The chat will start when you send the first message.
1Mfalme Salomo akapenda wanawake wageni pamoja na binti Farao, wa Kimoabu na wa Kiamoni na wa Kiedomu na wa Kisidoni na wa Kihiti.[#5 Mose 17:17.]
2Wote ni wa wamizimu wale, ambao Bwana aliwaagiza wana wa Isiraeli kwamba: Msiingie kwao, wala wao wasiingie kwenu! Kwani wataigeuza mioyo yenu, mwifuate miungu yao. Wao ndio, Salomo aliogandamana nao kwa kuwapenda.[#2 Mose 34:16.]
3Naye alikuwa na wanawake wa kifalme 700 na masuria 300; hao wakeze ndio waliougeuza moyo wake.
4Ikawa, Salomo alipokuwa mzee, ndipo, wakeze walipougeuza moyo wake, afuate miungu mingine; kwa hiyo moyo wake haukuwa wote mzima upande wa Bwana Mungu wake, kama moyo wa baba yake Dawidi ulivyokuwa.
5Salomo akamfuata Astoreti, mungu wa kike wa Sidoni, na Milkomu, tapisho lao Waamoni.
6Ndivyo, Salomo alivyoyafanya yaliyokuwa mabaya machoni pake Bwana, asipojihimiza kumfuata Bwana kama baba yake Dawidi.
7Siku zile Salomo akamjengea Kemosi, tapisho lao Wamoabu, kijumba cha kumtambikia juu ya mlima ulioko mbele ya Yerusalemu, hata Moleki, tapisho lao wana wa Amoni.[#4 Mose 21:29; 2 Fal. 23:13.]
8Ndivyo, alivyowafanyia wakeze wageni wote, wapate kuivukizia na kuitambikia miungu yao.
9Ndipo, Bwana alipomchafukia Salomo, kwa kuwa ameugeuza moyo wake, usimwelekee Bwana Mungu wa Isiraeli aliyemtokea mara mbili.[#1 Fal. 3:5; 9:2.]
10Naye alikuwa amemwagiza neno hilo, asifuate miungu mingine; lakini hakuyashika, Bwana aliyomwagiza.
11Kwa hiyo Bwana akamwambia Salomo: Kwa kuwa mambo yako yameendelea hivyo, usilishike agano langu, wala usiyafuate maongozi yangu, niliyokuagiza, nitakunyang'anya kweli ufalme, nimpe mtumishi wako.[#1 Sam. 15:28.]
12Lakini sitavifanya katika siku zako za kuwapo kwa ajili ya baba yako Dawidi, ila nitaunyang'anya mkononi mwa mwanao.[#1 Fal. 12:19.]
13Lakini sio ufalme wote, nitakaomnyang'anya, ila nitampa mwanao shina moja kwa ajili ya mtumishi wangu Dawidi, na kwa ajili ya Yerusalemu, niliouchagua.
14Bwana akainua mtu, awe mpingani wake Salomo, ni Mwedomu Hadadi aliyekuwa wa kizazi cha mfalme wa Edomu.
15Ilikuwa siku zile, Dawidi alipowashinda Waedomu; hapo Yoabu, mkuu wa vikosi, alipanda kuwazika waliouawa. Ndipo, alipomwua kila mtu wa kiume aliyepatikana kule Edomu.[#2 Sam. 8:14.]
16Kwani Yoabu na Waisiraeli wote walikaa huko miezi sita, mpaka wakiisha kuwaangamiza watu wa kiume wote kule Edomu.
17Lakini Hadadi alikimbia pamoja na waume wengine wa Edomu waliokuwa watumwa wa baba yake, wakaenda naye Misri, naye Hadai alikuwa akingali kijana mdogo.
18Wakaondoka Midiani, wakaja Parani, wakachukua watu wengine kule Parani kwenda nao Misri, kisha wakafika Misri kwa Farao, mfalme wa Misri. Huyu akampa nyumba, akamwagizia chakula, akampa nayo mashamba.
19Hadadi akapata upendeleo kabisa machoni pa Farao, akamwoza ndugu ya mkewe, ndiye ndugu ya Tahapenesi aliyekuwa mkewe mfalme.
20Huyu ndugu ya Tahapenesi akamzalia mwana wa kiume, Genubati; naye Tahapenesi akamkuza nyumbani mwa Farao. Kwa hiyo Genubati alikuwa nyumbani mwa Farao katikati ya wanawe Farao.
21Hadadi aliposikia kule Misri, ya kuwa Dawidi amelala na baba zake, tena ya kuwa Yoabu, mkuu wa vikosi, amekufa, ndipo, Hadadi alipomwambia Farao: Nipe ruhusa, niende kwetu katika nchi yangu!
22Farao akamwambia: Unakosa nini huku kwangu ukitafuta njia ya kwenda katika nchi yako? Akamwambia: Hakuna, lakini nipe ruhusa, nijiendee!
23Kisha Mungu akamwinua Rezoni, mwana wa Eliada, awe mpingani wake; ni yule aliyetoroka kwa bwana wake Hadadezeri, mfalme wa Soba.
24Akakusanya watu kwake, akawa mkuu wa kile kikosi, Dawidi alichowaua. Halafu wakaja Damasko, wakakaa huko na kupata ufalme wa Damasko.[#2 Sam. 8:3; 10:18.]
25Akawa mpingani wa Waisiraeli siku zote za maisha yake Salomo. Akayaongeza yale mabaya, Hadadi aliyoyafanya, akachukizwa na Waisiraeli, akawa mfalme wa Ushami.
26Alikuwako naye Yeroboamu, mwana wa Nebati wa Efuraimu wa mji wa Sereda; jina la mama yake ni Serua aliyekuwa mjane. Yeroboamu alikuwa mtumishi wa Salomo, lakini aliinua mkono kwa kumkataa mfalme.
27Naye akiinua mkono, amkatae mfalme, ilikuwa kwa ajili ya jambo hili: Salomo alipojenga Milo, apafunge mahali pale palipokuwa wazi penye mji wa baba yake Dawidi,[#1 Fal. 9:15,24.]
28yeye Yeroboamu alikuwa fundi wa vita mwenye nguvu. Salomo alipomwona huyu kijana, alivyofanya kazi, akamweka kuwa msimamizi wa kazi zote za nguvu za mlango wa Yosefu.
29Ikawa siku moja, Yeroboamu alipotoka Yerusalemu, mfumbuaji Ahia wa Silo akamwona njiani, naye alikuwa amevaa kanzu mpya; nao hao wawili walikuwa peke yao huko mashambani.
30Ahia akajivua kanzu yake mpya, aliyokuwa ameivaa, akairarua, itoke vipande 12.
31Akamwambia Yeroboamu: Jitwalie vipande kumi! Kwani ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyokuambia: Utaniona, nikimnyang'anya Salomo ufalme mkononi mwake, nikupe wewe mashina kumi.[#1 Fal. 12:15; 14:2.]
32Shina moja litakuwa lake kwa ajili ya mtumishi wangu Dawidi na kwa ajili ya Yerusalemu, niliouchagua katika mashina yote ya Isiraeli.
33Kwani wameniacha, wakamtambikia Astoreti, mungu wa Sidoni, na Kemosi, mungu wa Moabu, na Milkomu, mungu wa wana wa Amoni, hawakuendelea kuzishika njia zangu na kuyafanya yanyokayo machoni pangu na kuyafuata maongozi yangu na maamuzi yangu kama baba yake Dawidi.
34Lakini sitauondoa ufalme wote mkononi mwake yeye, ila nitamweka kuwa mkuu siku zote za maisha yake kwa ajili ya mtumishi wangu Dawidi, niliyemchagua, aliyeyaangalia maagizo yangu na maongozi yangu.[#2 Sam. 7:12.]
35Nitauondoa ufalme mkononi mwa mwanawe, nikupe mashina kumi.[#1 Fal. 12:16.]
36Mwanawe nitampa shina moja, kusudi mtumishi wangu Dawidi awe siku zote na taa iwakayo mbele yangu huko Yerusalemu, mle mjini, nilimochagua kuwa mwa kulikalishia humo Jina langu.
37Lakini wewe nitakuchukua, nikupe kuyatawala yote, roho yako iyatamaniyo, utakuwa mfalme wao Waisiraeli.
38Kama utayasikia yote, nitakayokuagiza, uzifuate njia zangu na kuyafanya yanyokayo machoni pangu na kuyaangalia maongozi yangu na maagizo yangu, kama mtumishi wangu Dawidi alivyofanya, ndipo, nitakapokuwa na wewe, nikujengee nyumba itakayokuwa yenye nguvu, kama nilivyomjengea Dawidi, nao Waisiraeli nitakupa.[#1 Fal. 9:4.]
39Lakini wao wa kizazi cha Dawidi nitawatesa kwa ajili ya mambo hayo, lakini si siku zote.
40Salomo akataka kumwua Yeroboamu, kwa hiyo Yeroboamu akaondoka, akakimbia kwenda Misri kwa Sisaki, mfalme wa Misri, akawa huko Misri, hata Salomo alipokufa.[#1 Fal. 14:25.]
41Mambo mengine ya Salomo nayo yote, aliyoyafanya, na maneno ya werevu wake uliokuwa wa kweli, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya Salomo?
42Nazo siku, Salomo alizokuwa mfalme mle Yerusalemu na kuwatawala Waisiraeli wote, ni miaka 40.
43Kisha Salomo akaja kulala na baba zake, akazikwa mjini mwa baba yake Dawidi, naye mwanawe Rehabeamu akawa mfalme mahali pake.