13basi ujihadhari uwe macho, maadamu unakwenda katikati ya hatari ya kuanguka.

14-15Kila kiumbe hupenda kilichofanana nacho, na kila mwanadamu humpenda aliyefanana naye.

16Wanyama wote huandamana aina kwa aina; vile vile mwanadamu ataambatana na mmojawapo wa aina yake.

17Jinsi gani mbwamwitu ashirikiane na mwana-kondoo? Vivyo hivyo mwenye dhambi na mwenye haki.

18Kuna amani gani kati ya fisi na mbwa? Tena amani gani kati ya tajiri na maskini?

19Punda mwitu ni mawindo ya simba nyikani; ndivyo maskini walivyo malisho ya tajiri.

20Unyonge ni chukizo kwa mwenye kiburi; na umaskini ni chukizo kwa tajiri.

21Tena tajiri akitikisika huegemezwa na rafiki zake; mnyonge akiisha kuanguka husukumizwa mbali na rafiki zake.

22Tajiri akianguka, wapo wasidizi wengi; hata akinena yasiyoneneka, watu humkiri kuwa ana haki; mnyonge huanguka, na watu humshutumu; hata akitoa maneno ya hekima hakuna ampishaye.

23Tajiri anena, na wote wanyamaza na yale ayanenayo huyasifu hata mawinguni; maskini anena, nao husema, Nani huyu? Na iwapo amejikwaa, kumbe! Watazidi kumwangusha.

24Lakini utajiri pasipo dhambi ni mwema; na umaskini ni mbaya ukitoka katika ubaya.

25Moyo wa mtu hufanya kubadili uso,

Kwamba ni kwa wema au kwa ubaya.

26Uso mkunjufu hufunua moyo ulio fani;

Na kubuni mifano ni kuchosha akili.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania