1 Yohana 3

1 Yohana 3

Sisi tu wana wa Mungu.

1*Tazameni, jinsi Baba alivyotupenda sana, tuitwe watoto wa Mungu! Nasi ndio. Kwa hiyo ulimwengu haututambui, kwani haukumtambua yeye.[#Yoh. 1:12-13; 16:3.]

2Wapendwa, sasa tu watoto wa Mungu, lakini havijafunuliwa bado, tutakavyokuwa; twajua tu, ya kuwa vitakapofunuliwa tutafanana naye, tumwone, alivyo.[#Rom. 8:17; 1 Kor. 15:49; Kol. 3:4.]

3Kila mwenye kumngojea hivyo hujing'aza, kama yeye alivyo mng'avu.

4Kila mwenye kukosa hukataa kuonyeka, nako kukosa ndiko kukataa kuonyeka.

5Nanyi mwajua, ya kuwa yule ametokea waziwazi, ayaondoe makosa, maana mwake yeye hamna kosa.*[#Yes. 53:4-5,9; 1 Petr. 2:24.]

6Kila mwenye kukaa mwake hakosi; lakini kila mwenye kukosa hakumwona yeye, wala hakumtambua.[#1 Yoh. 3:24; Rom. 6:14; 2 Kor. 5:17; 3 Yoh. 11.]

7Vitoto, pasioneke mwenye kuwapoteza! Mwenye kufanya wongofu ni mwongofu, kama yeye alivyo mwongofu.[#1 Yoh. 2:29.]

8Mwenye kukosa ametoka kwake Msengenyaji, kwani Msengenyaji hukosa tangu mwanzo. Kwa hiyo mwana wa Mungu alitokea waziwazi, azivunje kazi zake Msengenyaji.[#Yoh. 8:44.]

9Kila aliyezaliwa naye Mungu hakosi, kwani mbegu zake hukaa mwake; kwa hiyo hawezi kukosa, maana alizaliwa naye Mungu.[#1 Yoh. 3:6; 5:18; Rom. 6:11.]

10Hapo ndipo panapoonekana wazi walio watoto wa Mungu nao walio watoto wa Msengenyaji: kila asiyefanya wongofu hakutoka kwake Mungu, naye asiyempenda ndugu yake vilevile.

11Kwani huu ndio utume, mliousikia tangu mwanzo: Tupendane sisi kwa sisi![#Yoh. 13:34.]

12Tusiwe kama Kaini aliyekuwa wa yule Mbaya, akamwua nduguye. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yeye yalikuwa mabaya, lakini yake nduguye yalikuwa yenye wongofu.[#1 Mose 4:8.]

Anayemchukia ndugu yake ni mwua watu.

13*Msistaajabu, ndugu, ulimwengu ukiwachukia ninyi![#Mat. 5:11; Yoh. 15:18-19.]

14Sisi twajua, ya kuwa tumetoka kwenye kufa na kuingia kwenye uzima, kwani twawapenda ndugu; asiyewapenda yuko kufani bado.[#1 Yoh. 2:11; Yoh. 5:24.]

15Kila amchukiaye ndugu yake ni mwua watu, nanyi mwajua: hakuna mwua watu aliye mwenye uzima wa kale na kale, atakaoukalia.[#Mat. 5:21-22.]

16Hapo ndipo, tulipoutambua upendo: Yeye aliitoa roho yake kwa ajili yetu; nasi imetupasa kuzitoa roho zetu kwa ajili ya ndugu.[#Yoh. 15:13.]

17Lakini mtu mwenye mali za humu ulimwenguni akimtazama tu ndugu yake aliyekosa chakula, akamfungia moyo ake, asimgawie, upendo wa Mungu unamkaliaje?[#1 Yoh. 4:20; 5 Mose 15:7.]

18Vitoto, tusipendane kwa maneno, wala kwa ndimi, ila kwa matendo na kwa kweli!*[#Yak. 1:22; 2:15-16.]

19Hapo tutatambua, kama sisi tu wenye kweli, tena hivyo tutaituliza mioyo yetu mbele yake yeye.

20Kwani mioyo yetu ikituchafukia, Mungu ni mkubwa kuliko mioyo yetu, naye huyatambua yote.

21Wapendwa, mioyo yetu isipotuchafukia, sisi humshangilia Mungu.[#Rom. 5:1-2; Ebr. 4:16.]

22Ndipo, tutakapopewa naye lolote, tutakaloliomba, kwani twayashika maagizo yake kwa kuyafanya yanayompendeza.[#Mar. 11:24.]

23Hili ndilo agizo lake, tulitegemee Jina la Mwana wake Yesu Kristo na kupendana sisi kwa sisi, kama yeye alivyotuagiza.[#Yoh. 6:29; 15:17.]

24Naye mwenye kuyashika maagizo yake hukaa mwake yeye, naye yeye mwake huyo. Hapo twatambua, ya kuwa yumo mwetu, tukiwa na Roho, aliyetupa sisi.[#1 Yoh. 4:13; Rom. 8:9.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania