1 Yohana 2

1 Yohana 2

Mwombezi kwa Baba.

1Ninyi vitoto, mlio wangu, haya nawaandikiani, msikose. Lakini kama yuko aliyekosa, tunaye mwombezi kwa Baba, ndiye Yesu Kristo aliye mwongofu.[#Rom. 8:34; Ebr. 7:25.]

2Naye ndiyo kole iliyotolewa kwa ajili ya makosa yetu, lakini si kwa ajili ya makosa yetu tu, ila hata kwa ajili ya makosa ya ulimwengu wote.[#Kol. 1:20.]

3Namo humu ndimo, tutambuamo, ya kuwa tumemtambua, tukiyashika maagizo yake.

4Mtu akisema: Nimemtambua, lakini maagizo yake hayashiki, mtu huyo ni mwongo, nayo kweli haimo mwake.

5Lakini mtu akilishika Neno lake, mwake yeye upendo wa Mungu umetimia kweli. Humu ndimo, tutambuamo, kama tumo mwake.[#Yoh. 14:21,23.]

6Mtu anayesema: Nafuliza kuwa mwake, huyo inampasa kufanya mwenendo, kama yeye alivyofanya mwenendo.[#Yoh. 13:15; 1 Petr. 2:22.]

Agizo jipya.

7Wapendwa, siwaandikii agizo jipya, ila agizo la kale, mlilokuwa nalo tangu mwanzo. Agizo hilo la kale ndilo Neno, mlilosikia.[#1 Yoh. 1:5; Yoh. 13:34; 2 Yoh. 5.]

8Tena nawaandikia agizo jipya lililo kweli mwake namo mwenu ninyi, kwamba: Giza hupita, nao mwanga wa kweli umekwisha kumulika.[#Yoh. 13:34; Rom. 13:12.]

9Mtu akisema: Nimo mwangani, akamchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa hivi.[#1 Yoh. 4:20.]

10Mwenye kumpenda ndugu yake hukaa mwangani, asiwe na kwazo lililomo mwake.

11Lakini mwenye kumchukia ndugu yake yumo gizani na kuendelea gizani, asijue, anakokwenda, kwani giza imempofusha macho yake.

Msiupende ulimwengu huu!

12Nawaandikia ninyi mlio vitoto, kwani mmeondolewa makosa yenu kwa ajili ya jina lake.

13Nawaandikia ninyi mlio baba, kwani mmemtambua yeye aliye mwenye kuwapo tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi mlio vijana, kwani mmemshinda yule Mbaya.

14Naliwaandikia ninyi mlio wana, kwani mmemtambua Baba. Naliwaandikia ninyi mlio baba, kwani mmemtambua yeye aliye mwenye kuwapo tangu mwanzo. Naliwaandikia ninyi mlio vijana, kwani mko na nguvu, hata Neno la Mungu linakaa mwenu, nanyi mmemshinda yule Mbaya.[#Ef. 6:10.]

15Msiupende ulimwengu huu, wala vilivyomo ulimwenguni! Mtu akiupenda ulimwengu huu, upendo wa Baba haumo mwake huyo.[#Yak. 4:4.]

16Kwani vyote vilivyomo ulimwenguni: tamaa za miili nazo tamaa za macho nayo mambo makuu, watu wanayojivunia, havikutoka kwake Baba, ila ulimwenguni.

17Ulimwengu huu utapita pamoja na tamaa zake; lakini ayafanyaye, Mungu ayatakayo, hukaa kale na kale.*

Mpinga Kristo.

18Vitoto, sasa ni saa ya mwisho. Kama mlivyosikia, ya kuwa Mpinga Kristo anakuja, sasa wapinga Kristo wamekwisha kuwapo wengi; kwa hiyo twatambua, ya kuwa ni saa ya mwisho.[#Mat. 24:5,24; 2 Tes. 2:3-4.]

19Walitoka kwetu sisi, lakini hawakuwa wa kwetu; kwani kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka, kusudi waonekane waziwazi, ya kuwa hao wote sio wa kwetu.[#Tume. 20:30.]

20Nanyi mmemiminiwa mafuta naye aliye Mtakatifu, mkayajua yote.[#1 Yoh. 2:27; Yoh. 16:13.]

21Sikuwaandikia ninyi, kwa sababu hamkuyajua yaliyo ya kweli, ila kwa sababu mmeyajua, tena mmejua, ya kuwa hakuna uwongo utokao kwenye ukweli.

Anayemkana Mwana hanaye Baba vilevile.

22Tena yuko nani aliye mwongo, asipokuwa yeye anayekana kwamba: Yesu siye Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo anayemkana Baba na Mwana.

23Kila anayemkana Mwana hata Baba hanaye vilevile; lakini anayemwungama Mwana anaye hata Baba.[#1 Yoh. 4:15; Yoh. 5:23; 1 Yoh. 2:7.]

24Nanyi mliyoyasikia tangu mwanzo, sharti yakae mwenu! Hayo, mliyoyasikia tangu mwanzo, yakikaa mwenu, hata ninyi mtakaa mwake Mwana namo mwake Baba.

25Nacho kiagio, alichotuagia mwenyewe, ndicho hiki: uzima wa kale na kale.

26Haya nimewaandikia ninyi kwa ajili yao wanaowapoteza.[#1 Yoh. 2:20; Yer. 31:34; Yoh. 16:13; 2 Kor. 1:21-22.]

27Yale mafuta, mliyomiminiwa naye, huwakalia, msifundishwe tena na mtu; ila kama mafuta yake yalivyowafundisha mambo yote, ndivyo, yalivyo kweli, huu si uwongo. Kwa hiyo yakalieni, kama yalivyowafundisha ninyi.

28Sasa, vitoto, kaeni mwake yeye, tupate kushangilia, atakapotokea waziwazi, tusipatwe na soni naye hapo, atakaporudi![#1 Yoh. 4:17.]

29Mkijua, ya kuwa yeye ni mwongofu, na mtambue, ya kuwa kila anayefanya wongofu amezaliwa naye yeye![#1 Yoh. 3:7,10.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania