The chat will start when you send the first message.
1Baada ya kula, wazazi wa Sara walimwongoza kijana Tobia chumbani kwa bibiarusi.
2Tobia alikumbuka maagizo ya Rafaeli. Basi, akafungua mfuko wake, akatoa ini na moyo wa samaki, akaviweka juu ya moto wa ubani; moshi ukafuka.
3Harufu yake ikalitimulia mbali lile jini, likakimbilia Misri. Rafaeli akalifuatia huko na bila kukawia akalikaba na kulifunga.
4Basi Tobia na Sara walibaki peke yao chumbani baada ya wale wazazi kwenda zao na milango kufungwa. Kisha Tobia aliondoka kitandani, akamwambia mkewe, “Inuka, dada, tumwombe Bwana atuonee huruma na kutukinga salama.”
5Sara akainuka. Tobia akaanza kusali:
“Utukuzwe ee Mungu wa wazee wetu.
Jina lako lisifiwe milele na milele.
Mbingu zikutukuze,
navyo viumbe vyako vyote,
milele na milele.
6Ndiwe uliyemuumba Adamu;
ndiwe uliyemuumba Hawa mkewe,
amsaidie na kumtegemeza.
Binadamu wote wametokana na hao wawili.
Ndiwe uliyesema:
Si vizuri mwanamume kuwa peke yake;
Tumuumbe mtu wa kumsaidia aliye kama yeye.
7Kwa hiyo namchukua dada yangu
si kwa sababu ya tamaa ya mwili
ila nafanya hivyo kwa dhamiri safi.
Uwe na huruma kwake na kwangu
utufikishe uzeeni pamoja!”
8Wote wawili wakaitikia, “Amina! Amina.”
9Kisha wakalala usiku huo.
Wote walipokuwa usingizini, Ragueli akaamka, akawaita watumishi wake, akaenda nao kuchimba kaburi,
10maana aliwaza, “Labda na huyo atakufa, na watu watatucheka na kutudhihaki!”
11Walipomaliza kuchimba kaburi, Ragueli akaingia nyumbani na kumwambia mkewe,
12“Umtume mtumishi mmoja wa kike akapeleleze kama Tobia angali hai. Kama amekufa, basi, tumzike kabla watu hawajagundua.”
13Basi, huyo mtumishi alichukua taa, akafungua mlango wa kuingia chumbani kwao. Aliwakuta wote wawili wamelala fofofo.
14Basi, akarudi na kuwaarifu Ragueli na Edna kwamba Tobia alikuwa bado hai.
15Hapo Ragueli akamtukuza Mungu wa mbinguni kwa maneno haya:
“Utukuzwe ewe Mungu wangu
kwa sifa za mioyo safi!
Utukuzwe milele na milele.
16Utukuzwe kwa sababu umenifurahisha.
Lile nililohofia halikutukia;
badala yake umetuonesha huruma yako kuu.
17Utukuzwe kwa sababu umewarehemu vijana hao wawili
watoto wa pekee kwa wazazi wao.
Uwajalie ee Bwana huruma na kinga yako;
uwajalie maisha ya upendo na furaha.”
18Halafu Ragueli akaamuru watumishi wake wafukie lile kaburi kabla jua halijachomoza.
19Kisha Ragueli akamwambia mkewe aoke mikate, naye mwenyewe akaenda akachagua ng'ombe wawili na kondoo wanne kutoka kundi la mifugo yake akampata mtumishi atayarishe karamu.
20Ragueli alimwita Tobia, akamwambia, “Sipendi kusikia juu ya safari yako mpaka baada ya majuma mawili. Utakaa papa hapa ule na kunywa pamoja nami, umfurahishe binti yangu baada ya taabu zote alizopata.
21Baada ya hapo, utachukua nusu ya mali yangu na kumchukua Sara salama mpaka kwa wazazi wako. Mimi na Edna tutakapofariki utapata ile nusu ya mali yangu iliyobaki. Jipe moyo mwanangu! Tangu sasa mimi ni baba yako na Edna ni mama yako. Tutakuwa wazazi wako hata baadaye kama tulivyo wazazi wa Sara. Jipe moyo mwanangu!”