The chat will start when you send the first message.
1Ahabu akamsimulia Izebeli yote, Elia aliyoyafanya, na jinsi alivyowaua wafumbuaji wote wa Baali.[#1 Fal. 18:40.]
2Ndipo, Izebeli alipotuma mjumbe kwake Elia kumwambia: Mungu na anifanyizie hivi, tena hivi, nisipoifanyizia roho yako kuwa kesho wakati huuhuu kama roho yake mmoja wao!
3Ndipo, aliposhikwa na woga, akaondoka, akaenda zake. Alipofika Beri-Seba ulioko katika nchi ya Yuda akamwacha huko kijana, aliyekuwa naye.
4Mwenyewe akaenda nyikani mwendo wa siku moja, akaja kukaa chini ya mfagio mmoja, akajiombea kufa akisema: Nimechoka sasa; Bwana, ichukue roho yangu! Kwani mimi si mwema kuliko baba zangu.[#Iy. 7:16; Yona 4:3; Fil. 1:23.]
5Kisha akalala usingizi penye huo mfagio mmoja. Mara malaika akamgusa, akamwambia: Inuka, ule!
6Alipotazama akaona kichwani kwake mkate uliochomwa na kibuyu cha maji; akala, akanywa, kisha akarudi, akalala.
7Ndipo, malaika wa Bwana aliporudi mara ya pili, akamgusa na kumwambia: Inuka, ule! Kwani njia, utakayokwenda, ni ndefu ya kuzishinda nguvu zako.
8Akainuka, akala, akanywa. Kisha akaenda kwa nguvu ya hicho chakula siku 40 mchana na usiku, mpaka akiufikia mlima wa Mungu, jina lake Horebu.[#2 Mose 24:18.]
9Akaingia huko pangoni, akalala mle. Ndipo, neno la Bwana lilipomjia la kumwuliza: Unafanya nini humu, Elia?
10Akajibu: Nimejihimiza sana kwa ajili ya Bwana Mungu Mwenye vikosi, kwa kuwa wana wa Isiraeli wameliacha Agano lako, wakapabomoa pote pa kukutambikia, nao wafumbuaji wako wakawaua kwa panga, nikasalia mimi peke yangu; tena roho yangu nayo wanaitafuta, waichukue.[#Yes. 49:4; Rom. 11:3; 1 Fal. 18:22.]
11Akaambiwa: Toka, usimame mlimani mbele ya Bwana, uone jinsi Bwana anavyopita! Pakaja upepo wenye nguvu nyingi ulioporomosha milima na kuvunja magenge, ukamtangulia Bwana, lakini Bwana hakuwamo mle upeponi. Upepo ulipokwisha pita, pakafuata mtetemeko wa nchi, lakini Bwana hakuwamo katika mtetemeko.[#2 Mose 33:22.]
12Mtetemeko ulipokwisha pita, pakafuata moto, lakini namo motoni Bwana hakuwamo. Moto ulipokwisha pita, pakaja sauti nyembamba yenye upole.[#2 Mose 34:6.]
13Elia alipoisikia, akaufunika uso wake kwa kanzu yake, akatoka kusimama langoni mwa pango; ndipo, aliposikia, sauti ikimwuliza: Unafanya nini humu, Elia?
14Akajibu: Nimejihimiza sana kwa ajili ya Bwana Mungu Mwenye vikosi, kwani wana wa Isiraeli wameliacha Agano lako, wakapabomoa pote pa kukutambikia, nao wafumbuaji wako wakawaua kwa panga, nikasalia mimi peke yangu; tena roho yangu nayo wanaitafuta, waichukue.[#1 Fal. 19:10; Sh. 69:10.]
15Ndipo, Bwana alipomwambia: Nenda kuirudia hiyo njia ya nyikani, ufike Damasko! Utakapofika, umpake Hazaeli mafuta, awe mfalme wa Ushami.[#2 Fal. 8:13,15.]
16Naye Yehu, mwana wa Nimusi, umpake mafuta, awe mfalme wa Waisiraeli! Naye Elisa, mwana wa Safati, wa Abeli-Mehola umpake mafuta, awe mfumbuaji mahali pako![#1 Fal. 19:19; 2 Fal. 9:2-3.]
17Itakuwa, atakayeukimbia upanga wa Hazaeli Yehu atamwua, naye atakayeukimbia upanga wa Yehu Elisa atamwua.
18Nami nitasaza katika Waisiraeli 7000, ndio wote wasiompigia Baali magoti, ndio wote wasiomnonea.[#Rom. 11:4.]
19Alipoondoka huko akamwona Elisa, mwana wa Safati, akilima na ng'ombe, jozi 12 zilikuwa mbele yake, naye alikuwa pale penye ile ya kumi na mbili; Elia akamwendea, akamtupia kanzu yake.
20Ndipo, alipowaacha ng'ombe wake, akamkimbilia Elia, akamwambia: Nipe ruhusa, kwanza ninoneane na baba na mama! Kisha nitakufuata. Akajibu: Nenda, uridi upesi! Usisahau niliyokutendea![#Luk. 9:61.]
21Aliporudi, amfuate, akachukua ng'ombe wawili, akawaua; kisha akazipika nyama zao na kuvitumia vyombo vya hao ng'ombe kuwa kuni; hizo nyama zao akawagawia watu wake, wazile. Kisha akaondoka, akamfuata Elia na kumtumikia.