The chat will start when you send the first message.
1Mfalme Dawidi alipokuwa mzee kwa kuendelea sana kuwa mwenye siku nyingi, wakamfunika kwa nguo, lakini hakupata joto.
2Ndipo, watumishi wake walipomwambia: Sharti wamtafutie bwana wetu mfalme kijana aliye mwanamwali wa kusimama mbele ya mfalme na kumtunza. Naye akilala kifuani pako, bwana wetu mfalme, utapata joto.
3Wakatafuta msichana aliyekuwa mzuri kuwashinda wengine waliokuwa mipakani kwa Waisiraeli, wakamwona Abisagi wa sunemu, wakampeleka kwake mfalme.
4Huyu msichana alikuwa mzuri mno, akawa mtunzaji wa mfalme, akamtumikia, lakini mfalme hakumjua.
5Naye Adonia, mwana wa Hagiti, akajikweza kwamba: Mimi nitakuwa mfalme, akajipatia magari na farasi na watu 50, wamtangulie kwa kupiga mbio.[#2 Sam. 3:4; 15:1.]
6Lakini baba yake hakumsikitisha tangu siku zake za kale kwamba: Mbona unafanya kama hayo? Naye kwa kutazamwa alikuwa mtu mzuri mno, naye mama yake alimzaa baada ya Abisalomu.
7Akapiga shauri na Yoabu, mwana wa Seruya, tena na mtambikaji Abiatari, wakamsaidia kwa kurudi upande wake Adonia.[#1 Fal. 2:22.]
8Lakini mtambikaji Sadoki na Benaya, mwana wa Yoyada, na mfumbuaji Natani na Simei na Rei na mafundi wa vita wa Dawidi hawakuwa upande wake Adonia.
9Kisha Adonia akatambika penye Jiwe la Zoheleti (Mwamba wa Nyoka) karibu na Eni-Rogeli (Chemchemi ya Wafua nguo) na kuchinja kondoo na ng'ombe na vinono, akawaalika ndugu zake wote waliokuwa wana wa mfalme wa waume wote wa Yuda waliomtumikia mfalme.[#Yos. 15:7.]
10Lakini mfumbuaji Natani na Benaya nao mafundi wa vita naye ndugu yake Salomo hakuwaalika.
11Ndipo, Natani alipomwambia Bati-Seba, mamake Salomo, kwamba: Hukusikia, ya kuwa Adonia, mwana wa Hagiti, amejipa ufalme, bwana wetu Dawidi asivijue?
12Sasa nitakupa shauri upate kujiponya mwenyewe pamoja na roho yake mwanao Salomo.
13Nenda, uingie mwake mfalme Dawidi, umwambie: Je? Wewe, bwana wangu mfalme, hukumwapia kijakazi wako kwamba: Mwanao Salomo atakuwa mfalme nyuma yangu, yeye akae katika kiti changu cha kifalme? Mbona Adonia amekwisha kujipa ufalme?
14Ukiwa hujamaliza bado kusema mle na mfalme, utaniona mimi, nikiingia nyuma yako, niyamalize maneno yako.
15Ndipo, Bati-Seba alipoingia chumbani mwake mfalme, naye mfalme alikuwa mzee sana, naye Abisagi wa Sunemu alimtumikia mfalme.
16Bati-Seba akainama na kumwangukia mfalme; mfalme akamwuliza: Una nini?
17Akamwambia: Bwana wangu, wewe ulimwapia kijakazi wako na kumtaja Bwana Mungu wako kwamba: Mwanao Salomo atakuwa mfalme nyuma yangu, yeye akae katika kiti changu cha kifalme.
18Lakini sasa tazama, Adonia amekwisha kujipa ufalme, nawe bwana wangu mfalme huvijui!
19Akatambika na kuchinja ng'ombe na vinono na kondoo wengi, akawaalika wana wote wa mfalme na mtambikaji Abiatari na Yoabu, mkuu wa vikosi, lakini mtumwa wako Salomo hakumwalika.[#1 Fal. 1:9-10.]
20Nawe, bwana wangu mfalme, macho ya Waisiraeli wote yanakuelekea wewe, uwaambie, kama ni nani atakayekaa katika kiti cha kifalme cha bwana wangu mfalme nyuma yake.
21Hivyo itakuwa, bwana wangu mfalme atakapolala na baba zake, mimi na mwanangu Salomo tuwe wakosaji.[#2 Mose 5:16.]
22Alipokuwa akisema bado na mfalme, mara mfumbuaji Natani akaja.
23Wakamwambia mfalme kwamba: Mfumbuaji Natani amekuja. Alipokuja mbele ya mfalme, akamwangukia mfalme na kuufikisha uso wake chini.
24Kisha Natani akasema: Bwana wangu mfalme, umesema: Adonia awe mfalme nyuma yangu, naye akae katika kiti changu cha kifalme?
25Kwani siku hii ya leo ameshuka, akatambika na kuchinja ng'ombe na vinono na kondoo wengi, akaalika wana wote wa mfalme na wakuu wa vikosi na mtambikaji Abiatari, nao wamo katika kula na kunywa mbele yake wakisema: Pongezi, mfalme Adonia![#2 Sam. 16:16.]
26Lakini mimi niliye mtumwa wako na mtambikaji Sadoki na Benaya, mwana wa Yoyada, na mtumwa wako Salomo hakutualika.[#1 Fal. 1:10.]
27Inakuwaje? Neno hilo limetoka kwako, bwana wangu mfalme, usimjulishe mtumwa wako, kama ni nani atakayekaa katika kiti cha kifalme cha bwana wangu mfalme nyuma yake?
28Mfalme Dawidi akajibu akisema: Niitieni Bati-Seba! Alipokuja mbele ya mfalme na kusimama mbele ya mfalme,
29ndipo, mfalme alipoapa akisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyeiokoa roho yangu katika masongano yote,
30siku hii ya leo nitavifanya, nilivyokuapia na kumtaja Bwana Mungu wa Isiraeli kwamba: Mwanao Salomo atakuwa mfalme nyuma yangu, yeye akae katika kiti changu cha kifalme mahali pangu.
31Bati-Seba akauinamisha uso chini, akamwangukia mfalme akisema: Bwana wangu mfalme Dawidi na awepo uzimani kale na kale!
32Kisha mfalme Dawidi akasema: Niitieni mtambikaji Sadoki na mfumbuaji Natani na Benaya, mwana wa Yoyada! Walipokuja mbele ya mfalme,
33mfalme akawaambia: Wachukueni watumishi wa bwana wenu kwenda nanyi, mkimpandisha mwanangu Salomo katika nyumbu wangu mimi, mmtelemshe huko Gihoni!
34Huko mtambikaji Sadoki na mfumbuaji Natani wampake mafuta, awe mfalme wa Waisiraeli. Kisha mtapiga mabaragumu kwamba: Pongezi, mfalme Salomo!
35Baadaye mtampandisha kufika huku, aje kukaa katika kiti changu cha kifalme, yeye awe mfalme mahali pangu. Yeye ndiye, niliyemwagiza kuwa mtawalaji wa Waisiraeli na wa Wayuda.
36Benaya, mwana wa Yoyada, akamwitikia mfalme akisema: Amin. Naye Bwana Mungu wa bwana wangu mfalme na aseme hivyo!
37Kama Bwana alivyokuwa na bwana wangu mfalme, vivyo hivyo na awe naye Salomo akikikuza kiti chake cha kifalme kuliko kiti cha kifalme cha bwana wangu mfalme Dawidi!
38Mtambikaji Sadoki na mfumbuaji Natani na Benaya, mwana wa Yoyada, na Wakreti na Wapuleti wakashuka, wakampandisha Salomo katika nyumbu wa mfalme Dawidi, wakampeleka Gihoni.[#2 Sam. 8:18.]
39Naye mtambikaji Sadoki alikuwa ameichukua pembe ya mafuta mle Hemani, akampaka Salomo mafuta; ndipo, walipopiga mabaragumu, nao watu wote wakasema: Pongezi, mfalme Salomo![#1 Mambo 23:1; 29:22.]
40Kisha watu wote pia wakapanda na kumfuata wakipiga filimbi kwa kufurahi furaha kubwa, hata nchi ikavuma kwa sauti zao kuu.
41Adonia nao watu walioalikwa naye waliokuwa naye walipovisikia walikuwa wamekwisha kula. Yoabu alipozisikia sauti za mabaragumu akauliza: Makelele na mavumo ya mjini ni ya nini?
42Alipokuwa akisema bado, mara akaja Yonatani, mwana wa mtambikaji Abiatari; Adonia akamwambia: Njoo! Kwani wewe u mtu mwenye nguvu, utatuletea habari njema.[#2 Sam. 15:27,36.]
43Lakini Yonatani akajibu akimwambia Adonia: Sivyo! Bwana wetu mfalme Dawidi amempa Salomo kuwa mfalme!
44Mfalme akatuma pamoja naye mtambikaji Sadoki na mfumbuaji Natani na Benaya, mwana wa Yoyada, na Wakreti na Wapuleti, wakampandisha katika nyumbu wa mfalme.
45Mtambikaji Sadoki na mfumbuaji Natani wakampaka mafuta kule Gihoni, awe mfalme, kisha wakapanda kutoka huko wenye furaha, mji ukavuma; hizo ndizo sauti, mlizozisikia.
46Kisha Salomo akapata hata kukaa katika kiti cha kifalme.[#1 Mambo 28:5.]
47Hata watumishi wa mfalme wamekwisha kwenda kumpongeza bwana wetu mfalme Dawidi wakisema: Mungu wako na alitukuze jina la Salomo kuliko jina lako! Tena kiti chake cha kifalme na akikuze kuliko kiti chako cha kifalme! Ndipo, mfalme alipojiinamisha kitandani pake,
48naye mfalme akasema kama haya: Bwana Mungu wa Isiraeli na atukuzwe, kwa kuwa leo amemtoa atakayekaa katika kiti changu cha kifalme, macho yangu yakiviona![#1 Fal. 3:6.]
49Ndipo, wote walioalikwa waliokuwa kwake Adonia waliposhikwa na woga, wakaondoka, wakajiendea, kila mtu akishika yake njia.
50Adonia akamwogopa Salomo, akaondoka, akaenda, akazishika pembe za meza ya Bwana.
51Salomo akapashwa habari kwamba: Tazama, Adonia anamwogopa mfalme Salomo! Tazama, amezishika pembe za meza ya Bwana akisema: Mfalme Salomo sharti aniapie leo, asimwue mtumwa wake kwa upanga![#1 Fal. 2:28.]
52Salomo akasema: Kama atakuwa mtu mwelekevu, unywele wake mmoja tu hautaanguka chini; lakini ukionekana ubaya kwake, atakufa.[#2 Sam. 14:11.]
53Mfalme Salomo akatuma, wamshushe penye meza ya Bwana; ndipo, alipokuja, akamwangukia mfalme Salomo, Salomo akamwambia: Nenda nyumbani mwako!