1 Wafalme 18

1 Wafalme 18

Elia anamtokea Ahabu.

1Siku zilipopita nyingi, neno la Bwana likamjia Elia katika mwaka wa tatu kwamba: Nenda kumtokea Ahabu! Kwani nitanyesha mvua katika nchi.

2Ndipo, Elia alipokwenda kumtokea Ahabu, lakini njaa ilikuwa ngumu huko Samaria.

3Ahabu akamwita Obadia, mtumishi wake wa nyumbani, naye Obadia alikuwa mtu aliyemwogopa Bwana kabisa.[#1 Fal. 18:12.]

4Hapo, Izebeli alipowaangamiza wafumbuaji wa Bwana, Obadia alichukua wafumbuaji mia, akawaficha hamsini hamsini pangoni, akawatunza na kuwapa mikate na maji.

5Ahabu akamwambia Obadia: Tembea katika nchi kwenye chemchemi zote za maji na kwenye vijito kutazama-tazama, kama majani yanapatikana ya kuwaponya farasi na punda njaa, tusifiwe na hawa nyama wote.

6Wakajigawanyia nchi ya kupitia, Ahabu akashika njia moja peke yake, naye Obadia akashika njia nyingine peke yake.

7Obadia alipofika njiani, mara akakutana na Elia; alipomtambua akamwangukia usoni pake, akamwambia: Kumbe wewe ndiwe bwana wangu Elia!

8Akamjibu: Ndimi! Nawe nenda, kamwambie bwana wako: Elia ameoneka!

9Akajibu: Nimekosa nini, wewe ukimtia mtumishi wako mkononi mwa Ahabu, aniue?

10Hivyo, Bwana Mungu wako alivyo Mwenye uzima, hakuna taifa wala ufalme, bwana wangu asikotuma watu, wakutafute, nao walipomwambia: Hayuko! akawaapisha wenye ufalme, hata mataifa, ya kuwa hawakukuona.[#1 Fal. 17:12.]

11Na sasa wewe unasema: Nenda, kamwambie bwana wako: Elia ameoneka!

12Nami nitakapokwenda kutoka kwako, kisha Roho ya Bwana itakupeleka mahali, nisipopajua, nami nikienda kumpasha Ahabu hiyo habari, basi, asipokuona hataniua? Nami mtumishi wako ninamwogopa Bwana tangu ujana wangu.[#1 Fal. 18:3.]

13Wewe bwana wangu, hukuambiwa niliyoyafanya, Izebeli alipowaua wafumbuaji wa Bwana, ya kuwa mia yao hao wafumbuaji wa Bwana nimewaficha hamsini hamsini pangoni, nikawapa mikate na maji?

14Na sasa wewe unasema: Nenda, kamwambie bwana wako: Elia ameoneka! Ndipo, akaponiua.

15Elia akamwambia: Hivyo, Bwana Mwenye vikosi, ninayemtumikia, alivyo Mwenye uzima, leo hivi nitamtokea.[#1 Fal. 17:1; 2 Fal. 3:14.]

16Basi, Obadia akaenda kukutana na Ahabu, akampasha habari hiyo. Ndipo, Ahabu alipokwenda kukutana na Elia.

17Ikawa, Ahabu alipomwona Elia, Ahabu akamwambia: Je? Wewe siwe uwaponzaye Waisiraeli?[#Amo. 7:10; Tume. 16:20.]

18Akajibu: Mimi sikuwaponza Waisiraeli, ila ndiwe wewe pamoja na mlango wa baba yako, mkiyaacha maagizo ya Bwana kwa kuyafuata Mabaali.[#1 Fal. 16:31-32.]

19Sasa tuma, uwakusanye Waisiraeli wote kwangu mlimani kwa Karmeli pamoja na wale wafumbuaji wa Baali 450 nao wale wafumbuaji wa Ashera 400 wanokula mezani kwa Izebeli![#1 Fal. 16:33.]

20Ndipo, Ahabu alipotuma kuwaita wana wa Isiraeli wote, nao wafumbuaji akawakusanya mlimani kwa Karmeli.

Mungu anajijulisha mlimani kwa Karmeli.

21Elia akafika huko, watu wote waliko, akawaambia: Mpaka lini mtakwenda na kuchechemea pande mbili? Kama Bwana ni Mungu, mfuateni! Kama Baali ni Mungu, mfuateni! Lakini watu hawakumjibu neno.[#Yos. 24:15; Mat. 6:24.]

22Ndipo, Elia alipowaambia wale watu: Mimi nimesalia peke yangu kuwa mfumbuaji wa Bwana, lakini wafumbuaji wa Baali ni watu 450.

23Na tupewe ng'ombe wawili, nao wajichagulie dume mmoja, wamkatekate, wamweke juu ya chungu ya kuni, lakini wasitie moto! Nami nitamfanyizia yule dume mwingine vivyo hivyo, kisha nimweke juu ya chungu ya kuni, lakini moto sitatia.

24Ninyi litambikieni jina la mungu wenu, nami nilitambikie Jina la Bwana. Naye atakayeitikia na kuwakisha moto, yeye ndiye Mungu! Watu wote wakaitikia wakisema: Neno hili ni jema.

25Kisha Elia akawaambia watambikaji wa Baali: Jichagulieni dume mmoja, mwanze kumtengeneza! Kwani ninyi m wengi. Kisha litambikieni jina la mungu wenu, lakini moto msitie!

26Wakamchukua yule dume waliyepewa, wakamtengeneza, wakalitambikia jina la Baali kuanzia asubuhi, hata jua likawa kichwani, wakiomba: Baali, tuitikie! Lakini hakuna sauti, wala aitikiaye. Wakarukaruka na kupazunguka hapo pa kutambikia, walipopatengeneza.

27Jua lilipokuwa kichwani, Elia akawafyoza na kuwaambia: Mwiteni na kupaza sauti! Kwani ni mungu! Labda anafikiri neno, au ametoka, au yuko njiani, labda amelala, sharti aamke!

28Wakapaza sauti sana za kumwita, wakajichanjachanja kwa mapanga na kwa visu kama desturi yao, hata damu zikawatoka.

29Saa sita zilipopita, wakawa kama wenye wazimu hata hapo, vilaji vya tambiko vinapotolewa, lakini hakuna sauti, wala hakuna aitikiaye, wala hakuna asikiaye.[#1 Sam. 18:10; 4 Mose 28:4-5.]

30Ndipo, Elia alipowaambia watu wote: Njoni kwangu! Watu wote walipofika kwake, akapajenga tena hapo pa kumtambikia Bwana palipokuwa pamebomolewa.

31Elia akachukua mawe 12 kwa hesabu ya mashina ya wana wa Yakobo, ambaye neno la Bwana lilimjia la kwamba: Jina lako litakuwa Isiraeli.[#1 Mose 32:28; 2 Mose 24:4.]

32Hayo mawe akayajenga na kulitaja Jina la Bwana, pawe pa kutambikia, kisha akachimba mfereji wenye upana wa shamba litoshalo kumyagia humo pishi mbili za mbegu, ukapazunguka hapo pa kutambikia.

33Kisha akatandika kuni, akamkatakata dume lake la ng'ombe, akamweka juu ya zile kuni.

34Akasema: Jazeni mitungi minne maji, myamwage juu ya ng'ombe ya tambiko na juu ya kuni! Kisha akasema: Ongezeni mara ya pili! Wakaongeza mara ya pili! akasema tena: Mara ya tatu! Wakaongeza mara ya tatu.

35Maji yakaenea po pote hapo penye kutambikia, hata mfereji ukajaa maji.

36Walipotolea vilaji vya tambiko, mfumbuaji Elia akatokea, akasema: Bwana, Mungu wa Aburahamu na wa Isaka na wa Isiraeli, leo hivi na yajulikane, ya kuwa wewe ndiwe Mungu kwao Waisiraeli, mimi nami ndimi mtumishi wako. Tena kwa neno lako nimeyafanya haya yote.

37Niitikie, Bwana! Niitikie! Ndivyo, watu hawa watakavyojua, ya kuwa wewe Bwana ndiwe Mungu, ya kuwa wewe ndiwe anayeigeuza mioyo yao, wakufuate.

38Ndipo, moto wa Bwana ulipoanguka, ukaila ng'ombe ya tambiko, hata kuni na mawe na mavumbi, hata maji yaliyokuwa katika mfereji ukayakausha.[#3 Mose 9:24.]

39Watu wote walipoyaona wakaanguka nyusoni pao wakisema: Bwana ndiye Mungu! Bwana ndiye Mungu!

40Ndipo, Elia alipowaambia: Wakamateni wafumbuaji wa Baali, kwao asipone hata mmoja! Walipowakamata, Elia akawatelemsha kwenye kijito cha Kisoni, akawaua huko.[#5 Mose 13:5; 2 Fal. 10:25.]

Mvua inanyesha kwa kuomba kwake Elia.

41Elia akamwambia Ahabu: Nenda, ule, unywe! Kwani nasikia uvumi wa mvua.

42Ahabu alipokwenda zake huko juu kula na kunywa, Elia akapanda Karmeli pembeni, akainama chini na kuuweka uso magotini.[#Yak. 5:18.]

43Akamwambia kijana, aliyekuwa naye: Panda, uchungulie upande wa baharini! Akapanda, akapachungulia, akasema: Hakuna ninachokiona, akamwambia: Rudi mara saba!

44Alipofika mara ya saba akasema: Nimeona kiwingu kidogo kama kiganja cha mtu, kinatoka baharini. Akamwambia: Nenda kumwambia Ahabu: Tandika farasi, ushuke upesi, mvua isikuzuie!

45Punde si punde, mara mbingu ikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua kubwa. Ahabu akapanda garini, akaja Izireeli.

46Lakini mkono wa Bwana ukamjia Elia, akajifunga viuno vyake, akapiga mbio kwenda mbele ya Ahabu mpaka kufika Izireeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania