1 Wafalme 15

1 Wafalme 15

Mfalme Abiamu wa Wayuda.

(1-8: 2 Mambo 13.)

1Katika mwaka wa 18 wa mfalme Yeroboamu, mwana wa Nebati, Abiamu akapata kuwa mfalme wa Wayuda.

2Akawa mfalme miaka 3 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Maka, binti Abisalomu.

3Akaendelea kuyafanya makosa yote ya baba yake, aliyoyafanya machoni pake, nao moyo wake haukuwa wote mzima upande wa Bwana Mungu wake kama moyo wa baba yake Dawidi.

4Lakini kwa ajili ya Dawidi Bwana Mungu wake akampa kuwa taa iwakayo mle Yerusalemu, akimwinulia mwanawe wa kumfuata, tena akiuacha Yerusalemu, usimame vivyo hivyo.[#1 Fal. 11:36.]

5Kwani Dawidi aliyafanya yanyokayo machoni pake Bwana, tena yote aliyomwagiza hakuyaacha siku zote za maisha yake, lisipokuwa lile jambo la Mhiti Uria.[#2 Sam. 11:27; 12:9.]

6Vita vya kupigana kwao Rehabeamu na Yeroboamu vikawako siku zote za maisha yake.[#1 Fal. 14:30.]

7Mambo mengine ya Abiamu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Yuda? Navyo vita vya kupigana kwao Abiamu na Yeroboamu vikawako.

8Abiamu akaja kulala na baba zake, wakamzika mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Asa akawa mfalme mahali pake.

Mfalme Asa wa Wayuda.

9Katika mwaka wa 20 wa Yeroboamu, mfalme wa Waisiraeli, Asa akapata kuwa mfalme wa Wayuda.

10Akawa mfalme miaka 41 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Maka, binti Abisalomu.[#1 Fal. 15:2.]

(11-15: 2 Mambo 14:1-4; 15:16-18.)

11Asa akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama baba yake Dawidi.

12Akawatowesha wagoni wa patakatifu katika nchi yake, hata magogo yote ya kutambikia, baba zake waliyoyatengeneza, akayaondoa.[#1 Fal. 14:24; 22:47.]

13Naye mama yake Maka akamwondoa katika ukuu wake, kwa kuwa alitengeneza kinyago cha Ashera, nacho hicho kinyago chake Asa akakikatakata,, akakiteketeza penye kijito cha Kidoroni.

14Lakini matambiko ya vilimani hayakutoweka, lakini moyo wake Asa ulikuwa wote mzima upande wa Bwana siku zake zote.[#1 Fal. 22:44.]

15Navyo, baba yake alivyovitakasa, pamoja navyo, alivyovitakasa mwenyewe, fedha na dhahabu na vyombo, akavipeleka Nyumbani mwa Bwana.

Vita vya Asa na Basa, mfalme wa Waisiraeli.

(16-24: 2 Mambo 16:1-6; 11-14.)

16Vita vya kupigana kwao Asa na Basa, mfalme wa Waisiraeli, vikawako siku zao zote.

17Basa, mfalme wa Waisiraeli, akapanda kuijia nchi ya Yuda, akajenga Rama, asipatikane mtu anayeweza kutoka wala kuingia kwa Asa, mfalme wa Wayuda.

18Ndipo, Asa alipozichukua fedha zote na dhahabu zilizosalia katika vilimbiko vya Nyumba ya Bwana navyo vilimbiko vya nyumba ya mfalme, akavitia mikononi mwa watumishi wake; kisha mfalme Asa akawatuma kwa Benihadadi, mwana wa Taburimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Ushami, aliyekaa Damasko, kumwambia:[#2 Fal. 12:18; 16:8.]

19Liko agano, tuliloliagana mimi na wewe, naye baba yangu na baba yako; kwa hiyo ninatuma kwako matunzo ya fedha na ya dhahabu. Nenda, ulivunje agano, uliloliagana na Basa, mfalme wa Waisiraeli, aondoke kwangu!

20Benihadadi akamwitikia mfalme Asa, akawatuma wakuu wa vikosi vyake, alivyokuwa navyo, kwenda kupigana na miji ya Waisiraeli, akaipiga miji ya Iyoni na Dani na Abeli-Beti-Maka na Kineroti yote, hata nchi yote ya Nafutali.[#2 Fal. 15:29.]

21Basa alipoyasikia haya akaacha kuujenga Rama, akaja kukaa Tirsa.

22Ndipo, mfalme Asa alipowapigia Wayuda wote mbiu kwamba: Hakuna asiyepaswa na kazi yangu. Kwa hiyo wakayachukua mawe ya huko Rama nayo miti yake, Basa aliyoitumia ya kujenga, naye mfalme Asa akaitumia ya kujenga Geba wa Benyamini na Misipa.

Kufa kwake Asa.

23Mambo mengine yote ya Asa na matendo yake ya vitani yenye nguvu, hayo yote, aliyoyafanya, nayo miji aliyoijenga, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Lakini alipokuwa mzee akaugua miguu yake.[#2 Mambo 14:5-6.]

24Kisha Asa akaja kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Yosafati akawa mfalme mahali pake.[#1 Fal. 22:41.]

Ufalme wa Waisiraeli: Nadabu na Basa.

25Nadabu, mwana wa Yeroboamu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli katika mwaka wa pili wa Asa, mfalme wa Wayuda; akawa mfalme wa Waisiraeli miaka 2.[#1 Fal. 14:20.]

26Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, akaendelea kuishika njia ya baba yake na kuyafanya makosa yake, yaliyowakosesha Waisiraeli.[#1 Fal. 12:30.]

27Naye Basa, mwana wa Ahia, wa mlango wa Isakari, akamlia njama, kisha Basa akampiga kule Gibetoni ulioko kwa Wafilisti, yeye Nadabu na Waisiraeli wote walipokuwa wanausonga Gibetoni kwa kuuzinga.[#1 Fal. 16:9.]

28Basa akamwua katika mwaka wa tatu wa Asa, mfalme wa Wayuda, akawa mfalme mahali pake.

29Naye alipokwisha kuwa mfalme akawaua wote waliokuwa wa mlango wa Yeroboamu, hakusaza hata mmoja aliyevuta pumzi kwao wa Yeroboamu, akawamaliza kabisa, kama Bwana alivyosema kinywani mwa mtumishi wake Ahia wa Silo,[#1 Fal. 14:10-11.]

30kwa ajili ya makosa, Yeroboamu aliyoyakosa na kuwakosesha Waisiraeli; ndivyo, alivyomchafua sana Bwana Mungu wa Waisiraeli.

31Mambo mengine ya Nadabu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?

32Vita vya kupigana kwao Asa na Basa, mfalme wa Waisiraeli, vikawako siku zao zote.[#1 Fal. 15:16.]

33Katika mwaka wa tatu wa Asa, mfalme wa Wayuda, Basa, mwana wa Ahia, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli wote huko Tirsa, akawatawala miaka 24.[#1 Fal. 15:28.]

34Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, akaendelea kuishika njia ya Yeroboamu na kuyafanya makosa yake yaliyowakosesha Waisiraeli.[#1 Fal. 15:26.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania