Hekima ya 13

Hekima ya 13

Upumbavu wa kuabudu viumbe

1Basi, bila shaka wanadamu wote kwa asili ni ubatili, ambao hawana akili za kumtambua Mungu; tena hawakupata uwezo wa kumjua yeye aliyepo kwa kuvitazama viumbe vizuri vinavyoonekana, wala kwa kuyaangalia yaliyofanywa hawakumfahamu yule fundi aliyeyafanya.

2Lakini moto, ama upepo, ama hewa nyepesi, ama mzunguko wa nyota, ama mafuriko ya maji, ama mianga ya mbinguni walidhani kuwa ni miungu inayoutawala ulimwengu!

3Huenda ilikuwa kwa kupendezwa na uzuri wake walivyodhani viumbe hivyo kuwa ni miungu, basi na wajue kadiri gani BWANA, Mfalme wao, avipitavyo; kwa maana Yeye aliye asili ya uzuri ndiye aliyeviumba.

4Lakini kama ilikuwa kwa kuzistaajabia nguvu zake na maongozi yake, na wafahamu kwa kuviangalia kadiri gani Yeye aliyeviumba anayo nguvu zaidi;

5maana kwa jinsi uzuri hata wa viumbe vilivyoumbwa ulivyo mkuu, kwa kadiri hiyo hiyo mwanadamu huyatunga mawazo yake juu ya Muumba.

6Walakini watu hao hawana hatia nyingi. Madhali yawezekana kwamba hao wamekosea tu, pindi wanapomtafua Mungu, na kutamani kumwona;

7kwa sababu huishi katikati ya viumbe vyake, huvichunguza kwa bidii, na mwisho hujitoa kwa maono yao, mradi vitu vyenyewe wanavyovitazama ni vizuri kweli kweli.

8Walakini tena watu hao hawana udhuru.

9Kwa maana wakiwa walikuwa na uwezo wa kufahamu kadiri hiyo, hata kuweza kuchungulia taratibu ya viumbe, imekuwaje ya kwamba hawakudiriki upesi kumtambua Mfalme Mkuu wa viumbe vyake hivyo?

Upumbavu wa kuabudu sanamu

10Lakini wale wamekuwa wanyonge kabisa, ambao waliweka matumaini yao katika vitu vifu, wakiviita miungu vitu vilivyo kazi za mikono ya wanadamu; vitu vya dhahabu na fedha, vilivyofanyizwa kwa ustadi, au mifano ya wanyama, au hata jiwe la bure, kazi ya mkono wa mtu wa kale.[#Isa 44:9-20; Yer 10:1-16; Bar 6:8-73]

11Hata na mkata miti, akiisha kukata mti uwezao kuchukuliwa kwa urahisi, huondoa maganda yake yote, kisha huchonga vizuri na kufanyiza chombo kifaacho kwa matumizi ya maisha;

12kisha kuchoma takataka za kazi yake ili kukipika chakula chake, na kula na kushiba;

13kisha huchukua, katika mabaki yasiyofaa kitu, kipande cha mti kilichopotoka, tena kimejaa mafundo, hukitia nakshi kwa bidii ya ubwete wake na kukiumba kwa ustadi wa ulegevu wake; kisha hukipa umbo la sanamu ya mwanadamu,

14au kukifananisha na mnyama hafifu, akikipaka zingefuri, na kukitia rangi nyekundu, na kulifunika kila waa liliomo;

15kisha hukifanyiza chumba cha kukistahili, na kukiweka ukutani, na kukikaza kwa chuma;

16maadamu akiangalia kisianguke, kwa sababu anajua ya kwamba hakiwezi kujisaidia; mradi kwa hakika ni sanamu, inahitaji msaada!

17Basi, mwisho wa yote, anapoomba dua yake katika habari ya biashara, au harusi, au watoto, huyo haoni aibu kusema na kitu kisicho hao; naam, kuomba afya hukiitia kilicho dhaifu,

18na kuomba uhai hukisihi kile kilicho dhaifu, na kuomba msaada hukililia kisicho na ujuzi, na kuomba safari njema hukiomba kisichoweza kwenda hata hatua moja,

19na kuomba utajiri, au mapato, au kufanikiwa mikono yake, hutaka ustadi kwa kitu kile kilicho mtovu kabisa wa ustadi wa mikono!

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania