The chat will start when you send the first message.
1Benihadadi, mfalme wa Ushami, akavikusanya vikosi vyake vyote, hata wafalme 32 walikuwa naye pamoja na farasi na magari, akaja kuusonga Samaria kwa kuuzinga, apigane nao.
2Akatuma wajumbe kwenda mjini kwa Ahabu, mfalme wa Waisiraeli.
3akamwambia: Ndivyo, Benihadadi anavyosema: Fedha zako na dhahabu zako ni zangu, na wake zako na watoto wako walio wazuri ni wangu.
4Mfalme wa Waisiraeli akajibu kwamba: Na yawe, kama ulivyosema, bwana wangu mfalme! Mimi ni mtu wako, navyo vyote, nilivyo navyo, ni vyako.
5Wajumbe wakarudi tena, wakasema: Hivi ndivyo, Benihadadi anavyosema kwamba: Kweli nimetuma kwako kukuambia: Fedha zako na dhahabu zako na wake zako na watoto wako utanipa.
6Lakini kesho saa hizi nitatuma watumishi wangu kwako, waichunguze nyumba yako, nazo nyumba za watumishi wako, wakamate kwa mikono yao yote yanayokupendeza, wayachukue.
7Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipowaita wazee wote wa nchi, akawaambia: Jueni, mwone, ya kuwa huyu anatafuta mabaya. Kwani alipotuma kwangu kuwataka wake zangu na watoto wangu na fedha zangu na dhahabu zangu, sikumnyima.[#2 Fal. 5:7.]
8Wazee wote na watu wote wakamwambia: Usimwitikie, wala usikubali!
9Basi, akawaambia wajumbe wa Benihadadi: Mwambieni bwana wangu mfalme: Yote, uliyomtumia mtumishi wako hapo kwanza, nitayafanya; lakini neno hili siwezi kulifanya. Wajumbe wakaenda zao kumpelekea hili jibu.
10Benihadadi akatuma kwake kumwambia: Mungu anifanyizie hivi, tena hivi, kama mavumbi ya Samaria yatatosha kuyajaza magao ya watu wote waliozifuata nyayo zangu!
11Mfalme wa Waisiraeli akajibu akisema: Mwambieni: Mwenye kujifunga mata asijivune akiwa hajayavua!
12Naye alipolisikia neno hili, alikuwa akinywa na wafalme wenziwe mabandani, akawaambia watumishi wake: Haya! Jipangeni! Wakajipanga, waujie huo mji.
13Mara mfumbuaji mmoja akafika kwa Ahabu, mfalme wa Waisiraeli, akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kumbe umeuona huo mtutumo mkubwa wote wa watu? Utaona leo, nikiwatia mkononi mwako, upate kujua, ya kuwa mimi ni Bwana.
14Ahabu akauliza: Kwa msaada wa nani? Akasema: Hivi ndivyo, Bwana anvyosema: Kwa msaada wa vijana wa wakuu wa majimbo. Akauliza tena: Ni nani atakayeanza kupigana? akajibu: Wewe.
15Kwa hiyo akawakagua vijana wa wakuu wa majimbo, wakawa 232; kisha akawakagua watu wote wa wana wa Isiraeli, wakawa 7000.
16Wakatoka mnamo saa sita, Benihadadi alipokuwa anakunywa na kulewa mabandani pamoja na wale wafalme wenziwe 32 waliomsaidia.
17Wale vijana wa wakuu wa majimbo walipoanza kutoka, wote, Benihadadi aliowatuma, wakampasha habari kwamba: Watu wanatoka Samaria.
18Akasema: Kama wanatokea mapatano, wakamateni, wa hai! Kama wanatokea mapigano, vilevile wakamateni, wa hai!
19Lakini hao vijana wa wakuu wa majimbo walipokwisha kutoka mjini pamoja na vikosi vilivyowafuata,
20wakaua kila mtu wake wa kukutana naye; ndipo, Washami walipokimbia, nao Waisiraeli wakawakimbiza, lakini Benihadadi, mfalme wa Washami, akapona kwa farasi pamoja na wengine waliopanda farasi.
21Kisha naye mfalme wa Waisiraeli akatoka, akapiga farasi na magari, akawapiga Washami, wakauawa wengi mno.
22Kisha yule mfumbuaji akamtokea mfalme wa Waisiraeli, akamwambia: Nenda, ujipatie nguvu! Kwa hayo, uliyoyaona, ujue ya kufanya! Kwani mwaka utakapopita, mfalme wa Ushami atapanda tena, akujie.[#1 Fal. 20:13.]
23Watumishi wa mfalme wa Ushami wakamwambia: Mungu wa milima ni Mungu wao, kwa sababu hii wametushinda. Lakini tungepigana nao katika nchi ya tambarare, tungewashinda.[#1 Fal. 20:25.]
24Fanya hivi tu: waondoe wafalme kila mmoja mahali pake, uweke watawala nchi mahali pao!
25Kisha jihesabie vikosi, kama vile vilivyokuwa ulivyofiwa navyo, tena farasi kwa farasi, na gari kwa gari, tupigane nao katika nchi ya tambarare, tuone, kama sisi hatutawashinda. Basi, akayaitikia, waliyomwambia, akafanya hivyo.
26Mwaka ulipopita, Benihadadi akawakagua Washami, akawapeleka Afeki kupigana na Waisiraeli.
27Nao wana wa Isiraeli walipokwisha kukaguliwa na kupewa posho wakatoka kuja kukutana nao, wakapiga makambi nyuma yao, wakawa kama vikundi viwili vya mbuzi, nao Washami walikuwa wameieneza hiyo nchi.
28Ndipo, yule mtu wa Mungu alipofika kwake mfalme wa Waisiraeli, akasema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa kuwa Washami wamesema: Bwana ni Mungu wa milima, lakini siye Mungu wa mabonde, basi, huu mtutumo mkubwa wote wa watu nitautia mkononi mwako, mpate kujua, ya kuwa mimi ni Bwana.[#1 Fal. 20:22.]
29Hivyo wakakaa makambini na kuelekeana siku saba; siku ya saba wakakaribiana kupigana. Ndipo, wana wa Isiraeli walipowaua hiyo siku moja Washami 100000 waendao kwa miguu.
30Waliosalia wakaukimbilia mji wa Afeki, boma la mji likawaangukia wale watu 27000 waliokuwa wamesalia, naye Benihadadi aliukimbilia huo mji na kuingia chumba kwa chumba.
31Kisha watumishi wake wakamwambia: Tazama, tumesikia, ya kuwa wafalme wa mlango wa Isiraeli ndio wafalme wenye upole; na tuvae magunia viunoni petu na kamba vichwani petu, kisha tumtokee mfalme wa Waisiraeli, hivyo labda atakuacha, ukae.
32Wakajifunga magunia viunoni pao na kamba vichwani pao, wakaja kwa mfalme wa Waisiraeli, wakasema: Mtumishi wako Benihadadi anaomba: Niache, nikae! Akauliza: Kumbe yuko mzima bado? Ni ndugu yangu!
33Neno hili wale watu wakaliwazia kuwa si ndege mbaya, wakajihimiza kutambua, kama ndilo lililomo moyoni mwake kweli, wakauliza: Benihadadi ni ndugu yako kweli? Akajibu: Nendeni kumchukua! Ndipo, Benihadadi alipomtokea, naye akampandisha garini.
34Benihadadi akamwambia: Miji, baba yangu aliyoichukua kwa baba yako, nairudisha; tena utajipatia njia za kuingia Damasko, kama baba yangu alivyojipatia njia ya kuingia Samaria. (Ahabu akasema): Kwa agano hili nitakuacha, ujiendee. Basi, akafanya agano naye, kisha akamwacha, ajiendee.
35Kisha mmoja wao wanafunzi wa wafumbuaji akamwambia mwenziwe kwa kuagizwa na Bwana: Unipige! Yule mwenziwe akakataa kumpiga.
36Naye akamwambia: Kwa kuwa hukuiitikia sauti ya Bwana, ukitoka kwangu, utaona simba, naye atakuua! Basi alipotoka kwake, simba akamwona, akamwua.[#1 Fal. 13:24.]
37Alipoona mtu mwingine akamwambia: Nipige! Yule mtu akampiga sana na kumtia kidonda.
38Kisha huyu mfumbuaji akaja kusimama njiani, mfalme alipotaka kupitia, lakini alikuwa amejigeuza, asijulikane, kwa kufunga kitambaa machoni pake.
39Ikawa, mfalme alipopita, yeye akamlilia mfalme akisema: Mtumishi wako alikuwa amekwenda penye yale mapigano; mara mwenzangu aliyekuwa ameondoka akaniletea mtu, akaniambia: Mwangalie mtu huyu! Atakapopotea, mwenyewe utaingia mahali pake au utajikomboa kwa kulipa kipande cha fedha, ndio shilingi 12000.[#2 Fal. 10:24.]
40Basi, mtumishi wako alipokuwa anafanya hivi na hivi, mara yule mtu alikuwa hayuko. Mfalme wa Waisiraeli akamwambia: Basi, shauri lako ni lilelile, ulilojikatia mwenyewe!
41Ndipo, alipokiondoa upesi kile kitambaa machoni pake, naye mfalme wa Waisiraeli akamtambua, ya kuwa ni mmoja wao wafumbuaji.
42Naye akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtu, mimi niliyemtoa, aangamizwe, wewe umemwacha, aponyoke mikononi mwako, kwa sababu hii roho yako itakuwa mahali pake, nao wa ukoo wako watakuwa mahali pao wa ukoo wake.
43Kisha mfalme wa Waisiraeli akaenda nyumbani kwake mwenye moyo uliokasirika na kuchafuka, akafika Samaria.