Hekima ya 18

Hekima ya 18

Nuru iliwaangaza Waisraeli

1Lakini watakatifu wako walikuwa na nuru tele; na hao Wamisri wakasikia sauti zao bila kuona sura zao, wakaihesabu kuwa vema ya kwamba wao pia wameteswa,[#Kut 13:17-22]

2ila hushukuru kwa kuwa wale waliolemewa kwanza hawawadhuru sasa, na kuwaomba waondoke.

3Hata hivyo uliwapa watu wako nguzo ya moto uliowaka, ili kuwa kiongozi wakienda wasikojua, na jua la kuwafadhili katika uhamisho wao wenye heshima.

4Kwa maana hao Wamisri walistahili sana kunyimwa nuru na kufungwa gizani, mradi hao walikuwa wamewafunga watoto wako kwa nguvu, ambao kwa nuru isiyoharibika ya torati itatolewa kati ya wanadamu.

Kifo cha wazaliwa wa kwanza wa Wamisri

5Hata walipokuwa wameshauriana kuwaua watoto wachanga wa watakatifu wako, na mtoto fulani ametupwa, na kuokolewa ili kuwahukumu, uliwaondolea wingi wa watoto wao, na kuwaangamiza jeshi lao katika mafuriko makuu.

6Usiku ule baba zetu walitangulia kuonywa, ili wakiwa na ufahamu hakika, wafurahishwe na viapo walivyovitegemia;

7kwa hiyo watu wako waliutazamia wokovu wa wenye haki na uharibifu wa adui.

8Madhali uliwalipiza kisasi watesi wale, na kwa njia ile ile uliwatukuza ukituita ili tukujie.

9Zaidi ya hayo watoto watakatifu wa watu wema walitoa dhabihu kwa siri, na kwa moyo mmoja walijitwalia agano la torati ya dini, ya kwamba watashirikiana katika mambo mema na vile vile katika hatari; pindi walipoimbisha nyimbo takatifu za mababu katika kumhimidi Mungu.

10Lakini adui wakaitika sauti zisizolingana, wakaeneza malalamiko ya kuhuzunisha kwa ajili ya watoto wao;

11mtumwa pamoja na bwana wake wakaadhibiwa kwa adhabu ya haki sawasawa, na raia pamoja na mfalme,

12naam, wote pamoja chini ya namna moja ya kifo, wakawa na maiti pasipo idadi; hata waliokuwa hai hawakutosha ili kuwazika, maana kwa pigo moja wazao wao waliopendwa hasa waliangamizwa.

13Na maadamu wasiposadiki mambo yote kwa sababu ya uchawi, kwa kuangamia watoto wa kwanza wao walikiri kuwa taifa hili, Israeli, ni mtoto wa Mungu.

14Kwa maana majira mambo yote yalipokuwa kimya, na usiku ulikuwa katikati ya mwendo wake mwepesi.

15Neno lako Mwenyezi alishuka mbinguni kutoka kiti chao cha kifalme, shujaa aliye hodari, katika nchi iliyopasishwa hukumu, mwenye upanga mkali, ndio amri yako isiyopindika,

16akasimama na kujaza mambo yote mauti, na pindi alipogusa mbingu akaikanyaga nchi.

17Mara maono ya ndoto zao yakawafadhaisha sana, na maogofya yasiyotazamiwa nao yakawajia;

18na kila mtu, mmoja huko na mmoja huko, ameanguka nusu ya kufa, akaonesha sababu ya kifo chake;

19mradi zile ndoto zilizowahangaisha zikadhihirisha hiyo, ili wasipotee bila kutambua sababu ya kuteswa kwao.

Tisho la kuangamia katika jangwa

20Kadhalika iliwapasa wenye haki nao kuionja mauti, na wengi wao walipigwa jangwani; ila hasira ile haikudumu sana[#Hes 16:41-50]

21kwa sababu Haruni, mtu mnyofu, alifanya haraka kuwa mjasiri wao. Huyo alileta silaha za utumishi wake, sala na kipatanisho cha uvumba, akaipinga hasira ile na kuukomesha msiba, akajionesha kuwa ni mtumishi wako.

22Akamshinda mwenye hasira, si kwa nguvu za mwilini wala kwa mafaa ya silaha, ila kwa neno akamtuliza yeye aliyekuwa akiwaadhibu, kwa kukumbusha viapo na maagano waliyopewa mababu.

23Kwa maana wafu walipokwisha kuanguka mafungu mafungu hata kulundika alisimama katikati, akaipinga njia mbele ya hasira, akaizuia isiwafikie waliokuwa hai.

24Madhali juu ya vazi lake refu ulikuwapo ulimwengu, na sifa za mababu zilikuwapo juu ya mchoro wa safu nne za vito, na enzi yako juu ya kilemba kichwani pake.

25Mambo hayo mharabu aliyaondokea, na watu waliyaacha; maana ilitosha kuonja tu hasira ile.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania