Baruku 3

Baruku 3

1“Ee Bwana, Mungu Mwenye Nguvu, Mungu wa Israeli, tunakulilia wewe kwa moyo uliotaabika na hoi.

2Usikilize ee Bwana, na utuhurumie, maana sisi tumetenda dhambi mbele yako.

3Wewe wadumu milele, lakini sisi, tumeangamia milele!

4Ee Bwana, Mwenye Nguvu, Mungu wa Israeli! Usikilize sasa sala ya Waisraeli walio kama wafu, sala ya hao waliokukosea, waliokataa kutii sauti yako wewe Bwana Mungu wao, hata balaa zikatuandama.

5Usikumbuke maovu ya wazee wetu, bali ukumbuke uwezo wako na jina lako.

6Wewe ni Bwana Mungu wetu, nawe ndiwe tutakayekusifu peke yako.

7Wewe umeweka mioyoni hali ya uchaji wako ili tupate kukuomba kwa jina lako. Sisi tutakusifu huku uhamishoni tuliko, maana tumeweka mbali nasi uovu wote wa wazee wetu waliokukosea.

8Tazama, sisi sasa tumo uhamishoni ambamo wewe umetutawanya, tudharauliwe, tulaaniwe na kuadhibiwa kwa sababu ya maovu yote ya wazee wetu ambao walikuacha wewe Bwana Mungu wetu.”

Hekima mwongozo wa Israeli

9Sikiliza amri za uhai, ewe Israeli!

Tega sikio, ukajifunze hekima!

10Imekuwaje, ee Israeli,

imekuwaje uko nchini mwa maadui zako;

kwamba umezeeka katika nchi ya kigeni

na kutiwa unajisi kwa maiti?

11Imekuwaje umehesabiwa pamoja na walio kuzimu?

12Wewe umeiacha chemchemi ya Hekima.

13Kama ungalifuata njia ya Mungu

ungalikuwa unaishi kwa amani milele.

14Jifunze palipo na Hekima,

mahali penye nguvu,

mahali penye maarifa, upate kugundua penye maisha marefu na uhai,

penye mwanga wa kuangazia macho na penye amani.

15Nani amewahi kugundua alipo Hekima,

Nani aliyefaulu kuingia katika ghala zake?

16Wako wapi watawala wa mataifa,

wale watawalao wanyama duniani kwa mabavu?

17Wako wapi wale wachezao na ndege wa angani,

wenye kurundika fedha na dhahabu

ambazo watu huzitegemea,

hata hawatosheki kuzitafuta?

18Wapi waliopanga na kuhangaika kupata fedha tu

na ambao kazi zao hazikuacha alama yoyote?

19Wote hao watoweka na kuishia chini kuzimu,

na wengine wamezuka mahali pao.

20Kizazi kipya kimeikalia nchi,

nacho pia kikauona mwanga wa mchana,

lakini hakikujifunza njia ya maarifa

wala hakikuzijua njia zake, wala hakikufaulu kumpata Hekima.

21Wazawa wake walipotoka njiani mwa Hekima.

22Hekima hajapata kusikika Kanaani,

wala kuonekana katika Temani.

23Wazawa wa Hagari watafutao maarifa duniani,

wafanyabiashara wa Merani na Temani,

wasimulizi wa visa na wenye kutafuta maarifa,

hawajajifunza njia ya Hekima,

hawajui chochote juu ya njia zake.

24Ee Israeli, jinsi gani ilivyo kubwa nyumba ya Mungu!

Na jinsi gani ilivyo kubwa nchi anayomiliki!

25Ni kubwa na haina mipaka,

haina kimo na haipimiki.

26Majitu maarufu ya kale yalizaliwa humo;

watu wakubwa kwa kimo na stadi vitani.

27Mungu hakuwateua hao

wala kuwajulisha njia ya maarifa.

28Hivyo waliangamia kwa kutokuwa na hekima;

waliangamia kwa upumbavu wao wenyewe.

29Nani aliyepanda mbinguni akamchukua Hekima,

akamleta chini kutoka mawinguni?

30Nani aliyewahi kusafiri baharini na kumpata?

Nani awezaye kumnunua kwa dhahabu?

31Hakuna mtu ajuaye njia ya kwenda kwake,

wala anayejali njia iendayo kwake.

32Lakini yeye ajuaye kila kitu anamjua Hekima,

alimpata kutokana na maarifa yake.

Yeye aliyeitayarisha dunia tangu milele

aliijaza viumbe vyenye miguu minne.

33Yeye huutuma mwanga nao huenda;

aliuita nao ukamtii kwa hofu.

34Nyota huangaza mahali pao kwa furaha,

yeye huziita nazo husema, “Tupo hapa”.

Huangaza kwa furaha kwa ajili yake yeye aliyeziumba.

35Huyu ni Mungu wetu,

hakuna awezaye kulinganishwa naye.

36Mungu aliigundua njia yote ya maarifa

akampatia Yakobo mtumishi wake,

naam, akampatia Israeli aliyempenda.

37Baadaye Hekima alitokea duniani

akaishi pamoja na binadamu.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania