1 Wafalme 12

1 Wafalme 12

Ukorofi wa Rehabeamu.

(1-19: 2 Mambo 10.)

1Rehabeamu akaenda Sikemu, kwani Waisiraeli wote walifika Sikemu kumpa ufalme.[#1 Fal. 11:40.]

2Naye Yeroboamu, mwana wa Nebati, akayasikia, lakini alikuwa angaliko huko Misri, alikokimbilia alipomkimbia mfalme Salomo; huko Misri ndiko, Yeroboamu alikokaa.

3Walipotuma kumwita, Yeroboamu akaja na mkutano wote wa Waisiraeli, wakamwambia Rehabeamu kwamba:

4Baba yako alitutwisha mzigo mzito, nawe wewe sasa utupunguzie ule utumwa mgumu wa baba yako nao mzigo wake mzito, aliotutwisha! Kisha tutakutumikia.

5Akawaambia: Nendeni kwanza siku tatu, kisha rudini kwangu! Watu walipokwenda zao,

6mfalme Rehabeamu akafanya shauri na wazee waliomtumikia baba yake Salomo, alipokuwa mzima bado, akawauliza: Ninyi shauri lenu ni nini? Watu hawa tuwape majibu gani?[#Fano. 12:5.]

7Wakamwambia hivi: Ukiwaitikia leo watu hawa na kuwatumikia, tena ukiwajibu na kuwaambia maneno mema, ndipo, watakapokuwa watumishi wako siku zote.

8Lakini akaliacha shauri la wazee, walilompa, akafanya shauri na vijana waliokua naye na kumtumikia,

9akawauliza: Ninyi shauri lenu ni nini? tuwape majibu gani watu hawa walioniambia: Tupunguzie mzigo, aliotutwisha baba yako?

10Vijana hawa waliokua naye wakasemezana naye kwamba: Haya ndiyo, uwaambie watu hao waliokuambia kwamba: Baba yako aliukuza mzigo wetu kuwa mzito, wewe utupuzie huo mzigo wetu, basi uwaambie hivyo: Kidole changu kidogo na kinenepe kuliko viuno vya baba yangu,

11sasa vitakuwa hivi: kama baba yangu aliwatwisha mzigo mzito, mimi nitauzidisha mzigo wenu; kama baba yangu aliwapiga fimbo, mimi nitawapiga viboko vyenye miiba.

Ufalme wa Dawidi unagawanyika.

12Yeroboamu na watu wote wakaja kwake Rehabeamu siku ya tatu, kama mfalme alivyosema kwamba: Rudini kwangu siku ya tatu![#1 Fal. 12:5.]

13Ndipo, mfalme alipowapa hawa watu majibu magumu akiliacha shauri la wazee, walilompa,

14akasema nao na kulifuata shauri la vijana kwamba: Kama baba yangu aliwatwisha mzigo mzito, mimi nitauzidisha; kama baba yangu aliwapiga fimbo, mimi nitawapiga viboko vyenye miiba.

15Mfalme hakuwasikia wale watu, kwani Bwana aliyageuza kuwa hivyo, apate kulitimiza neno lake, alilomwambia Yeroboamu, mwana wa Nebati, kinywani mwa Ahia wa Silo.[#1 Fal. 11:31.]

16Waisiraeli wote walipoona, ya kuwa mfalme hakuwasikia, ndipo, watu walipomjibu mfalme neno la kwamba: Sisi tuna bia gani na Dawidi? Hatuna fungu lo lote kwake mwana wa Isai. Waisiraeli, haya! Rudini sasa mahemani kwenu! Nawe Dawidi, na uuangalie mwenyewe mlango wako! Ndipo, Waisiraeli walipokwenda mahemani kwao.[#Fano. 15:1; 2 Sam. 20:1.]

17Ni wana wa Isiraeli waliokaa katika miji ya Yuda tu, Rehabeamu aliowapata, awe mfalme wao.

18Mfalme Rehabeamu alipomtuma Adoramu aliyekuwa msimamizi wa kazi za nguvu, wana wa Isiraeli wote wakampiga mawe, hata akafa. Kisha mfalme Rehabeamu akajihimiza kupanda garini na kukimbilia Yerusalemu.

19Ndivyo, Waisiraeli walivyojitenga na mlango wa Dawidi mpaka siku ya leo.

20Ikawa, Waisiraeli wote waliposikia, ya kuwa Yeroboamu amerudi, wakatuma kumwita kuja kwenya mkutano, wakamfanya kuwa mfalme wa Waisiraeli wote, hakuna aliyeufuata mlango wa Dawidi, ni shina la Yuda peke yake tu.

Rehabeamu anakatazwa kupigana na Waisiraeli.

(21-24: 2 Mambo 11:1-4.)

21Rehabeamu alipofika Yerusalemu akaukusanya mlango wote wa Yuda na shina la Benyamini, watu 180000 waliochaguliwa kupiga vita, wapigane na mlango wa Waisiraeli, wamrudishie Rehabeamu, mwana wa Salomo, ufalme huo.

22Lakini neno la Mungu likamjia Semaya aliyekuwa mtu wa Mungu, kwamba:

23Mwambie Rehabeamu, mwana wa Salomo, mfalme wa Wayuda, nao wote wa milango ya Yuda na ya Benyamini nao wale watu waliosalia huku kwamba:

24Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msipande kwenda kupigana na ndugu zenu, wana wa Isiraeli! Rudini kila mtu nyumbani kwake! Kwani jambo hili limefanywa na mimi. Walipolisikia neno hili la Bwana, wakarudi kwenda zao, kama Bwana alivyosema.

Ufalme wa Waisiraeli: Yeroboamu anawakosesha Waisiraeli.

25Yeroboamu akaujenga Sikemu milimani kwa Efuraimu, akakaa humo; kisha akatoka humo, akajenga Penueli.[#1 Mose 32:30.]

26Yeroboamu akasema moyoni mwake: Sasa ufalme utarudi kuwa wa mlango wa Dawidi,

27watu wa huku wakipanda kwenda kutambikia Nyumbani mwa Bwana mle Yerusalemu; ndipo, mioyo ya watu wa huku itakapowageukia mabwana zao naye Rehabeamu, mfalme wa Wayuda, kisha wataniua, wapate kurudi kwa Rehabeamu, mfalme wa Wayuda.

28Mfalme alipokwisha kulifanya shauri hilo akatengeneza ndama mbili za dhahabu, akawaambia watu: Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; Waisiraeli, itazameni miungu yenu iliyowatoa katika nchi ya Misri![#2 Mose 32:4,8.]

29Ndama moja akaiweka Beteli, moja akaiweka Dani.[#Amu. 18:30.]

30Jambo hili likawakosesha watu, kwani watu wakaenda hata Dani kuitambikia hiyo moja.[#1 Fal. 14:16.]

31Hata vilimani juu akatengeneza vijumba vya kutambikia, akaweka nao watu wo wote kuwa watambikaji wasiokuwa na wana wa Lawi.

32Yeroboamu akafanya sikukuu katika mwezi wa 8 siku ya 15 ya huo mwezi kama sikukuu ya Wayuda, naye akatoa ng'ombe za tambiko hapo pa kutambikia. Ndivyo, alivyofanya hata Beteli, azitambikie zile ndama, alizotengeneza; kisha akaweka Beteli watambikaji wa kutambika katika vijumba, alivyovijenga vilimani.

33Napo hapo, alipopatengeneza pa kutambikia huko Beteli, akatoa ng'ombe za tambiko, ikawa ile siku ya 15 ya mwezi wa 8, aliyoizusha moyoni mwake; hapo, alipowafanyia wana wa Isiraeli sikukuu, akapanda kufika hapo pa kutambikia, avukize.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania