1 Wafalme 10

1 Wafalme 10

Mfalme wa kike wa Saba anamwamkia Salomo.

(1-28: 2 Mambo 9:1-28.)

1Mfalme wa kike wa Saba alipousikia uvumi wa Salomo nayo, aliyolifanyia Jina la Bwana, akaenda kumjaribu kwa maulizo ya kufumbafumba.[#Mat. 12:42.]

2Akaja Yerusalemu na vikosi vikubwa mno na ngamia waliochukua uvumba na dhahabu nyingi sana na vito. Alipofika kwa Salomo akasema naye na kumwuliza yote, aliyokuwa nayo moyoni mwake.

3Salomo akamwelezea yote, aliyomwuliza, halikuwako neno lililofichika maana kwake mfalme, asiloweza kumwelezea.

4Ndipo, mfalme wa kike wa Saba alipouona werevu wa Salomo kuwa wa kweli, kisha akaitazama nyumba,

5aliyoijenga, na vilaji vilivyopo mezani na vikao vya watumwa wake na kazi za watumishi wake na mavazi yao na watunza vinywaji wake na ng'ombe zake za tambiko za kuteketezwa nzima, alizozipeleka Nyumbani mwa Bwana, ndipo, roho yake ilipozimia,

6akamwambia mfalme: Kumbe ni ya kweli, niliyoyasikia katika nchi yangu ya mambo yako na ya werevu wako ulio wa kweli!

7Lakini sikuyaitikia hayo maneno kuwa ya kweli, mpaka nikija, nikayaona kwa macho yangu. Tena naona, ya kuwa sikuambiwa nusu tu, unauzidisha werevu wa kweli na wema, ni mkuu kuliko ule uvumi, niliousikia.

8Wenye shangwe ni watu wako, nao hawa watumwa wako ni wenye shangwe kwa kusimama mbele yako siku zote na kuyasikia maneno ya werevu wako ulio wa kweli.[#Luk. 10:23.]

9Bwana Mungu wako na atukuzwe, kwa kuwa alipendezwa na wewe, akakukalisha katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli. Kwa kuwa Bwana anawapenda Waisiraeli kale na kale, alikuweka kuwa mfalme wao, uwaamue kwa wongofu.[#1 Fal. 5:7.]

10Kisha akampa mfalme vipande vya dhahabu 120, ndio frasila 360, na uvumba mwingi sana na vito; uvumba mwingi kama huo, mfalme wa kike wa Saba aliompa mfalme Salomo, ulikuwa haujaingia huko bado.

11Kweli hata merikebu za Hiramu zilizochukua dhahabu huko Ofiri zikaleta toka Ofiri nayo miti ya uvumba mingi sana na vito.[#1 Fal. 9:27-28.]

12Naye mfalme akaitumia hiyo miti ya uvumba ya kuzikingia baraza za Nyumba ya Bwana na za nyumba ya mfalme na ya kutengeneza mazeze na mapango ya waimbaji. Miti ya uvumba kama hiyo ilikuwa haijaingia huko bado, wala haikuonekana tena hata siku hii ya leo.

13Kisha mfalme Salomo akampa mfalme wa kike wa Saba yote, aliyopendezwa nayo, aliyomwomba; kuyapita hayo mfalme Salomo akampa mwenyewe matunzo, kama ilivyompasa mfalme. Kisha akarudi kwenda kwao katika nchi yake, yeye na watumishi wake.

Mali za Salomo.

14Uzito wa dhahabu, Salomo alizoletewa katika mwaka mmoja ulikuwa vipande vya dhahabu 666, ndio frasila 2000,

15pasipo zile, alizozitoza watembezi na wachuuzi na wafalme wote wa nchi ya Waarabu na watawala nchi yake.

16Mfalme Salomo akatengeneza ngao 200 za dhahabu zilizofuliwa, kila ngao moja ikatumiwa sekeli 600, ndio nusu kubwa ya frasila ya dhahabu.[#1 Fal. 14:26.]

17Kisha akatengeneza ngao ndogo 300 za dhahabu zilizofuliwa, hizi ngao ndogo kila moja ikatumiwa mane tatu, ndio ratli sita za dhahabu, mfalme akaziweka katika nyumba ya mwituni kwa Libanoni.

18Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme cha pembe za tembo, akakifunikiza dhahabu zilizong'azwa.

19Hicho kiti cha kifalme kilikuwa na vipago sita vya kukipandia, tena huko nyuma hicho kiti cha kifalme kilikuwa kimeviringana juu. Tena hapo pa kukalia palikuwa na maegemeo huku na huko, nayo mifano miwili ya simba ilikuwa imesimama hapo penye maegemeo.

20Tena mifano kumi na miwili ya simba ilikuwa imesimama juu ya vile vipago sita, huku na huko. Kitu kilichotengenezwa vizuri hivyo hakikuwako katika ufalme wote.

21Navyo vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Salomo vilikuwa vya dhahabu, navyo vyombo vyote vya ile nyumba ya mwituni kwa Libanoni vilikuwa vya dhahabu zilizong'azwa, kwani fedha ziliwaziwa kuwa si kitu katika siku za Salomo.

22Kwani mfalme alikuwa na merikebu za Tarsisi zilizosafiri baharini pamoja na merikebu za Hiramu, kila miaka mitatu hizo merikebu za Tarsisi zikaja mara moja, zikaleta dhahabu na fedha na pembe za tembo na tumbili na madege wenye manyoya mazuri mno wanaoitwa tausi.

23Hivyo ndivyo, mfalme Salomo alivyokuwa mkuu kuwapita wafalme wote wa huku nchini kwa utukufu na kwa werevu wa kweli.

24Watu wa nchi zote wakataka kuuona uso wake Salomo, wayasikie maneno ya werevu wake wa kweli, Mungu alioutia moyoni mwake.

25Nao wakaleta kila mtu matunzo yake: vyombo vya fedha na vya dhahabu na mavazi na mata na uvumba na farasi na nyumbu; vikawa hivyo mwaka kwa mwaka.

(26-29: 2 Mambo 1:14-17.)

26Salomo akakusanya magari na wapanda farasi, hata akawa na magari 1400 na wapanda farasi 12000, akawakalisha katika miji ya magari namo mwake mfalme mle Yerusalemu.[#1 Fal. 4:26.]

27Mfalme akajipatia fedha kuwa nyingi mle Yerusalemu kama mawe, nayo miti ya miangati akajipatia kuwa mingi kama mitamba katika nchi ya tambarare.

28Nao farasi, Salomo aliokuwa nao, walitoka Misri, wachuuzi wengi wa mfalme waliwaleta wengi wakiwanunua na kuzilipa bei zao.

29Magari yaliyokuja kutoka Misri moja lilikuwa fedha 600 na farasi mmoja fedha 150. Vivyo hivyo waliwapelekea nao wafalme wote wa Wahiti na wafalme wa Ushami kwa mikono yao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania